Simba inakaba hadi kivuli

Yanga dk 90 bila shuti golini

Na Andrew Peter

Dar es Salaam 

Yanga imeweka rekodi mpya ikicheza dakika 90 bila kupiga shuti hata moja lililolenga goli wakati walipolazimishwa suluhu na watani wao Simba kwenye Uwanja wa Mkapa mwishoni mwa wiki.

Kwa matokeo hayo, Yanga imeendelea kuongoza ligi ikiwa na pointi 55, bila ya kupoteza mechi, wakifuatiwa na Simba yenye pointi 42, huku Namungo na Azam zikifuatia katika nafasi ya tatu na nne wakiwa na pointi 29 kila moja wakitofautiana mabao.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga iliingia katika mchezo huo ikiwa na rekodi ya kufunga mabao 35 katika michezo 20 ya Ligi Kuu, lakini walishindwa kufua dafu mbele ya ngome ya Simba kwa kufanikiwa kupiga mashuti matatu tu – mawili ya Feisal Salum na moja la Fiston Mayele ambayo yote hayakulenga goli.

Wakati Simba katika mchezo huo ilipiga mashuti mawili yaliyolenga goli na manne hayakulenga lango la Yanga katika mchezo huo uliotawaliwa na viungo zaidi.

Safu ya ulinzi ya Simba chini ya Henock Inonga na Joash Onyango iliendeleza pale ilipoishia katika mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Yanga kwa kumficha kabisa Mayele.

Kinara wa ufungaji wa mabao katika Ligi Kuu, Mayele, akiwa amezifumania nyavu mara 12 hadi sasa, alikuwa chini ya ulinzi mkali wa Inonga na Onyango katika dakika zote za mchezo huo.

Pamoja na jitihada zake, Mayele alifanikiwa kupiga shuti moja tu lililogonga nyavu za pembeni mwa goli katika dakika ya 71 baada ya kupokea pasi ndefu ya Saido Ntibazonkiza.

Lakini muda wote kila Mayele alipogusa mpira alikuwa chini ya ulinzi wa Inonga au Onyango waliokuwa makini katika kumpoka mipira au kuzuia mpira kabla ya kufika kwa mfumania nyavu huyo.

Kosa la Nabi

Katika mchezo huo Yanga ilicheza bila ya Kocha wake, Mohamed Nabi, anayetumikia adhabu, hivyo jukumu lake kuwa chini ya msaidizi wake, Fredrick Kaze. 

Yanga walifanya kosa kumchezesha Saido katika winga, kwani alikosa kabisa mbinu za kuipenya ngome ya Simba.

Uamuzi wa kumchezesha Saido pembeni ulimnyima uhuru Mrundi huyo na kumweka mbali na Mayele, jambo lililofanya Yanga ishindwe kulisogelea kabisa lango la Simba.

Saido mwenye mabao sita hadi sasa amekuwa na mchango mkubwa akicheza nyuma ya Mayele kutokana na uwezo  wake wa kupiga pasi na kukaa na mpira.

Ni wazi Nabi na Kaze walifanya kosa kuamua Saido acheze pembeni huku wakijua hana kasi kutokana na umri wake pamoja na mwili wake, jambo lililofanya Kapombe kuwa huru zaidi.

Uamuzi wa kuwatoa Moloko na Fei Toto na kuingia chipukizi Denis Nkane na Farid Mussa kwenda kucheza katika winga na Saido kucheza kati, ndipo Mrundi huyo alipopata nafasi ya kupiga pasi nzuri ya juu iliyomkuta Mayele na kupiga shuti lililogonga nyavu za pembeni mwa goli katika dakika ya 71.

Kosa jingine la Kocha Nabi, aliingia katika mchezo huo akitumia mfumo wa 4-2-3-1 akiwa na mabeki Djuma Shaaban, Kibwana Shomari, Bakari Mwamnyeto na Dickson Job wakati viungo wakiwa ni Yannick Bangala, Khalid Aucho na Feisal Salum ‘Fei Toto’ huku Saido na Moloko wakitokea pembeni na Mayele akiwa mshambuliaji pekee.

Mbinu hii ilifanya Yanga kumiliki mpira, lakini ilishindwa kupita kupitia pembeni, kwani Moloko na Saido walikosa namna bora ya kuwapita Shomari Kapombe na Mohamed Hussein na kujikuta wakipiga mipira mirefu kwa Mayele aliyekuwa chini ya ulinzi wa mabeki wawili.

Yanga walikuwa bora zaidi katika kujilinda na mashambulizi ya kushtukiza ya Simba, kwani mara zote walikuwa wachezaji wanane katika ukuta wao, jambo lililowanyima nafasi wapinzani wao.

Aucho na Fei Toto muda mwingi walikuwa wakicheza pasi wakiwa katika nusu yao huku wakienda kushambulia kwa kasi ndogo iliyotoa mwanya kwa mabeki wa Simba kujipanga na kuharibu mipango hayo.

Mhispania noma

Kocha wa Simba, Pablo Martin, alijua ubora wa Yanga katika kushambulia, naye aliingia katika mchezo huo na mfumo wa 4-2-3-1 kama ule aliotumia katika mchezo wao wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates waliotolewa kwa penalti.

