Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitaka Serikali kutoa sababu zilizosababisha Mfuko wa Taifa wa Bima (NHIF) kuwa na hali mbaya ya kifedha.

Hayo yamesemwa leo Septemba 20,2022 na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar, Salim Mwalimu alipokuwa akitoa taarifa ya maazimio ya kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Septemba 17 na 18, mwaka huu.

“Sio kutueleza kuwa hali mbaya pekee,tunataka taarifa ya sababu za kufikiwa kwa hali hiyo, kazi hii ifanywe na CAG,” amesema Mwalimu.

Aidha Mwalimu amesema kuhusu muswada wa Bima ya Afya kwa wote uliowasilishwa bungeni hivi karibuni, Mwalimu amesema Kamati Kuu imeitaka Serikali kutoa muda wa kutosha kwa wananchi kutoa maoni juu ya suala hilo.

“Kamati Kuu imeitaka Serikali kutoa muda wa kutosha kwa wananchi kuijadili Sheria Mpya ya Bima ya Afya kwa wote badala ya kutumia utaratibu wa Hati ya Dharura kuwasilisha Muswada Bungeni. Serikali itumie utaratibu wa kawaida katika kutunga sheria hiyo” amesema Mwalimu.

Kamati Kuu inamtaka Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalum kwenye mfuko wa Bima ya Afya nchini na kutoa taarifa yake kwa umma kuhusu mwenendo wa hali ya fedha za wanachama wa mfuko huo ikiwa ni pamoja na madeni yake.

Pia Kamati Kuu imeitaka Serikali kupunguza msururu wa Kodi na Tozo kwenye Mafuta ili kupunguza bei kubwa ya mafuta nchini.

Kamati Kuu imeitaka Serikali kuja na mpango madhubuti wa uhakika wa upatikanaji wa chakula na kuthibiti kasi ya ukuaji wa bei za chakula nchini.”

Mwalimu amesema kuwa Kamati Kuu ilikuwa na ajenda kadhaa zikiwemo kupokea na kuijadili taarifa ya hali ya siasa na uchumi nchini, pia ilihusisha taarifa ya hali ya siasa Zanzibar,mwenendo wa mazungumzo ya Maridhiano baina ya Chadema, CCM na Serikali, Bajeti ya Serikali ya mwaka 2022/23 na …

“‘Madhara yake kwa wananchi, hatari ya Mfuko wa Bima ya Afya kufilisika na kutungwa Kwa sheria Mpya ya bima ya Afya kwa wote. Hali ya upatikanaji na bei kubwa ya chakula nchini. Bei kubwa ya mafuta na bidhaa nyinginezo kadhaa.” amesema

By Jamhuri