Na Edward Kondela, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mradi wa kuwawezesha wanawake katika mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi kwa nchi za Afrika Mashariki kupitia Ziwa Victoria umezinduliwa ili kumuwezesha mwanamke kuongeza kipato kupita kupitia mazao hayo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Machi 23, 2024 wakati wa kufunga mafunzo ya siku tatu ya Mtandao wa Wanawake Afrika Wanaojishughulisha na Uchakataji na Biashara ya Samaki (AWFISHNET), uliohusisha wanawake ambao ni viongozi wa mtandao huo kutoka takriban nchi 44 za Afrika, Mkurugenzi wa mradi huo Bi. Suzanne Njeri amesema utatekelezwa katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Afisa Uvuvi Mkuu Bi. Jovice Mkuchu akikata keki na Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Afrika la Rasilimali za Wanyama (AU-IBAR), Bi. Patricia Lumba (kulia), wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi wa kuwawezesha wanawake katika mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi kwa nchi za Afrika Mashariki kupitia Ziwa Victoria. Hafla hiyo fupi imefanyika jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha Mtandao wa Wanawake Afrika Wanaojishughulisha na Uchakataji na Biashara ya Samaki (AWFISHNET). (23.03.2024)

Bi. Njeri ameongeza kuwa mradi huo wa majaribio utatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili na nusu na mpango ni kuwafikia wanawake 5,000 Afrika Mashariki, ambapo kwa kila nchi watakuwa wanawake 1,667.

Amefafanua kuwa mradi huo utakuwa na mambo mbalimbali ya kumuwezesha mwanamke lakini kubwa zaidi ni kumuinua mwanamke kuanzia pale alipo ili aweze kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi.

Akiiwakilisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika hafla hiyo, Afisa Uvuvi Mkuu Bi. Jovice Mkuchu amesema wizara imeweza kufanya tathmini mbalimbali kwenye Sekta ya Uvuvi, ambapo mradi unaenda kutatua changamoto za wanawake katika kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi tangu yanapovuliwa.

Mkurugenzi wa mradi wa kuwawezesha wanawake katika mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi kwa nchi za Afrika Mashariki kupitia Ziwa Victoria Bi. Suzanne Njeri akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi huo utakaotekelezwa katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, kwenye kikao cha Mtandao wa Wanawake Afrika Wanaojishughulisha na Uchakataji na Biashara ya Samaki (AWFISHNET). (23.03.2024)

Aidha, amesema wizara inashukuru uwepo wa mradi huo ambao umeona umuhimu wa kuwainua wanawake wa Tanzania katika Sekta ya Uvuvi kwa kuwa wizara ni mlezi wa mtandao wa Wanawake Wanaojishughulisha na Uvuvi Tanzania (TAWFA) na kwamba wizara itakuwa bega kwa bega kuwezesha mradi huo kuwa na tija.

Naye Bi. Editrudith Lukanga ambaye ni Mshauri Mkuu Elekezi wa mradi huo, amesema mradi unafadhiliwa na taasisi ya Bill and Melinda Gates kwa thamani ya takriban Dola za Kimarekani Milioni 1.5 na utakuwa wezeshi kwa kuwa umewashirikisha wadau kuanzia ngazi ya chini.

Amesema katika tafiti walizofanya kwenye mialo mbalimbali wamebaini wanawake wamechukulia zao la samaki kama biashara huku wakiwa na upungufu mkubwa wa wao wenyewe katika ulaji wa samaki na kukimbilia kuuza na kupata fedha ili wanunue chakula kingine au kununua mahitaji mengine ya familia.

Ameongeza kuwa kumekuwa pia na changamoto ya upatikanaji wa rasilimali fedha kama mtaji ili kuwasaidia wanawake kununua bidhaa kwa kiwango kikubwa ili kukidhi ushindani sokoni.

Pia, ametaja upotevu wa samaki kabla ya kuwafikisha sokoni baada ya kuvuliwa imekuwa ni changamoto kwa wanawake.

Mshauri Mkuu Elekezi wa mradi wa kuwawezesha wanawake katika mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi Bi. Editrudith Lukanga, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo jijini Dar es Salaam, ambapo amesema mradi unafadhiliwa na taasisi ya Bill and Melinda Gates kwa thamani ya takriban Dola za Kimarekani Milioni 1.5 na utakuwa wezeshi kwa kuwa umewashirikisha wadau kuanzia ngazi ya chini. (23.03.2024)

Ili kutatua changamto hizo amebainisha kuwa lengo kubwa kabisa katika mradi ni kuwezesha wanawake katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya uvuvi pamoja na viumbe maji vingine vinavyofugwa majini ili kuwezesha kubadilisha hali ya maisha yao.

Mradi wa kuwawezesha wanawake katika mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi katika nchi za Afrika Mashariki kwa sasa unatekelezwa kupitia Ziwa Victoria, lengo likiwa ni kufikia maeneo mengine ya bara la Afrika ambayo yana maji ya asili ikiwemo bahari na maziwa.

Washiriki wa kikao cha Mtandao wa Wanawake Afrika Wanaojishughulisha na Uchakataji na Biashara ya Samaki (AWFISHNET) kilichofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salaam, wakisikiliza hoja mbalimbali juu ya manufaa ya mradi wa kuwawezesha wanawake katika mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi kwa nchi za Afrika Mashariki kupitia Ziwa Victoria ambao unalenga kuwafikia wanawake 5,000.