Mabingwa hao watetezi waliingia kwa lengo la kuharibu mipango ya kushambulia ya Yanga na kushambulia kwa kushtukiza.

Simba ilianza na viungo wawili wakabaji – Jonas Mkude na Saido Kanoute, huku ikiwaweka pembeni Bernard Morrison na Pape Sakho kwa lengo la kuwafanya Djuma na Kibwana wasipandishe mashambulizi kupitia pembeni.

Mbinu ya kuwazuia Djuma na Kibwana ilifanikiwa, kwani mabeki hao muda mwingi walishindwa kushambulia kama kawaida yao zaidi ya kuimarisha ulinzi golini kwao.

Muda mwingi wa mchezo ilikuwa rahisi kuona Morrison na Pape wakibadilisha upande kwa lengo la kuwachanganya mabeki wa Yanga, jambo lililofanikiwa hata pale Morrison alipotoka na nafasi yake kuchukuliwa na Kibu Denis.

Katikati ya uwanja viungo wa Simba, Kanoute na Mkude walitimiza vema majukumu yao kwa kuhakikisha Aucho,  Fei Toto na Saido hawapati kabisa nafasi ya kupitisha pasi kwa Mayele.

Unaweza kusema Aucho alijua kikwazo kwao ni Kanoute na kuamua kumchezea vibaya katika dakika ya 49, na kusababisha kiungo huyo wa kimataifa wa Mali kutolewa nje.

Kutoka kwa Kanoute kulitoa nafasi kwa Yanga kutengeneza nafasi kadhaa za kufunga, ikiwamo ile ya dakika ya 71, ambayo Mayele alipokea pasi ndefu ya Saido na kupiga shuti lake pekee katika mchezo huo lililogonga nyavu za pembeni.

Nguvu, ubabe, mbinu zilizotumiwa na viungo wa timu zote mbili katikati ya uwanja halikuwa jambo la ajabu kuona Yanga ikicheza madhambi 17 huku Simba ikicheza mara 13.

Shukrani kwa mwamuzi Ramadhani Kayoko aliyekuwa makini kwa kwenda na kasi ya mchezo huo na kushuhudi kadi saba za njano. Yanga kadi nne na Simba kadi tatu kutokana na matukio mbalimbali.

Yanga, Simba yanukia nusu fainali ASFC

Yanga na Simba zinaweza kukutana tena katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) iwapo mabingwa watetezi watashinda mechi yao ya robo fainali dhidi ya Pamba.

Simba inajua nafasi kubwa ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani itapatika kupitia Kombe la ASFC, kuliko Ligi Kuu ambako wako nyuma kwa tofauti ya pointi 13 kwa watani wao Yanga wanaosaka taji la kwanza la ligi baada ya miaka minne.

Mara ya mwisho Yanga kutwaa mataji yote mawili ilikuwa ni msimu wa 2016, kabla ya kupisha utawala wa Simba ambayo misimu miwili 2019-20 na 2020-21 ilitwaa mataji yote.

Rekodi ya Simba

Suluhu hii inaiweka Yanga katika nafasi nzuri ya kuisaka rekodi Simba ya miaka 12 iliyopita ya kutwaa ubingwa wa ligi bila ya kufungwa iwapo haitapoteza katika mechi zake tisa zilizobaki za Ligi Kuu.

Msimu wa 2009-10, Simba ilitwaa ubingwa bila kufungwa mchezo wowote katika michezo 22 iliyocheza ilipoteza pointi 4 pekee, baada ya kutoka sare mbili pekee dhidi ya African Lyon na Kagera Sugar, huku ikishinda mechi 20, na kujikusanyia pointi 62 huku ilifunga jumla ya mabao 50 na kufungwa mabao 12.

Yanga inaweza kutangaza ubingwa iwapo itashinda michezo hii: Dhidi ya Ruvu Shooting utakaochezwa Mei 4, kabla ya kuwakaribisha Mbeya Kwanza kwenye Uwanja wa Taifa (Mei 21). 

Itakwenda mkoani Mara kuivaa Biashara United (Mei 24). Itarudi jijini Dodoma (Juni mosi) kuwakabili Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri.

Aprili ngumu

Watani wa Jadi,  Yanga na Simba wameendelea kuthibitisha kwamba mechi za Aprili ni ngumu kwao kupata ushindi. Tangu mwaka 1982 zimekutana mara 12, zikitoka sare mara sita huku kila timu ikishinda mechi tatu tu.

Rekodi ya Aprili Yanga na Simba

 APRILI 29, 1982 

Yanga 1-0 Simba

APRILI 16, 1983 

Yanga 3-1 Simba

APRILI 30, 1988 

Yanga 1-1 Simba

APRILI 12, 1992 

Yanga 1-0 Simba

APRILI 26, 1997 

Yanga 1-1 Simba

APRILI 17, 2005 

Simba 2-1 Yanga

APRILI 27, 2008

Simba 0-0 Yanga

APRILI 19, 2009 

Simba 2-2 Yanga

APRILI 18, 2010 

Simba 4-3 Yanga

APRILI 19, 2014 

Simba 1-1 Yanga

APRILI 29, 2018 

Simba 1-0 Yanga

APRILI 30, 2022

Yanga 0-0 Simba