Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameeleza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na MAendeleo, Freeman Mbowe na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema wanamuonea wivu Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa kwa kupata nafasi ya kuongea na Rais Dkt Magufuli.

Mrisho Gambo amesema hayo baada ya viongozi hao pamoja na wengine wengi kuibuka kuikosoa hatu ya Lowassa kufanya mazungumzo na kumsifia Rais Magufuli.

Gambo amesema kuwa wanaokosoa hatia hiyo iliyofanywa na Lowassa ni kwa sababu ya wivu na kwa kuwa hawajapata bahati hiyo ya kuonana na Rais Magufuli ili kuzungumza nae huku akiwataka kufuata hatua stahiki kama wanataka kuonana na Rais.

“Lowassa alikuwa na kiu ya muda mrefu kutaka kumuona Rais hatimaye Rais amemaliza kiu hiyo. Mbowe na Lema nao kama watu wenye akili timamu bila shaka nao wanayo kiu ya kuonana na kiongozi mkuu wa nchi, hivyo niwatake wafuate taratibu na kama Rais atakuwa na nafasi ataonana nao hana shida katika hilo,” amesema Gambo.

Jana Jumanne, Januari 9, Waziri mkuu Mstaafu alipata nafasi ya kuonana na Rais Dkt Magufuli, ambapo walizungumza mengi ikiwa ni pamoja na Lowassa kumpongeza Rais kwa kuwezesha elimu bure na kuleta maendeleo na ajira kwa vijana.

Hatua hiyo ilipelekea viongozi wakubwa wa CHADEMA pamoja na wadau wengine mbalimbali kuikosoa hatua hiyo, kwamba Lowassa hakupaswa kumsifia Rais bali kumkosoa kwa mambo yanayoendelea nchini.

Please follow and like us:
Pin Share