Ottawa

Na Chambi Chachage 

Hakika mengi yamekwisha kusemwa. Mazuri na mabaya. Bila shaka yataendelea kusemwa na kuandikwa. Ni kuhusu aliyekuwa Rais wa Tano Tanzania, Dk. John Magufuli, aliyetutoka rasmi kipindi kama hiki mwaka jana.

Jukumu langu katika makala hii ni moja tu. Kutimiza ahadi niliyoitoa wakati huo ya kuandika waraka wa kumuaga Rais huyo wa aina yake. Pengine wahenga hawakukosea waliposema ‘polepole ndio mwendo’, ‘haraka haraka haina baraka’ na ‘kawia ufike’. Basi muda muafaka sasa umefika wakati taifa linaposimama tena kumkumbuka kiongozi huyo.

Labda aliyekuwa Rais wa Kwanza, Mhenga Mwalimu Julius Nyerere, naye alikuwa sahihi aliposisitiza ‘lazima tukimbie wakati wengine wakitembea’. Alikuwa akimaanisha, kwa kiwango hafifu cha maendeleo ya kisasa tulichokuwa nacho ukilinganisha na mataifa yaitwayo yameendelea, hatukuwa na budi kujenga taifa letu kwa kasi kama ya wakimbiaji wa Marathon.

Sidhani kama kumekuwa na Rais wa Tanzania ambaye ameuishi ‘urais’ kwa msemo huo wa mmoja wa waasisi wa taifa hili kama Magufuli. Hata Rais wa Nne, Jakaya Kikwete na kaulimbiu yake ya ‘Ari Mpya, Kasi Mpya na Nguvu Mpya’ hakukimbia hivyo. Magufuli alikimbia hasa! Ilikuwa kama anakimbizwa. Na akakimbiza (naye). Akaishia kuwa ‘mwendazake’.

Nakumbuka vilivyo kipindi cha uchaguzi wa mwaka 2015 uliomweka Magufuli madarakani. Sikuwa miongoni mwa waliompigia kura. Lakini nilibahatika kwenda kupiga kura nikiongozana na wadau waliosoma naye chuoni. 

Japo walikuwa na wasiwasi kuhusu mwamko wa wapiga kura wa mpinzani wake wa wakati huo, Edward Lowassa, walikuwa na shauku kuona mwanafunzi mwenzao wa enzi hizo ambaye hakuwa na mzaha mzaha, akiongoza nchi.

Kwa kweli nilishindwa kuwaamini maana picha niliyokuwa nayo kichwani ni ya orodha ya waliouziwa nyumba za serikali katika mazingira tete enzi za uwaziri wake wa Ujenzi niliyoiona kwenye ofisi moja kwa bahati mbaya. 

Hata wenzangu tuliokulia nao maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kipindi cha uanafunzi wake hawakuweza kunifanya niamini. Walitukumbusha jinsi Magufuli alivyokuwa mnoko, yaani mkali walipokuwa wakileta mchezo mchezo kijiweni wakati akijisomea. Ukali huo waliamini utanyoosha mambo.

Bila ajizi, Rais Magufuli alianza kwa kasi kunyoosha watu na mambo yao. Sifa zake zikaenea kila kona ya nchi na Bara la Afrika pamoja na pande nyingi za dunia. Waliokuja kuwa wakosoaji wake wakuu baadaye wakawa mstari wa mbele kumtumia kama mfano wa kuigwa kwa kutupa kipimo kirahisi cha kujiuliza: Je, Magufuli angefanyaje? 

Hata watoto ujumbe uliwafikia. Namkumbuka mtoto mmoja alituuliza hicho kipimo kina maana gani hasa na baada ya kumuelezea naye akajiuliza: “Nilitaka ninunue runinga bapa kwa ajili ya kutazama vibonzo ila nikajiuliza, je, Magufuli angefanyaje, basi nikachukua kitabu nijisomee.”

Ilikuwa ni vigumu kusema lolote dhidi ya shujaa huyo mpya hasa alipoanza kufanya kile alichokiita ‘kutumbua majipu’, yaani kufukuza watu kazi hima kutokana na yaliyoonekana ni makosa yao. 

Hata dalili zilipoanza kujitokeza kuwa kasi yake inaweza kuleta madhara, ujumbe ulikuwa tutulie dawa ituingie. 

Mapema kabisa Desemba 10, 2015 nilijaribu kusema haya baada ya kuchambua ‘Majibu ya Magufuli na Kazi ya Wanahabari Wetu’ na kuona walakini:

“Wahenga walinena kuwa ‘nyota njema huonekana asubuhi’ na ‘dalili ya mvua ni mawingu’. Kipindi hicho kifupi cha maswali na majibu kati ya wanahabari na Rais kinaweza kutupa mwelekeo wa huko tuendako. Japo madai ya Katiba mpya yanazidi kusahaulika katika kipindi hiki cha mwamko wa ‘Magufulika’, tukumbuke kuwa hata hii Katiba ya Mwaka 1977 tuliyonayo inasisitiza kwamba:

    “‘Kila mtu… anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii’” – Ibara ya 18 (d)

    “Lakini pia Ibara ya 18 (b) ya Katiba hiyo tuirekebishayo inasema:

    “‘Kila mtu… anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi’.

