Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) imetambuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kama Mlipa Kodi Bora Mkoa wa Kikodi Temeke.

Akizungumza na JAMHURI ofisini kwake hivi karibuni, Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa MSD, Jackson Rogasian, anasena imetokana na ushirikiano mzuri miongoni mwa watumishi.

“Kwa TRA kututambua kama Mlipa Kodi Bora Mkoa wa Temeke ni heshima kubwa kwetu. Hadhi hii tuliyopewa inatufanya tuchape kazi kwa bidii na kuchangia maendeleo ya taifa.

“Siku zote MSD hufuata taratibu, sheria na kanuni zilizowekwa, ikiwa ni pamoja na zile za TRA. Tunafuata na kuzingatia sheria zote za kikodi kama Kodi ya Mapato (Income Tax), Kodi ya Zuio (Withholding Tax), Kodi ya Majengo, Kodi ya Watumishi (PAYE) na nyinginezo.

“Hatucheleweshi kodi kwa kuwa Bodi ya Wadhamini ya MSD mbali na majukumu mengine iliyonayo, imepewa jukumu la kufuatilia na kuhakikisha kuwa taasisi inakidhi viwango; kwamba tunafuata sheria zote pamoja na miongozo ya ndani,” amesema.

Rogasian anaamini kuwa Rais Dk. Samia anastahili pongezi kwa mafanikio ya MSD kwa sasa, kwa kuwa anaisaidia kwa kiasi kikubwa kifedha.

“Rais anathamini sana sekta ya afya na kwa kusaidiana na mlezi wetu, Ummy Mwalimu (Waziri wa Afya), wanahakikisha bidhaa zote zinazohitajika zinapatikana kwa kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba,” anasema.

Kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa MSD, Jackson Rogasian

Fedha zinazotolewa na Serikali kwa MSD kwa mwaka zimeongezeka kutoka Sh bilioni 30 miaka minane iliyopita hadi kufikia Sh bilioni 205 kwa sasa; hivyo kuongeza ufanisi kwenye mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini; huku kodi ikilipwa bila shaka yoyote.

“Katika mnyororo mzima wa ugavi wa bidhaa za afya unaofanywa na MSD, kila idara ina mchango wake. Mfano mimi ni mtu wa fedha, ili kuhakikisha mtu anayehitaji dawa huko mbali kabisa vijijini anapata kwa wakati, ni lazima nitoe fedha za malipo mbalimbali kwa wakati.

“Mimi hapa (mhasibu) nikichelewesha malipo, ni sawa na kusababisha kifo kwa Mtanzania (au Watanzania) anayeishi sehemu fulani kwa kukosa dawa inayohitajika kwa wakati huo,” amesema Rogasian.

Anasema MSD inatambua kuwa ili nchi yoyote iendelee ni lazima kila anayetakiwa kulipa kodi alipe, tena alipe kwa wakati kwa ajili ya maendeleo.

MSD ni taasisi ya umma inayofanya kazi na kampuni na taasisi nyingine kama Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Udhibiti na Ununuzi wa Umma (PPRA) na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), na kwa kufanya hivyo hulazimika kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo nchini.

Rogasian anasifu mwenendo wa mnyororo (usiokatika) wa ugavi wa bidhaa za afya nchini, akiweka wazi kuwa unafanikiwa zaidi kutokana na uwepo wa Mkurugenzi Mkuu ambaye ni mtaalamu katika eneo hilo, akisaidiana na watumishi wataalamu katika kada mbalimbsali wanaowezesha kushauriana katika kushughulikia mahitaji ya wateja kwa usahihi.