Na Tatu Saad,JAMHURIMedia

Klabu ya walima miwa kutoka mjini Morogoro ‘Mtibwa Sugar’ imetoa shukrani zake kwa wote waliokuwa nao katika kipindi kigumu cha msiba wa aliyekuwa mchezaji wao Iddy Mobby Mfaume.

Kabla ya kukutana na wekundu wa msimbazi Machi 11, mwaka huu, na kupigwa goli 3-0 pale uwanja wa Manungu mjini Morogoro, klabu ya Mtibwa ilipata mtikisiko mkubwa kwa kufiwa na beki wao wa kulia Iddy Mobby.

Akizungumza kutoka mkoani Morogoro Afisa habari wa Mtibwa Sugar Thobias Kifaru, amesema wao kama Mtibwa Sugar wanawashukuru sana wote waliyojitokeza katika msiba huo na wote waliowafariji kwa namna moja ama nyingine katika kipindi hiki kigumu kwao.

“Sisi kama Mtibwa Sugar tunatoa shukrani zetu za ndhati kwa wale wote waliokuwa pamoja na sisi katika kipindi hiki kigumu na kutufariji kwa namna moja ama nyingine” amesema Kifaru.

Kifaru amesema anawashukuru sana Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi ya Tanzania, kwani baadhi ya viongozi waliacha majukumu yao yote na kwenda katika mazishi ya mchezaji huyo, ambapo kwao kama klabu na familia ya marehemu wamefarijika sana kwa uungwana huo wa viongozi wa soka nchini.

Vilevile shukrani nyingine zimeenda kwa mwenyekiti wa chama cha mpira mjini Shinyanga kwa kuwapokea vizuri na kuwakirimu vyema tangu walipofika Shinyanga.

Hata hivyo Mtibwa hawakuwasahau madaktari walioshiriki katika matibabu ya marehemu Iddy Mobby katika kipindi cha ugonjwa wake kabla umauti kumfika, Kifaru amesema wanawashukuru sana kwa jitihada na mchango wao.

Baada ya shukrani Kifaru amemzungumiza Marehemu Iddy Mobby kwa uchache kuwa ni mtu wa kipekee sana aliyekuwa akiishi na kila mtu vizuri, hakuwa na majivuno alikuwa ni mtu wa kujifunza sana, hakuwahi kuwa mbali na Mungu, Iddy Mobby alikuwa ni mtu wa kuswali anayejali sana dini.

Uongozi wa klabu hiyo pia umeahidi kuitembelea familia ya Iddy Mobby katika kila safari yao ya mechi itakayokuwa njia hiyo ya Shinyanga, huku wakimuenzi Mobby kwa kutompa mtu yoyote jezi namba nne kwa muda wa miaka minne kwani ndio namba aliyokuwa akiivaa kipindi chote alichoitumikia Mtibwa.

By Jamhuri