Mubarak: Rais wa Misri aliyetorosha mabilioni

Na Nizar K Visram

Mahakama ya Umoja wa Ulaya (EU) imeamuru mali za rais wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak, ambazo ziko Ulaya zisizuiwe, hivyo kuiruhusu familia yake kuzimiliki bila pingamizi.

Hukumu hiyo imetolewa Aprili 6, mwaka huu, ikihitimisha kesi iliyowasilishwa na familia kuhusu mali za Mubarak zilizokuwa zimezuiwa katika nchi za EU. 

Vikwazo viliwekwa na EU vikiwazuia Mubarak, mke wake na watoto wao wawili kuchukua mali hizo, kufuatia kupinduliwa kwa Mubarak Januari 2011. 

Lengo lilikuwa kuiwezesha Serikali ya Misri kuzidai mali za Mubarak ambazo inaaminika alizipata kwa njia zisizo halali. Sasa familia yake itaweza kuzichukua badala ya kurudishwa kwa wananchi wa Misri. 

Inakisiwa kuwa Mubarak alitorosha dola bilioni 70. Kati ya fedha hizo ni dola milioni 664 tu ziligunduliwa katika benki za Uswisi. Ni kwa sababu zimefichwa katika nchi mbalimbali ambazo haziko tayari kufichua habari kikamilifu.

Kama ilivyo kawaida kwa fedha zinazotoroshwa nje ya nchi, benki na nchi za Magharibi zinaweka masharti magumu ili fedha hizo zirudishwe zilikotoka. Mara nyingi zinadai kuwa ili fedha zirudishwe ni lazima mtuhumiwa afikishwe mahakamani na ithibitishwe kuwa amezipata kwa njia za kifisadi. 

Swali ni je, watawala wa Misri walipenda Mubarak achukuliwe hatua kama hiyo? Kama watawala waliomrithi nao pia wanafanya kama yeye maana yake ‘leo kwake kesho kwako’. 

Hapa ndipo nchi za Kiafrika kama Misri zinakwama kuchukua hatua, kwani tatizo hili lipo katika nchi nyingi barani Afrika. 

Kwa mujibu wa Gazeti la Washington Post, Mubarak na watoto wake wawili wanamiliki majumba katika miji kama London, Los Angeles na New York. Kwa mfano, mwanawe Gamal anamiliki jengo lenye ghorofa tano jijini London lenye thamani ya dola milioni 20. Anwani yake ni 28 Wilton Place, Belgravia.

Gazeti la Kiarabu liitwalo Al Khabar limesema Mubarak ana majengo New York katika maeneo ya Manhattan na Beverly Hills (Rodeo Drive).  Pia limesema familia ya Mubarak ilificha fedha nyingi katika benki za Swisi, UBS, Bank of Scotland na Lloyds.

Mubarak hakukusanya mali zote hizi kutokana na mishahara na posho. Alianza kujilimbikizia mali tangu alipokuwa ofisa katika jeshi la anga. Hii ni kawaida nchini Misri ambako makamanda wana hisa katika mikataba ya kijeshi kama vile ununuzi wa silaha au misaada ya kijeshi kutoka nje. Watoto wake nao walikuwa wakila rushwa kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje. Hii ni kwa mujibu wa Gazeti la Sunday Telegraph.

Christopher Davidson, profesa wa siasa za Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Durham, anasema nchini Misri ni kawaida kuwataka wawekezaji wa kigeni watoe asilimia 20. Anasema kila mradi wa kigeni ulitakiwa uwe na mdhamini wa kienyeji na hapa ndipo Mubarak alikuwa akipiga dili tangu alipokuwa jeshini na baadaye Ikulu. 

Aladdin Elaasar aliandika kitabu kiitwacho ‘Farao wa Mwisho: Mubarak’ (The Last Pharaoh: Mubarak). Yeye anaeleza jinsi Mubarak alivyomiliki majumba nchini Misri. Kuna aliyoyarithi kutoka kwa marais waliomtangulia na mengine ni ya mfalme aliyepinduliwa.   

Ni nadra kwa wanaotorosha fedha kufanya hivyo kwa kuzijaza katika mabegi wanaposafiri. Nicholas Shaxson ni mwandishi wa kitabu kiitwacho ‘Watu Walioiba Dunia’ (Men Who Stole the World). Anaeleza kwa kutoa mfano wa ununuzi wa mashine ya dola milioni moja. 

Unalipa milioni mbili ili milioni moja ziwekwe katika akaunti yako ya siri nje ya nchi. Mwandishi anasema kwa njia hii Mubarak alificha fedha ‘zake’ London, Singapore au Dubai na kununua majengo Marekani na Uswisi.

