Mfanyabiashra Mohamed Dewji ‘Mo’ ameendelea kung’ang’ania kwenye orodha ya matajiri Barani Afrika iliyotolewa na Jarida maarufu la Forbes, ambapo ameshika nafasi ya 13 huku maarufu Aliko Dangote akishika nafasi ya kwanza.

Katika orodha hiyo iliyotolewa na jarida la Forbes linalofuatilia utajiri wa watu, mwaka huu limemtaja Mo (47) kuwa bilionea wa 13, akitoka nafasi ya 15 mwaka jana.
Kwa mujibu wa jarida hilo, Mohammed Dewji mwenye utajiri wa Dola za kimarekani bilioni1.5 ambazo ni sawa na Sh3.5 trilioni amefungana na bilionea Youssef Mansour kutoka Misri na Aziz Akhannouch kutoka Morocco wote wakiwa na utajiri wa Dola za kimarekani Bilioni 1.5.

Dewji, anayefanya biashara mchanganyiko ambaye mara kadhaa ameahidi kuwa lengo lake ni kuajiri watu 100,000 hivi sasa ameongeza ajira hadi kufikia 35,000 kutoka 28,000.
Mo mara kwa mara ndiye anayeliwakilisha taifa kila orodha hiyo ikitolewa na jarida la Forbes.

Tajiri mwingine kutoka Afrika Kusini Johann Rupert (72) ndiye anaeshikilia nafasi ya pili kwa mwaka wa pili mfululizo katika orodha hii nchi za Afrika Kusini, Nigeria na Misri zimeonekana zikitawala.

Dewji mwenye umri wa miaka 47, ni tajiri pekee kutoka Afrika Mashariki na Kati kwenye orodha iliyotajwa na Jarida la Forbes na pia ndiye kijana pekee kwenye orodha hiyo yenye mabilionea waliozidi zaidi ya miaka 60.

Mfanyabiashara wa viwanda wa Nigeria Aliko Dangote, mwenye utajiri wa dola bilioni 13.5, ndiye mtu tajiri zaidi kwa mwaka wa 12 mfululizo akiongoza barani Afrika akiendelea kuwabwaga wenzie bila huruma.

Nafasi ya mwisho imeshikwa na Bilionea Christoffel Wiese (81) mwenye utajiri wa dola za kimarekani bilioni 1.1 kutoka nchini Afrika Kusini yeye ndiye akifunga dimba.

Kuendelea kung’ara kwa Mo licha ya changamoto ya Uviko-19 na vita vya Russia na Ukraine ni kuonyesha namna mfanyabiashara huo alivyoweka misingi madhubuti katika biashara zake zilizopo ndani na nje ya nchi.

By Jamhuri