Nimemsikia mtu anailaumu Yanga kwanini walimuacha Saido na kumsajili Kisinda, kwanini hasemi walimuacha Saido na kumsajili Aziz Ki? Kwani Saido amejiunga na Simba akitokea Yanga au Geita Gold? Kwanini hawalaumiwi Geita kwa kumuacha Saido lakini inalaumiwa Yanga?

Walitaka Saido akijiunga na Simba asifanye vizuri? Binafsi nimefurahia Saido kutua Simba na kufanya vizuri. Yanga walimuacha kwa madai ya utovu wa nidhamu na mahitaji makubwa aliyoyataka kabla ya kusaini mkataba. Simba wamekubaliana na yote na kumpa mkataba.

Saido anailipa Simba kwa maamuzi yao ya kufumba macho na kutia pesa nzuri ya usajili na mahitaji mengine ya Saido. Kuhusu mambo ya kinidhamu Tujipe muda kuangalia ili akiishi vizuri na Simba bila hayo matatizo ya kinidhamu tuinyooshe kidole Yanga na kuwaambia Saido hana tatizo la kinidhamu ila ninyi ndio mlishindwa namna ya kuishi naye. 

Usajili wa Saido kwenda Simba unafanana tu na ule wa Morrison kurejea Yanga ingawa Saido alipita Geita Gold kabla ya kutua Simba, Simba walimuacha Morrison sababu ya matatizo ya kinidhamu na tukajipa muda tuone huko Yanga watamudu kukaa naye kwa utulivu lakini tayari tumeshaona Morrison ni mchezaji anayeongoza kwa matatizo ya kifamilia Kila siku. 

Saido alipokuwa Geita Gold alikuwa katika mawindo ya timu kubwa kwa hiyo sio rahisi kuhukumu kuhusu nidhamu yake kule. Alificha makucha alikubali kushusha mahitaji ya usajili na mshahara ili atue Geita Gold kuonesha nini bado anaweza na hatimaye ametua Simba. Ametua kwa kishindo, amepiga hat trick na assist moja katika mechi yake ya kwanza tu hapo jana.

 

Tuendelee kumtamkia mema, kwani tulitaka aende wapi ili tuwe na amani? Ilikuwa muhimu abaki Tanzania tena katika timu kubwa inayokubaliana na mahitaji yake ili tuone soka bora zaidi. Tulitaka asifanye vizuri akitua Simba ili tuseme Yanga walikuwa sahihi? Huo sio uchambuzi ni uganga na ugawa laana. 

Kama hoja hizi za Yanga ‘kumuacha Saido na kumsajili Kisinda’ zingekuwa zina mantiki basi zingesemwa toka mwanzo wa msimu. Ndio zingesemwa walau Saido alipojiunga tu na Simba lakini kuzisema baada ya Saido kufanya vizuri ni ishara ya kwamba wachambuzi wale walitarajia akitua Simba hatafanya vizuri na ndio maana baada ya kufanya vizuri ndio wameibuka na kuilaumu Yanga kumuacha Saido na hawailaumu Geita Gold.