Ndoto za Kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii tiba nchini zinaendelea kutimia ambapo safari hii Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Mloganzila imeandaa kambi ya siku tano ya upasuaji rekebishi wa macho.

Kambi hiyo inatarajiwa kuanza Machi 11 hadi 15, katika Hospitali ya Mlonganzila jijini Dar es Salaam.

Akizungumza  leo Msemaji wa Global Medicare ambao ndiyo waratibu wa kambi hiyo ya matibabu maalum ya macho, Albert Kilalah, amesema kambi hiyo inawahusu watu wenye makengeza, kope zinazoshindwa kufunguka na wenye makovu ya ajali.

Amesema Kambi hiyo itaendeshwa na madaktari bobezi kutoka nje ya nchi ambao ni Dk Nabila Elias na Dk. Safwat El badri kutoka Dubai.

 “Wenye changamoto  zilizotajwa hapo juu wakipata taarifa hizi wafike Mlonganzila kwaajili ya kufanyiwa vipimo vya awali kabla ya kuanza kwa kambi hiyo siku ya Jumatatu tarehe 11 hii ni fursa nzuri ya kukutana na madaktaari bingwa kwa hiyo waitumie ,” amesema

Amesema madaktari hao bingwa watashirikiana na madaktari bingwa wazawa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Mlonganzila.

Amesema ili kubakiza ujuzi huo hapa nchini wamealikwa madaktari kutoka hospitali za Benjamin Mkapa Dodoma, Hospitali ya Kanda Mbeya, Bugando Mwanza, Tumbi Kibaha, Hospitali ya Mtwara RRH  pamoja na CCBRT ya Msasani Dar es Salaam.

“Hawa madaktari wazawa watashirikiana na hawa madaktari bingwa kutoka Dubai kufanya upasuaji huu fursa ambayo wataitumia kama sehemu ya kujifunza ili wageni watakapoondoka wazawa wawe wanaendelea kufanya upasuaji wa aina hii,” amesema.

Amesema kambi hiyo inakuja kufuatia uwekezaji mkubwa wa vifaa tiba vilivyonunuliwa na serikali ya awamu ya sita samabamba na madaktari kusomeshwa kwa wingi na kupewa utaalamu wa hali ya juu kufanya matibabu ya kibingwa.

Amesema zamani matibabu kama hayo yalikuwa yakifanyika nje ya nchi lakini kutokana na uwekezaji huo matibabu hayo yanafanyika hapahapa nchini.

“Zamani wagonjwa kama hawa tuliwapeleka nje ya nchi, lakini sasa madaktati bingwa kutoka nje wanakuja kuwatibu wagonjwa wetu hapahapa kwasababu nchi ina kila aina ya vifaa tiba ambavyo tulikuwa tunalazimika kuvifuata  nje ya nchi na kwa sasa nchi ina madaktati bingwa wenye uwezo mkubwa wa kutumia vifaa hivyo,” amesema

“Haya yote ni matunda ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amefanya uwekezaji mkubwa na ambao anaendelea kuufanya kwenye sekta ya afya na huu umesababisha wagonjwa kutoka nje ya nchi hasa majirani kuja kupata huduma za bingwa hapa nchini ambazo awali walizifuata nje ya nchi,” amesema Kilalah.

Daktari bingwa wa macho wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Pwani Tumbi, Fadhili Swai, amesema anafurahi kuona wanakwenda kutoa huduma ambayo ni nadra sana kufanywa hapa nchini.

“Natoa rai kwa watanzania wazitumie siku hizo tano kwasababu hiyo ni huduma ya kipekee na adimu sana kutokea nchini. Wanapokuja madaktari bingwa kutoka nchi mbalimbali tunabadilishana ujuzi na mbinu za tiba kwa hiyo hii ni hatua muhimu sana kwetu,” alisema

Dakari bingwa wa macho wa Hospitali ya RRH Mtwara, Mganga Majura amesema ujio wa madaktari hao unakwenda kutambulisha hospitali za hapa nchini kimataifa kwani baadhi ya watanzania wakiwemo wageni hawajui uwekezaji mkubwa kwenye afya ya macho uliofanywa katika hospitali ya Muhimbili.

 “Hii ni fursa ya kutambulika duniani na tukiwa na madaktari hawa watalii wanaokuja nchini watakuwa na imani kwamba hata wakiugua macho watapata matibabu ya kitaalamu kama ambayo wangepata wakienda nchi zilizoendelea,” amesema.

Amesema kambi hiyo itawasaidia madaktari wa ndani na wale wageni kupeana mbinu mpya za tiba ya kibingwa ya macho na baadaye tiba kama hiyo kufanyika kwenye hospitali za mikoa mbalimbali bila kulazimika kuja Muhimbili.