Na Mwandisho Wetu, JamhuriMedia,

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema tayari mtambo namba nane kutoka kwenye Mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere umekamilika na sasa unaingiza megawati 235 kwenye gridi ya taifa.

Dkt Biteko ametoa taarifa hiyo tarehe 14 juni 2024 wakati akizindua taarifa za utendaji katika Sekta ndogo ya Umeme, Gesi Asilia na Mafuta kwa mwaka 2022/2023 jijini Dodoma ambapo amesema kwa sasa Jumla ya megawati 470 zinazalishwa kutoka JNHPP na tayari zimeingizwa kwenye gridi ya taifa.

Kuhusu sekta binafsi amesema, “Sekta binafsi imetutoa kimasomaso, Serikali haiwezi kufanya kila kitu, wamefanya kazi kubwa mno kwenye mafuta, gesi na hata kwenye uzalishaji umeme, wito wangu kwenu msibaki nyuma changamkieni fursa, na kwa taasisi zilizo chini ya Wizara msione sekta binafsi kama watu wajanjawajanja, tuwape kipaumbele.” amesema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa katika tathmini iliyozinduliwa inaonesha Sekta ya Nishati imepiga hatua kwenye maeneo mengi ikiwemo uhakika wa upatikanaji umeme, upatikanaji na usambazaji wa mafuta kuimarika hasa baada ya Mhe. Dkt. Doto Biteko kuanza kuongoza Wizara ya Nishati.

Ameongeza kuwa, taarifa ya Benki ya Dunia kwa nchi za Dunia ya Tatu zinazofadhiliwa na Benki hiyo inaonesha kuwa Sekta ya Nishati kwa Tanzania inafanya vizuri zaidi katika nchi zote zinazoendelea na Bara la Afrika kwa ujumla na hii ni matunda ya usimamizi madhubuti wa Mhe.Dkt. Doto Biteko ambapo eneo lililofanya vizuri zaidi ni usambazaji umeme vijijini na miradi mingine ya nishati kama JNHPP na mradi wa TAZA.

Ameongeza kuwa Benki ya Dunia imeidhinisha Dola.za Marekani milioni 300 ili ziendeleze sekta ya umeme kutokana na ufanisi huo wa Tanzania.

Akitoa taarifa za utendaji katika Sekta ya Nishati, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dkt. James Andilile alisema kuwa Sekta ya Nishati inaendelea kuimarika ikiwemo uwekezaji kwenye miundombinu ya umeme uwekezaji umeongezeka katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji, upotevu wa umeme unazidi kupungua na kubainisha wateja wa umeme wameongezeka kutoka milioni 3.8 mwaka 2021/22 hadi milioni 4.4 mwaka 2022/2023.

Kwa upande wa changamoto zilizoainishwa kwenye taarifa hiyo katika sekta ya umeme ni uchakavu wa miundombinu ambao bado unaendelea kufanyiwa kazi kwa ukarabati wa miundombinu na uwekezaji endelevu.