    “Kupewa taarifa ni haki. Na kutoa habari ni kazi. Hapa hakikazi tu.”

Haikuchukua muda mrefu makucha ya Magufuli yakaanza kukunjuka na kuonekana zaidi. Uhuru wa habari na haki ya kupata taarifa ikawa mwiba mchungu kwake. Aliona vinampunguzia kasi ya kukimbia na kukimbiza. Cha ajabu Rais aliyeonekana kuwa mstari wa mbele kupiga vita rushwa na ufisadi akawa mstari wa nyuma kuwaunga mkono wale ambao kazi zao kuu ni kufichua wala rushwa na mafisadi. Mpenda mwanga akaruhusu giza litamalaki.

Tukaona aliyekuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, akiondolewa kwenye nafasi yake katika mazingira ya kutatanisha. Kama unapenda ukweli iweje usimpende msema kweli? Na wanahabari na mabloga cha moto tulikiona. Wapo waliofunga blogu zao, wengine tukazihamishia zetu nje ya nchi huko Zimbabwe. Vyama vya upinzani navyo vilionja joto ya ‘Jiwe’ kutoka kwa Rais aliyepachikwa jina hilo na la ‘Chuma’.

Pengine ni ushunuzi, yaani saikolojia, pekee unaoweza kutusaidia kuelewa kwa nini Magufuli alikuwa na pande mbili kinzani. Ni kama vile Magufuli wa upande mmoja angekutana na Magufuli mwingine wangetumbuana. Magufuli mpenda mwanga na msema kweli dhidi ya Magufuli mkubali ‘giza’ na ‘udanganyifu’. 

Huku Magufuli mpenda ‘ufichuaji’ na ‘utumbuaji’, kule Magufuli mlinda ‘wafichaji’ na ‘wapigaji’. Pale Magufuli mpenda haki na demokrasia, hapo Magufuli msababisha wanahaki na wanademokrasia washindwe kufanya kazi na harakati.

Yin-Yang, ile dhana ya Kichina kuhusu uwili au upacha wa chanya na hasi, ilidhihirika sana katika hulka na utendaji wa Magufuli. Lakini mara nyingi Yin ilipingana na Yang badala ya kuwa katika uwiano/mizania. Hali hii ilisababisha mashabiki wake wengi wakanganyikiwe na wengine kubadili timu kabisa hasa baada ya kile kipindi cha awali cha fungate ya Magufulika.

Dai mojawapo la Timu Magufuli au ‘Magufuli Yekka’, kama walivyokuwa wanataniwa na baadhi ya wakosoaji wake, ni kuwa walalamikaji walikuwa ni watu wa daraja la kati na juu ambao walijiona miungu watu kabla hajawa Rais. 

Lakini ukiwabana kwenye suala la uminyaji wa uhuru na ukandamizaji wa demokrasia, wapo waliokiri ukweli. Ila baadhi waliona hiyo ni kafara tosha kwa ajili ya kuleta maendeleo makubwa na kuwanyanyua watu wa daraja la chini.

Si kila mtu alilitazama tatizo hili kama sehemu ya mbio za Magufuli. Nakumbuka kuwasikia wakati wa uchaguzi wa mwaka 2015 wadau waliosoma naye wakikumbushana kuhusu jinsi walivyomchangia kwenda kutibiwa ughaibuni. 

Wakati huo sikujua kwamba walilizungumzia kama sehemu ya hofu yao. Ila baadaye tulipokuja kujulishwa rasmi sababu rasmi ya kifo chake na kuona kipande cha gazeti cha enzi hizo alipokuwa akichangiwa, ndipo nikaanza kuelewa kwa nini alikuwa ni mtu aliyekuwa mbioni. Hata hotuba zake nyingi ziliashiria ukimbiaji huo.

Urais wa ‘mbiombio’ ndio uliotufikisha tulipo. Na ndio unaosababisha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ifanye mabadiliko kadha wa kadha kuturudisha kwenye mstari au kutupeleka kwingine. 

Kutokana na kukimbilia na kuiharakisha miradi mikubwa ya maendeleo katika muktadha wa demokrasia finyu ndiyo maana kumeonekana upungufu mwingi kwenye ripoti za CAG. 

Mfano halisi ni matokeo haya ya ukaguzi uliofanywa katika Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP):

“Ukaguzi wangu wa maelezo ya mkandarasi kuhusu ujenzi wa mikondo ya kuchepushia maji ya Mto Rufiji ili kupisha shughuli za ujenzi wa eneo la bwawa kuu ulibaini kuwa, mkandarasi alijenga mkondo mmoja wenye uwezo wa kupitisha maji kiasi cha mita za ujazo kwa sekunde 6,170 badala ya mikondo miwili kwa ajili ya kuchepusha maji yenye uwezo wa kupitisha maji kiasi cha mita za ujazo kwa sekunde 7,000 (main dam). Hii ni kinyume cha Kifungu cha 12.3 cha matakwa ya mwajiri Juzuu ya II ya Desemba 2017 kinachomtaka mkandarasi kujenga mikondo miwili kwa ajili ya kuchepusha maji yenye uwezo wa kupitisha maji kiasi cha mita za ujazo kwa sekunde 7,000.

