Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Msalala

MBUNGE wa Jimbo la Msalala, Kahama mkoani Shinyanga, Alhaj Idd Kassimu Idd (CCM) ametamba kwamba, fedha za miradi ya maendeleo zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, zimeibeba halmashauri hiyo.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa maendeleo kilichoitishwa na mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Khamis Katimba, Alhaj Idd alisema, Rais Samia ameitunuku halmashauri hiyo fedha nyingi za maendeleo kuliko halmashauri zingine za mkoa huo.

Na kwamba, hatua hiyo imewezesha miradi mingi ya kimkakati kwenye Halamshauri ya Msalala kusimamiwa na kukamilika kwa kiwango kinachoridhisha.

“Halmashauri ya Msalala ni miongoni mwa halmashauri zilizopokea fedha zote za kutekeleza miradi ya maendeleo kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ni halmashauri ya kwanza kupata fedha nyingi mkoani Shinyanga na ndio maana imefanya makubwa kwenye miradi yake chini ya usimamizi mzuri wa mkurugenzi wetu,” alisema.

Alitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kupitia fedha hizo kuwa ni ujenzi wa vituo vya afya katika Kata za Isaka, Mwalugulu, Segese, Bulige, Mwanase ambapo zaidi ya Tsh. bilioni 2.5 zilitumika kukamilisha vituo hivyo.

Mkurugenzi Mtendaji Khamis Katimba akielezea dhumuni la kuitishwa kwa kikao Cha wadau kupitia mpango mkakati wa Halmashauri

“Halmashauri ya Msalala imekamilisha zahanati 24 ambazo sasa zinatoa huduma, hii yote ni jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano,” alimema mbunge huyo.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo (Katimba), aliwataka wadau walioshiriki kikao hicho kupitia na kurekebisha kasoro zilizopo kwenye mpango huo tangu ulipoanza kutekelezwa miaka mitatu iliyopita, ili uwe na matokeo chanya zaidi.

“Mpango huu ulianza kutumika miaka mitatu iliyopita na sasa tunauishi, hivyo wadau tunayo nafasi nzuri ya kuchangia ili tufike mwaka 2025/2026 tukiwa pamoja na serikali yetu.

“Lengo letu ni kuhakikisha tunajua halmashauri inafanya nini kwa sasa na inalenga kufanya nini baadaye, ninaamini mtindo huu unitasaidia mimi kama mkurugenzi na watendaji wenzangu kuona kasoro wakati wa utekelezaji na kuchukua hatua,” alisema Katimba.

Miongoni mwa malengo yaliyomo kwenye mpango mkakati huo ni pamoja na kuwezesha wananchi wa Msalala kufanya kilimo cha kibiashara, uchimbaji wenye faida, kuweka mazingira rafiki kwa wajasiriamali, halmashauri kutangaza fursa za uwekezaji pia utunzaji wa mazingira na afya za wananchi.

Baadhi ya wadau wa maendeleo wameitaka halmashauri hiyo kuboresha zaidi mazingira ya wawekezaji ili kuinua wananchi kwa kuwa, ina mazingira mazuri.

Kizito Mtendaji kutoka Kata ya Isaka ameiomba halmashauri kukaribisha wawekezaji kujenga maghala ya kuhifadhia mpunga na mashine za kukoboreshea mpunga.


Hakimu Dismas, Hakimu kutoka Mahakama ya Mwanzo ya Lunguya ameshauri halmashauri kupima maeneo yote yanayomilikiwa na serikali na hasa maeneo ya mahakama kutokana na kuwepo kwa mradi wa wa kimataifa wa kujenga mahakama.

“Hapa kigezo kikubwa ni ardhi iwe imepimwa, hivyo halmashauri iwezeshe suala hili sambamba na kuwezesha vitendea kazi kwa ofisi za watendaji wa kata/vijiji na kuyajengea uwezo mabaraza ya ardhi ya kata, kwani mabaraza haya yamekuwa yakiingilia shughuli zisizowahusu,” alisema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala, Mibako Mabubu aliwashukuru wadau wa maendeleo ya halmashauri kwa kujitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao kuhusu shughuli za halmashauri jiyo.

“Michango mliyoitoa nitahakikisha Mkurugenzi Mtendaji anafanyia kazi yeye na watumishi wote wa halmashauri sambamba na mimi kufanya kazi niliyoagizwa na madiwani,” alisema.