Na Wilson Malima, JAMHURI MEDIA

Mtoto wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Mhoozi Kainerugaba ametangaza nia ya kutaka kumrithi Baba yake kiti cha Urais wa Uganda ambapo amesema atagombea Urais wa nchi hiyo ifikapo mwaka 2026.

Mhoozi ambaye ni Jenerali wa Jeshi la nchi hiyo ametangaza nia hiyo kupitia ujumbe wake katika mtandao wa Twitter jana Jumatano, akidai kuwa watu ndiyo wamemtaka kufanya hivyo.

“Katika jina la Yesu Kristo, kwa jina la Vijana wa Uganda na Dunia kwa ujumla na katika jina la Mapinduzi makubwa nitagombea Urais mwaka 2026” amesema Mhoozi

Mhoozi ameendelea kutoa kauli za aina hiyo katika mtandao huo akijilinganisha na baadhi ya viongozi mbalimbali duniani waliotawala na walioko madarakani wakiwa na umri mdogo, amesema sasa ni muda wa vijana kuanza kunga’ra na kuwa amechoshwa kuongozwa na wazee.

“Fidel Castro Shujaa wangu alikuwa Rais akiwa na umri wa miaka 32, ninakaribia kufikia miaka 49, sio sawa kabisa (Kutokuwa Rais), Vijana wanapaswa kuwa Marais wa Mataifa yao” amesema

“Nani anakubaliana na Mimi kwamba muda wetu Vijana umewadia?, inatosha sasa kuendelea kuongozwa na Wazee na kututawala, ni muda wa Vijana kung’aa, Waziri Mkuu wa Uingereza ana miaka 42, Waziri Mkuu wa Finland ana miaka 37, sisi wengine tunakaribia miaka 50, tumechoka kusubiri, nitasimama kugombea” amesema Mhoozi

Siyo mara ya kwanza kutangaza nia yake ya kutaka kugombea Urais wa taifa hilo, Mhoozi amekuwa akifanya hivyo hata mara baada ya  kuvuliwa cheo cha Jenerali wa Jeshi la Ardhini na kupandishwa kuwa Jenerali kamili, aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter nia yake ya Kutaka kugombea Urais wa nchi hiyo.

Mhoozi ambaye ni mtoto wa Kiume wa Rais wa Uganda Yoweri Mseveni amekuwa akitumia mtandao wa Twitter kutoa kauli mbalimbali ambazo huibua hisia mseto miongoni mwa watumiaji wa mtandao huo

By Jamhuri