Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Ofisi ya Msajili wa Hazina imeanza kutekeleza mageuzi katika muundo na utaratibu wa kusimamia mashirika na taasisi za umma hususani katika kuajiri na kufukuza watendaji wakuu wa mashirika hayo.

Pia, serikali imetekeleza utaratibu wa kufuta na kuvunja baadhi ya taasisi na mashirika ya umma yaliyopo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina nchini.

Kwa mujibu wa tangazo la ajira lililotolewa na Ofisi ya Msajili wa Hazina katika Gazeti la Serikali la Daily News, msajili ametangaza nafasi za ujumbe wa bodi katika mashirika ya umma waliobobea katika maeneo matano.

Tangazo hilo limetaja maeneo hayo kuwa ni mafuta na gesi, uchimbaji na utafiti wa madini, nishati na huduma, taasisi za fedha na utalii na ukarimu.

Aidha, Ofisi ya Msajili imeuhakikishia umma kuwa itatenda haki katika kuchagua wale wenye sifa na waliotimiza vigezo kisheria na kwa mujibu wa taratibu zinazosimamia shirika fulani.

Mwishoni mwa mwaka jana, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu alitangaza mageuzi makubwa katika muundo na utaratibu wa kusimamia mashirika na taasisi za umma hususani katika kuajiri na kufukuza watendaji wakuu wa mashirika hayo.

Mchechu alisema pamoja na mambo mengine imependekeza kuanza utaratibu wa kuajiri na kufukuza watendaji wakuu wa mashirika hayo.

Mchechu alisema utaratibu huo waliukopa kutoka baadhi ya nchi kama China ambayo walijifunza namna inavyofanya katika kushughulika na mashirika ya umma.

Aliongeza kuwa katika majukumu yanayotekelezwa na mataifa waliyoyatumia kama kielelezo, utaratibu wa kuteua na kuwaondoa watendaji wakuu wa mashirika, ni kipengele ambacho hakikuwa kikitekelezwa Tanzania.

By Jamhuri