Timu ya Taifa ya Morocco wameuungana na Senegal katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Dunia nchini Qatar baada ya kuicharaza Canada kwa mabao 2-1 na kuwafanya kuongoza kundi lao wakiwa na point 7 huku wakifuatiwa na Croatia wenye point 5.

Wanyonge katika kundi hilo ni Ubelgiji na Canada ambao wameiaga rasmi michuano hiyo na kurejea nyumbani. Mshangao mkubwa ni kwa Ubelgiji ambao wapo ukingoni mwa kizazi chao cha dhahabu ambacho kilitarajiwa kufanya makubwa katika michuano mikubwa kama hii ya Kombe la Dunia na Euro lakini mambo yamewagomea. 

8

Baada ya ushindi huo, Morocco wamevunja rekodi mbalimbali kama ifuatavyo:

Timu ya Taifa ya Morocco ni timu ya kwanza Afrika kuvuna point 7 katika Michuano ya Kombe la Dunia hatua ya makundi. 

Morocco wamefuzu kwenda hatua ya 16 Bora katika Michuano ya Kombe la Dunia kwa mara ya pili toka michuano hiyo ianzishwe na mara ya mwisho walifuzu kwenda hatua hiyo miaka 36 (1986) iliyopita ambapo waliongoza kundi lao pia.

Kocha wa timu ya taifa ya Morocco, Walid Regragui (47), hajapoteza mechi yeyote toka alipokabidhiwa kazi ya kuinoa Morocco ambao wamefuzu kwenda hatua ya 16 Bora wakiwa ndio vinara wa kundi F lenye timu za Ubelgiji, Canada, Croatia na wao Morocco.

Mei 30 mwaka huu kocha wa Morocco, Walid Regragui,  aliiongoza Wydad Casablanca kutwaa taji la CAF Champions League na Jana Desemba mosi amekuwa kocha wa kwanza kabisa kuiongoza timu ya Afrika kukusanya point 7 katika hatua ya makundi. 

Straika  Youssef En-Nesyri (25) ambaye anaitumikia Sevilla ya Hispania amekuwa mchezaji wa kwanza wa Morocco kufunga magoli katika michuano miwili tofauti ya Kombe la Dunia ikiwa ni mwaka 2018 na mwaka 2022. 

Aidha mchezaji huyo amefunga magoli katika michuano yote mitano ya kimataifa aliyoitumikia taifa hilo ambapo AFCON 2017 alifunga goli 1, Kombe la Dunia 2018 alifunga goli 1, AFCON 2019 alifunga goli 2, AFCON 2021 alifunga goli 1, Kombe la Dunia 2022 goli 1. 

Goli alilofunga mchezaji wa Morocco,  Hakim Ziyech, dakika ya 4 ya mchezo dhidi ya Canada linakuwa ndio goli la kwanza kwa mchezaji huyo kufunga katika Michuano ya Kombe la Dunia katika maisha yake ya soka.

Baada ya Morocco kuandikisha ushindi huo, nchi za Afrika zinavunja rekodi kwa kupata ushindi katika mechi 5 kwa awamu moja ya Michuano ya Kombe la Dunia huku rekodi kubwa ilikuwa ni kupata ushindi katika mechi 3 pekee. 

By Jamhuri