*Mgonjwa hupona kwa muda mfupi 

*Bima ya Afya ni suluhu upatikanaji huduma za kibingwa  

DAR ES SALAAM

Na Aziza Nangwa

Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) imepiga hatua nyingine kwenye maboresho ya miundombinu na vifaa vya kisasa katika upasuaji wa ubongo kupitia njia ya pua.

Kuthibitisha hili, JAMHURI limewatembelea kujionea maboresho ya miundombinu na vifaa vya kisasa vya upasuaji wa ubongo kupitia njia ya pua.

Mkurugenzi wa MOI, Dk. Respicious Boniface, anasema upasuaji wa kisasa kwa kutumia njia ya pua umewezekana kutokana na uwekezaji mkubwa wa serikali katika sekta ya afya.

Anasema uwekezaji uliopo kwa sasa umekwenda sanjali na uboreshaji wa vifaa vya kisasa na kuweka wataalamu waliobobea ili kusaidia utoaji wa huduma za kibingwa kwa njia ya kisasa.

“Lengo la serikali ni kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi na jamii iweze kupata huduma bora na za kisasa hapa hapa nchini, kwa gharama nafuu kupitia Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) sambamba na uongezaji wataalamu wa ndani badala ya kuwatoa nje ya nchi,” anasema Dk. Boniface.

Dk. Boniface anasema utendaji kazi wa  mashine ya upasuaji ubongo kwa kutumia  ‘microscope’ ya kisasa kupitia kwenye mashimo ya pua ni salama kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo nchini kwa sasa kutokana na kufanyika kidijitali zaidi.

“Mikakati yetu ni kuongeza idadi ya wataalamu wabobezi wenye utaalamu kwa sasa kwenye baadhi ya hospitali za kanda, wapunguze idadi ya wagonjwa wanaosafiri kutoka mikoani kuja MOI kupata huduma za kibingwa,” anasema Mkurugenzi wa MOI. 

Utoaji wa mafunzo ya watalaamu wa utoaji huduma za kibingwa katika kanda utarahisisha kutokuwapo kwa msongamano wa wagonjwa wanaohitaji huduma za kibingwa katika hospitali hizo kwa sababu wagonjwa watakuwa wachache. 

Laurent Lemery ni daktari bingwa wa kitengo cha matibabu ya ubongo kupitia mashimo ya pua, anasema upasuaji huo ni salama na wa kisasa, kwa sababu mgonjwa hatumii muda mrefu kupona tofauti na njia ya kufungua fuvu.

Dk. Lemery anasema upasuaji wa fuvu kwa kupitia njia ya mashino ya pua uko kwa ajili ya wagonjwa maalumu wenye uhitaji na wanafanyiwa vipimo kabla ili kuhakikisha wanapata huduma iliyo salama kwao. 

“Upasuaji wa ubongo kwa njia ya pua mara nyingi umekuwa na mafanikio makubwa kwani mgonjwa hutumia muda mfupi kukaa hospitalini tofauti na njia nyingine zilizokuwa zikitumia miaka ya nyuma kufanya kazi hiyo,” anasema.

Dk. Lemery anasema njia hii mgonjwa akifanyiwa hahitaji kupumua kwa kutumia mashine baada ya kumaliza, kwani anarejea katika hali yake kwa muda mfupi kuliko akitibiwa kwa kufungua fuvu. 

Kabla ya kufanyika kwa upasuji kunakuwa na vipimo kwa kupitia ‘microscope’ vinavyomsaidia mtaalamu kuona hali halisi ya tatizo lililopo kwenye ubongo ndani, na hapo kuna kifaa maalumu ambacho kitafanya kazi ya kutoa uvimbe na kuutoa nje au kuweka dawa ya kutibu eneo husika.

“Hii operesheni huko nyuma ilikuwa haifanyiki mara kwa mara nchini kutokana na uhaba wa vifaa uliokuwepo, lakini ilipofika mwaka 2017 taasisi ilinunua vifaa vya kisasa na kuongeza wataalamu hivyo kurudisha huduma ya upasuaji kwa njia ya pua,” anasema Dk. Lemery. 

Huduma hiyo huhitaji vifaa vya kisasa na wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu watakaotumia teknolojia kwa umakini na kutoa mafanikio chanya yaliyokusudiwa kwa wagonjwa.

“Mara nyingi upasuaji huo hufanyiwa wagonjwa wenye mahitaji maalumu; hasa wenye vivimbe ndani chini ya uvungu wa ubongo. Tunapitia matundu ya pua kutoa vivimbe hivyo,” anasema Dk. Lemery na kuongeza:

“Katika operesheni hii hatutumii sehemu yoyote kupasua, zaidi ya puani. tunapitisha vifaa maalumu kwa kushirikiana na ‘microscope’ mpaka tunafika kwenye mfupa unaotenganisha ubongo na mapango ya nyuma ya pua.

“Baada ya uvimbe kutolewa nje vile vifaa vilivyotumika awali kufanya upasuaji ndivyo hivyo hivyo vinatumika katika kufunga zile njia zilizotumika kupita na kuzirudisha upya kwa kushikilia kwa gundi maalumu.”

Anasema kila wiki mgonjwa mmoja hufanyiwa upasuaji MOI.

Dk. Mechris Mango, mtaalamu mbobezi wa mashine hiyo, anasema upasuaji wa ubongo kupitia pua kitaalamu huitwa ‘transsphenoidal surgery’.

“Upasuaji huu hufanyika baada ya kujiridhisha katika vipimo, ramani ya pua ya mgonjwa imekaaje. Upasuaji huu ni rahisi na salama kuliko upasuaji mwingine wa kufika katika ubongo, kuliko njia nyingine tulizozoea,” anasema Mango.

Anasema kabla ya upasuaji yeye kama mtaalamu anahakikisha kunakuwapo na microscope maalumu itakayotumika na daktari ipo salama, na imeunganishwa na screen ya kompyuta ili kuratibu shughuli nzima inapofanyika.

Microscope ya upasuaji huu imeundwa kitaalamu zaidi na vifaa vyake ni vya  kisasa, kwa sababu inamwezesha daktari kufika eneo la tukio na kuona ugonjwa, mwishowe kuanza matibabu yenyewe na kutoa uvimbe uliopo nje kwa kutumia vifaa maalumu vilivyopo kwenye mashine hiyo kwa sasa.

559 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!