Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika na (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama, amesema mradi wa Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba, pamoja na Miradi mingine ya kimkakati imeleta ajira na kuchangia kasi na chachu ya ukuaji wa uchumi hususan katika Jiji la Dodoma.

Ameyasema hayo Agosti 3, 2023, alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua ujenzi wa Jengo la Mpigachapa Mkuu wa Serikali; Jengo la Kituo cha Taifa cha Usimamizi na Uratibu wa Maafa, Jengo la Wizara Mipango na Uwekezaji, na jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu).

Waziri Mhagama alisema kuwa, ujenzi wa Mradi hiyo mikubwa ya kimkakati inayoendelea umewezesha vijana wengi kupata ajira katika maeneo hayo, na kujiongezea pato binafsi sambamba na kuchangia ukuajia wa uchumi kutokana na manunuzi ya bidhaa zinazotumika katika mradi hiyo kufanyika katika viwanda vilivyopo nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akipokea taarifa ya ujenzi wa jengo la kiwanda cha Mpiga chapa wa Serikali katika ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Miundo mbinu katika idara zilizo chini ya Ofisi yake.

Alipokuwa katika jengo la Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Waziri Mhagama alisema kuwa mradi huo, mkubwa umefikia asilimia tisini na saba (97%) ambapo kiwanda hicho kitakapokamilika kitakuwa na hadhi na sifa ya kuwa ni kiwanda kikubwa kimojawapo cha Serikali,ambapo mashine mpya zimeagizwa na kiwanda hicho kitafanya kazi za ndani ya nje na nchi za Afrika Mashariki (EAC) pamoja na ukanda wa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

“Sisi tumejipanga kwa matumizi ya ndani na nje pia, nimefarijika kuona ujenzi kwa awamu, hii ya kwanza umefikia hatua kubwa, na ujenzi wa Ofisi umeanza na unaenda kwa kasi.” amesisitiza Waziri Mhagama.

Alipokuwa katika kituo cha Taifa cha Uratibu na Usimamizi wa Maafa Mhe. Mhagama alisema, ujenzi wa awamu ya kwanza ya kituo hicho pia umekamilika kwa Asilimia tisini na nne (94%) na kufafanua kuwa maghala mawili makubwa na Ofisi za Watumishi zimeshakamilika.

“Tunalo jukumu la kuhakikisha kwamba katika kituo hicho nchi inafikia malengo ya kitaifa na Maono na maelekezo ya Mhe. Rais, Dkt, Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa Ujumla” amebainisha Waziri Mhagama.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akipokea taarifa ya ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi na Uratibu wa Maafa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Miundo mbinu katika idara zilizo chini ya Ofisi yake.

Waziri Mhagama Alisema kuwa katika kituo hicho cha Maafa kutakuwa na vitu vingine vingi ambavyo vinajenga dhana nzima ya uratibu na usimamizi wa Maafa, ambapo kutakuwa na kiwanja ambacho, kitakuwa kinasaidia utuaji na uondokaji wa Helkopta ambazo zitaweza kwenda kwenye shughuli za maafa, kutakuwa na kituo cha tiba kitakachosaidia dharura za maafa hasa katika magonjwa ya milipuko na kitatumika pia katika masuala ya utafiti na tiba na kituo cha mafunzo kwa wataalam ambao watashughulika na usimamizi na uratibu huo wa dharura.

Waziri Mhagama pia alitembelea na kukagua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) pamoja na Jengo la Wizara ya Mipango na uwekezaji katika Mji wa Serikali Mtumba, na kuagiza kuongezeka kwa kazi ya ujenzi ili majengo hayo yaweze kukabidhiwa kwa wakati.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi Hiyo Bw. Anderson Mutatembwa, alisema Ofisi hiyo itasimamia kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Mhagama, ikiwa ni pamoja na kuzifanyia kazi chagamoto zilizojitokeza na kuhakikisha zinatatuliwa kwa wakati.

Awali akizungumza katika ziara hiyo, Mwakilishi na Msimamizi Mkuu wa miradi ya Ujenzi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi Mhandisi Anania Saudeni, Alikiri kuyapokea maagizo ya Mhe. Waziri Mhagama na kuyatekeleza kwa wakati, kimkataba na kukamilika katika ubora kulingana na maelekezo na kuhakikisha kazi zinafanyika usiku na Mchana na kuongeza nguvu kazi ya kutosha na usimamizi madhubuti.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama akipokea taarifa ya ujenzi wa Jengo la Wizara ya Mipango na Uwekezaji katika ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Miundo katika Mji wa Serikali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama akipokea taarifa ya ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) katika ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Miundo katika Mji wa Serikali.

By Jamhuri