Mei 2014, Mubarak na wanawe walishitakiwa nchini Misri kwa kuchota dola milioni 17.6  kutoka mfuko wa serikali ili kukarabati nyumba zao binafsi. Fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya kukarabati Ikulu. Mahakama ikamhukumu Mubarak kifungo cha miaka mitatu kwa kosa la kuiba fedha za umma. 

Watoto wake walihukumiwa kifungo cha miaka minne. Pia wakahukumiwa kulipa faini ya dola milioni tatu na kuzilipa hizo dola milioni 17.6.

Mubarak pia alishitakiwa kwa kutumia vibaya madaraka kwa kuamuru mauaji ya waandamanaji wasiopungua 800 waliokuwa wakimtaka aondoke madarakani mwaka 2011. Akaonekana ana hatia na akahukumiwa kifungo cha maisha.

Novemba 2014 mahakama ikamfutia Mubarak kesi ya mauaji. Wananchi wakaandamana, wakakumbana na majeshi yakiwa na vifaru, bunduki na mabomu ya machozi.

Mubarak alikuwa Mkuu wa Majeshi ya Anga na mwaka 1972 akateuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi.  Mwaka 1975 akawa Makamu wa Rais chini ya Rais Anwar Saadat. Mwaka 1981 Saadat aliuawa na wanajeshi waliopinga uamuzi wake wa kusaini mkataba wa urafiki na Israel. 

Mubarak akawa Rais. Mara moja akatangaza hali ya hatari akitoa mamlaka kamili kwa majeshi kudhibiti maandamano. Magazeti yakapigwa marufuku. Ikabuniwa mahakama ya kijeshi. Matokeo yake maelfu ya raia walifungwa bila mashitaka wala kesi. 

Mwaka 2011 wananchi wakaandamana kwa maelfu wakidai demokrasia na haki za kiraia. Licha ya majeshi kutumia nguvu maandamano yakaendelea kwa siku 18 mfululizo hadi Februari 16, 2011 Mubarak akalazimika kuachia madaraka na huo ukawa mwisho wa utawala wake wa miaka 30. 

Awali, Marekani ilimuunga mkono lakini hali ilipochafuka wakamwambia aondoke.

Mubarak akafariki dunia mwaka 2020 akiwa na umri wa miaka 91, akiicha Misri ikidaiwa dola bilioni 30 wakati yeye akiwa ameficha nje dola bilioni 70.

Huyu ndiye Hosni Mubarak ambaye mwaka 2008 Uingereza ilimpatia silaha za kijeshi za dola milioni 37. Mwaka uliofuata akapewa silaha za dola milioni 26. Marekani nayo imekuwa ikimpatia silaha za dola bilioni 1.3 kila mwaka. Ni Israel tu ndiyo iliyopewa zaidi ya hizo.

Mwaka 2011, ubalozi wa Marekani jijini Cario uliandika ripoti ya siri ikisema serikali ya Rais Obama ilikuwa na nia ya kujenga uhusiano wa karibu wa kidiplomasia na kijeshi na Mubarak. 

Ripoti nyingine ilisema silaha za dola bilioni 1.3 na bidhaa nyingine za  dola milioni 815 ambazo Marekani ilimpa Mubarak kila mwaka ni vivutio ili aendelee kuiunga mkono Israel. 

Kwa minajili hiyo, Mubarak alialikwa Marekani na akakutana na marais Bush na Obama.  

Edward Walker, aliyekuwa Balozi wa Marekani nchini Misri alisema misaada wanayotoa kwa Misri ilisaidia kuepukana na vurugu au mapinduzi. Ni dhahiri balozi huyo hakutazamia kuwa wananchi wangemuondoa Mubarak licha ya ‘misaada’ hiyo.

Moja ya kazi ya Marekani aliyokuwa akiifanya Mubarak ni kupokea wafungwa kutoka shirika la kijasusi la CIA, kwa madhumuni ya kuwatesa. CIA ilikuwa ikiwapeleka watuhumiwa wa ugaidi Misri ambako walikuwa wakiteswa mpaka wakubali kuwa walishiriki ugaidi. 

Kisha wafungwa hao wakichukuliwa na CIA na kufungwa katika Gereza la Guantanamo. Mtindo huo wenyewe waliuita ‘rendition’.

Mfano mmoja ni Ibn al Sheikh al-Libi  (Ali Mohammed al-Fakheri) ambaye aliteswa nchini Misri hadi akakubalishwa kuwa Saddam Hussein alikuwa akitoa silaha za kemikali kwa Al Qaeda. 

George W Bush akatumia ‘ushahidi’ huo bandia kumshutumu Saddam kuwa ana silaha za kemikali ambazo anampa Osama. Akajenga hoja bandia na kuishambulia Iraq na kumuua Saddam.

Kazi ya utesaji nchini Misri ilikuwa ikifanywa na Jenerali Omar Suleiman aliyekuwa mkurugenzi wa intelijensia wa Mubarak. 

[email protected]

+1 343 20448996 (WhatsApp)