Mnyika:Mfumo wa vyama vingi ulitolewa kama zawadi na CCM

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dar

Katibu Mkuu wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha (CHADEMA), John Mnyika amewataka Watanzania kuendelea kupigania katiba mpya kwa sababu ndiyo mkombozi.

Hayo ameyasema jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la maadhimisho ya siku ya kimataifa ya demokrasia ambayo lililowakutanisha wadau mbalimbali kujadili miaka 30 ya demokrasia ya Tanzania.

“Nawashauri Watanzania wenzangu tuendelee kupigania katiba mpya kwa sababu ndiyo mkombozi wetu naamini kama tutashirikiana pamoja katika kudai katiba yetu mpya tutafanikiwa,’ amesema.

Mnyika amesema kuwa katika mchakato ule wa mapendekezo ya katiba mpya Tume ya Nyalali ilipendeke za mabadiliko ya Katiba pamoja na sheria 40 ili ziendane na mazingira ya mfumo wa vyama vingi.

“Kama mapendekezo ya Tume ya Jaji Francis Nyalali yangefanyika baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, vyama vya upinzani vingefanya vizuri zaidi.

“Katika mabadiliko ya mapendekezo yale yangesaidia vyama vya uoinzani kufanya vizuri zaidi lakini watawala walikataa,” amesema Mnyika.

Amongeza kuwa watawala walikataa kutekeleza hilo kwa kuhofia kwamba wangepoteza dola hivyo ni vizuri sasa kwa Watanzania kuendelea kupigania katiba mpya kwa sababu ndiyo mkombozi,” amesema Mnyika ambaye mbunge wa zamani wa Jimbo la Kibamba.

Mnyika amesema kuwa Mapendekezo ya Tume ya Jaji Nyalali yangetekelezwa mwaka 1995, na kama katiba mpya ingeandikwa wakati ule, matokeo ya uchaguzi yasingekuwa vile yalivyokuwa.

“Huwezi ukasema nchi ina demokrasia wakati vyama haviwezi kufanya hata mikutano ya hadhara. Tunahitaji kujenga mifumo na taasisi imara,” alisema Mnyika.

“Mfumo wa vyama vingi ulitolewa kama zawadi na CCM. Wakati wowote mfumo wa vyama vingi unaweza kuondolewa kama ilivyokuwa mwaka 2020,” amesema Mnyika.