 “Hii inamaanisha kuwa, ujenzi wa mkondo mmoja badala ya miwili, umepunguza uwezo wa kupitisha maji kwa kiwango cha asilimia 11.9 (kutoka mita za ujazo kwa sekunde 7,000 kama ilivyokusudiwa hapo awali hadi kufikia mita za ujazo kwa sekunde 6,170 ambazo ndizo zilizojengwa).

“Hali hii ilisababisha ucheleweshaji wa mradi kwa miezi mitano kutokana na tuta-kingo la kuzuia maji kugharikishwa, kisha maji kufurika ndani ya mkondo wa kuchepushia maji ya mto. Athari hii ingeweza kuepukika iwapo utekelezaji wa usanifu wa mradi wa awali ungezingatiwa kwa kujenga mikondo miwili kwa kuanza kuchimba mkondo mmoja baada ya mwingine. Hii ni kwa sababu kabla ya eneo hilo kujaa maji, kiwango cha kazi kilikadiriwa kuwa cha kutosha kukamilisha uchimbaji wa mkondo mmoja mfupi (wa urefu wa mita 497 na uwezo wa mita za ujazo kwa sekunde 3,500) ili kuruhusu sehemu ya maji ya mafuriko kupita. Hivyo, wakati maji yaliyokuwa yamefurika yangekuwa yamepita kwenye mkondo mmoja uliokamilika baada ya tuta – kingo la muda kugharikishwa, ujenzi wa mkondo mwingine ungekuwa ukiendelea. Janga lilidumu kwa takriban miezi mitano ya ucheleweshwaji wa kazi za mradi, hivyo basi, iliwezekana kuepukika ikiwa umakini ungezingatiwa katika kutekeleza mikondo miwili ya kuchepushia maji.

“Aidha, uamuzi uliofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika kuidhinisha usanifu wa mkandarasi wa kujenga mkondo mmoja badala ya mikondo miwili kulingana na usanifu wa mradi wa awali haukuzingatia vya kutosha ukubwa wa mafuriko kulingana na taarifa za kihistoria za haidrolojia…

“Maofisa kutoka TANESCO walielezea kuwa, waliridhia mkandarasi kujenga mkondo mmoja badala ya miwili kama ilivyokusudiwa awali, kwa sababu walitaka kuharakisha maendeleo ya kazi, kwani kujenga mkondo wa kuchepusha maji ilikuwa kazi iliyo kwenye shughuli ya lazima katika mradi. Kwa kuwa mbinu ya utekelezaji iliyopendekezwa na mkandarasi ilikuwa na faida ikilinganishwa na muda wa utekelezaji wa mradi. Maofisa hao waliongeza kuwa, ikiwa wangeruhusu kufuata mpango wa awali ingeweza kuchukua hadi miaka mitatu kukamilika. Hata hivyo, TECU [TANROADS Engineering Consulting Unit] haikuzingatia teknolojia na mbinu za uchorongaji mwamba zilizotumiwa na mkandarasi ambazo pia zingesaidia utekelezaji wa ujenzi wa mikondo miwili ya kuchepusha maji ndani ya muda uliopangwa.”(Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali AGR/DP/2019/20, Kurasa za 100-102).

Rai yangu kwetu sote ni kujifunza kutoka kwenye urais huo. Ni urais ulioanza kwa matumaini makubwa. Ukaendelea na ahadi nyingi. Lakini ukazuia hata wale na vile ambavyo vingeufanya utimize mengi kwa maana ili upambane na ubadhirifu unahitaji kuonyeshwa wabadhirifu. Pia ili ulete maendeleo unahitaji wadau wenyewe wa maendeleo wawe huru kuyaleta na/au kuletewa.

Vilevile rai yangu kwa Rais Samia ni kutofuata nyayo za kujiona unajua kila kitu tu. Ni kweli urais humpa mtu fursa ya kujua mambo mengi ya nchi pengine kuliko mtu mwingine yeyote kama Rais Magufuli alivyopenda kusisitiza. Lakini kuna watu na ujuzi wao, wananchi na uzoefu wao, na wataalamu na utaalamu wao. 

Ukiwasikiliza kabla na badala ya kuwaumbua watakuambia maana ya ufikikaji. Ni huko kufikika ambako Watanzania wanakuhitaji waendelee.

Zama za Magufuli sasa zimekwisha. Daima tuenzi mazuri aliyotuachia. Kamwe tusiyaendeleze mabaya yoyote.

Fahari ya taifa ni uhuru. Ufikikaji wa uhuru uendelee. Tukimbie ila huo uhuru tusiubanebane.

Mwandishi wa makala hii ni Profesa (Msaidizi) wa Chuo Kikuu cha Carleton kilichopo Ottawa, Canada. Mara ya kwanza ilichapwa katika tovuti ya udadisi.

Please follow and like us:
Pin Share