Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu alimjulia hali Mchungaji Donald Lema ambaye amefanyiwa upasuaji mdogo wa moyo wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure – TAVI) katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI). Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Dkt. Peter Kisenge.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu alimjulia hali Mzee Kutbuddin Fakhryddin Taibali ambaye amefanyiwa upasuaji mdogo wa moyo wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure – TAVI). Upasuaji huo umefanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini katika kambi maalumu ya matibabu iliyofanywa na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Starcare ya nchini India.

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu akizungumza na wataalamu wa  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Hospitali ya Starcare ya nchini India mara baada ya kumalizika kwa kambi maalumu ya upasuaji mdogo wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure – TAVI). Wagonjwa watatu wenye umri wa zaidi ya miaka 70 walibadilishwa Valvu katika kambi hiyo.

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa  Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Hospitali ya Starcare ya nchini India mara baada ya kumalizika kwa kambi maalumu ya upasuaji mdogo wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure – TAVI). Wagonjwa watatu wenye umri wa zaidi ya miaka 70 walibadilishwa Valvu katika kambi hiyo.

…………………………

Kwa mara ya kwanza tangu huduma za matibabu ya moyo zianze kutolewa nchini Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefanya upasuaji mdogo wa moyo wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu (Aortic Valve) bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure – TAVI)

 Upasuaji huo wa historia umefanyika kwa wagonjwa watatu wenye umri wa zaidi ya miaka 70 katika kambi maalumu ya matibabu ya siku mbili iliyofanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu wa JKCI na wenzao wa Hospitali ya Starcare ya nchini India.

 Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu alisema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya afya hii ikiwa ni pamoja na kujenga majengo ya kisasa, kusomesha wataalamu na kuunua vifaa tiba vya kisasa kumewezesha kufanyika kwa upasuaji huo.

 Dk Jingu alisema kutokana na umuhimu mkubwa wa sekta ya afya Serikali itaendelea kuboresha huduma ya afya ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu katika  nchi mbalimbali ambao watakuja kutoa matibabu ya kibingwa nchini.

Kwa Julai hadi Desemba mwaka huu alidokeza kuwa JKCI imehudumia zaidi ya wagonjwa 3,000 katika kufanya upasuaji mkubwa na mdogo wa moyo na kusisitiza  Serikali itaendelea kuhakikisha  wananchi wanapata huduma za kibingwa za matibabu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge aliishukuru Serikali kwa kuiwezesha Taasisi hiyo ambayo imeweza kufanya  matibabu hayo ya kihistoria ambapo kwa nchi za Afrika  hakuna hospitali ya Serikali inayotoa huduma hiyo.

“Wagonjwa wa namna hii ambao ni wengi na walikuwa hawajui waende kutibiwa wapi, wengine tulikuwa tunawapeleka India, Afrika kusini kupata matibabu ambako walitumia fedha nyingi kulipia matibabu haya”,.

“Serikali ya awamu ya sita imetuwekea vifaa vingi ambavyo vimewezesha wagonjwa hawa kufanyiwa matibabu, hata wenzetu walifurahia aina ya vifaa tulivyonavyo ambavyo vimewawezesha wataalamu wetu kufanya upasuaji wenyewe kwa asilimia 90”,alisema Dkt. Kisenge.

Aidha Dkt. Kisenge alisema JKCI imeendelea  kuwa kituo cha utalii tiba ambapo wagonjwa kutoka nchi 20 za Afrika zinafika kwenye taasisi hiyo kupata matibabu

kutokana na wingi wa wagonjwa, aliiomba Serikali jengo lingine kwaajili ya kuwahamishia wagonjwa ombi ambalo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Jingu alisema linafanyiwa kazi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tiba ya Moyo Dkt. Tatizo Waane alisema ugonjwa huo hutokana mabadiliko ya mwili, alieleza kwamba kwa watu wazima tatizo hilo huchangiwa na umri mkubwa ambapo valvu husababisha kuzalishwa kwa madini chokaa ndani ya mshipa wa moyo.

“Chokaa hizo hujikusanya na baadae hufanya damu kushindwa kutoka na kuingia kwenye moyo hivyo figo, ubongo na viungo vingine mwilini huanza kupata damu kidogo na mhusika huanza kupata maumivu ya kichwa na kifua,”alisema Dkt. Waane.

Dkt. Waane ambaye pia ni daktari bingwa wa moyo na mishipa ya damu alisema kupitia njia ya tundu dogo daktari humhudumia mgonjwa ndani ya saa moja hadi mbili na mgonjwa kuondoka wodini siku inayofuata tofauti na upasuaji mkubwa wa kufungua kifua ambao mgonjwa hutumia zaidi ya wiki wodini.

Kuhusu gharama ya matibabu alisema, mgonjwa mmoja hapa nchini sasa atatibiwa kwa shilingi milioni 82 tofauti na nje ya nchi ambapo mgonjwa anatibiwa kwa shilingi milioni 150. 

 Nao wagonjwa waliofanyiwa upasuaji huo mdogo wa kubadilisha Valvu walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa imewasaidia kupunguza maumivu ya matibabu ambayo wangeyapata kama wangefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo. 

“Nilipelekwa Cathlab jana mchna kwaajili ya kufanyiwa upasuaji mdogo wa moyo wa kubadilisha Valvu na ilipofika jioni nilipelekwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) leo asubuhi wakanirudisha wodini ninamshukuru Mungu ninaendelea vizuri na daktari ameniambia kesho jioni nitaruhusiwa kurudi nyumbani”,.

 “Ninaishukuru sana Serikali kwa kunipunguzia gharama ya matibabu, gharama ya upasuaji huu ni shilingi milioni 82 lakini mimi nimepunguziwa na kulipia shilingi milioni 25,500,000/= ninawasihi watanzania wenzangu wasiende nje ya nchi kutibiwa moyo kwani huduma hizi zinapatikana hapa nchini na wataalamu wako wa kutosha”, alisema Mchungaji Donald Lema mkazi wa  Machame Kilimanjaro.

By Jamhuri