Mtambo wa kutibu magonjwa zaidi ya 10 wazinduliwa Muhimbili

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar

Hospitali ya ya Taifa Muhimbili leo imezindua mtambo unaotumia hewa tiba yenye mgandamizo ya oksijeni (Hyperbaric Medicine Treatment) ambao unatibu magonjwa zaidi ya 10 na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na ya pili Kusini mwa Jangwa la Sahara kutumia mtambao huo uliogharimu TZS. 250 Mil.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mtambo huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi amesema kupitia matibabu haya mgonjwa huingizwa kwenye kifaa maalumu na kupatiwa tiba kupitia hewa tiba ya oksijeni iliyogandamizwa kwa asilimia 100.

Ameyataja wagonjwa watakaonufaika kuwa ni wale wenye vidonda sugu ambavyo matibabu mengine yameshindikana kama wagonjwa wa sukari (diabetic foot), walioathirika na moshi baada ya kuungua na moto (carbon monoxide poisoning) na waliopata changamoto za upungufu wa oksijeni mwilini kama waliozama kwenye maji baharini n.k (decompression syndrome).

Prof. Janabi amesema wagonjwa wengine ni pamoja na walioungua na moto (acute thermal injury), wenye upungufu mkubwa wa damu ambao kwa njia moja au nyingine hawawezi kuongezewa damu (severe anemia), waliopata ajali na kupata majeraha mwilini yasiyopona (Crush injury, compartment syndrome and other acute traumatic ischemia) na wagonjwa wenye maambukizi kwenye mifupa isiyopona (Refractory osteomyelitis)

Ameongeza kuwa wagonjwa wengine waliopata mionzi na kusababisha sehemu zilizopata tiba mionzi kuathitika ikiwemo wenye saratani za koo, njia ya chakula na wale wenye tezi dume (delayed radiation injury both soft tissue and bony necrosis), waliofanyiwa upasuaji na kuwekewa/kupandikiziwa sehemu ya miili yao (compromised grafts and flaps), wenye changamoto ya kusikia ambao vipimo vimeshindwa kuonyesha tatizo (idiopathic sudden sensorineural loss), wenye tatizo la usaha kwenye ubongo (intracranial abscess), wenye changamoto ya oksijeni kwenye mishipa ya damu (arterial insufficiencies) na watoto wenye usonji (autisim).

Prof. Janabi ameishukuru Kampuni ya Sechrist ya nchini Marekani ambao ndio watengenezaji na ndiyo waliotoa msaada huo wenye thamani ya TZS. 250 Mil.

Amemshukuru Jaclyn Mackey pamoja na uongozi mzima wa Woundcare Education Partners, John Peters ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Undersea and Hyperbaric Medical Society ambao kwa nyakati tofauti kwa kipindi cha miaka miwili waliweza kutoa nafasi za mafunzo na kuwaidhinishwa madaktari watatu (Certified Hyperbaric Physician) pamoja na wauguzi watano (Certified Hyperbaric Nurses) ambao wataendelea kutumia mtambo huo kuhudumia wananchi.

Aidha, Prof. Janabi amemshukuru na Prof. Jay Buckley ambaye kupitia ushirikiano wake wa kitabibu na kitafiti kati ya Chuo Kikuu anachofanya kazi cha Dartmouth nchini Marekani na MUHAS alifanikisha upatikanaji wa mtambo huu.