Cutsleeve Riddim yagusa Tanzania

DAR ES SALAAM

Na Christopher Msekena

Kumekuwa na utaratibu wa lebo kutoa nyimbo zinazowahusisha wasanii wanaowasimamia na hakika zimekuwa zikifanya vizuri kwenye chati mbalimbali za muziki.

Mfano kipindi cha nyuma lebo ya WCB iliwahi kuachia wimbo wa pamoja unaoitwa ‘Zilipendwa’, hii ni miongoni mwa nyimbo zenye namba kubwa, hasa ukizingatia wasanii kama Diamond Platnumz, Rayvanny, Harmonize, Rich Mavoko, Queen Darleen, Mbosso na Lavalava, waliutendea haki ‘mradi’ huo.

Hata lebo ya Alikiba, Kings Music, nayo imewahi kuachia wimbo wa pamoja unaoitwa ‘Ndombolo’ huku wasanii kama King Kiba mwenyewe, Abdukiba, Lilly, Cheed, K2ga na Tommy Flavour wakiinogesha ngoma hiyo.

Pia mwaka uliopita Harmonize naye aliachia wimbo wa ‘Magufuli’ akiwa na wasanii wake wa Konde Gang. Ngoma hiyo inayoitwa Asante Magufuli ni miongoni mwa kazi zilizofanya poa sana kutokea kwenye lebo hiyo.

Mbali na hapa Bongo, huko mbele lebo kubwa kama Young Money Cash Money, imekuwa na utaratibu wa kuachia miradi mikubwa inayowakutanisha wasanii wa lebo hiyo na hakika zimekuwa zikifanya vizuri na hata kuziingizia fedha lebo hizo.

Miongoni mwa lebo zinazokuja juu kwa kasi kwenye ulimwengu wa muziki ni ‘Cutsleeve Records’, yenye asili ya Jamaica ila makazi yake ni nchini, imekuja kitofauti na lebo nyingine.

Mkurugenzi wa lebo hiyo, Jdart, ameweka wazi kuwa lengo la Cutsleeve Records ni kugusa nchi zote kwa kusapoti wasanii wa mataifa mbalimbali na kuwasimamia kwenye soko la muziki duniani.

“Lebo nyingi zimekuwa zinatoa wimbo mmoja ambao zimewashirikisha wasanii wanaowasimamia lakini kwetu ni tofauti. Sisi tumeachia albamu ambayo ina mkusanyiko wa nyimbo (audio na video) za msanii mmoja mmoja ambaye tunamsimamia na mradi huu unaitwa Cutsleeve Riddim ambao tayari umetoka,” amesema Jdart.

Jdart (pichani), ametamba kuwa Cutsleeve Riddim ni miongoni mwa miradi mikubwa ambayo imepokewa kwa kishindo na mashabiki wa muziki duniani kote, kwani namba za kila wimbo kwenye albamu hiyo zipo juu tofauti na matarajio yao.

“Cutsleeve Records tumetoa Cutsleeve Riddim kutoka kwa wasanii 20 wa mataifa sita, na tayari tumetoa video 11 na kati ya hizo zipo kazi za wasanii kutoka huko Afrika Mashariki nchini Tanzania, hii yote ni kuendelea kutanua wigo wa lebo yetu.

Jdart anasema ndani ya Cutsleeve Riddim, ana nyimbo mbili ambazo ni ‘Believe’ ambayo ina ujumbe wa 

kuhamasisha vijana kufanya kazi na kupambana bila kukata tamaa kwenye maisha pamoja na ‘Apologies’ , wimbo wa mapenzi kwenye ujumbe wa msamaha.

Jdart ameliambia gazeti hili kuwa kuwa lengo lake ni kubadilisha ulimwengu wa muziki kupitia Cutsleeve Riddim

 hivyo anaamini mashabiki wa mataifa mbalimbali watafurahia albamu hiyo iliyojaa ngoma kali.

“Tanzania ina vipaji vingi na sisi kama Cutsleeve Records tunawasimamia wasanii wawili ambao ni Madematrix na 

Lody Music, ambao huko Bongo wanafanya vizuri na katika Cutsleeve Riddim wamefanya vizuri sana kwani Madematrix ana wimbo unaoitwa ‘Show Me Love’ na ‘Lody Music’ ana ngoma yake inayoitwa ‘Sweet Love’,” amesema Jdart.

Ameongeza kwa kutaja wasanii wengine akisema: “Pia wasanii wengine ni Melodyne, Teejay, Chronic Law, Shatti, Int3ll, Jahvillani, Onsoundmynd, Cashan, Iquu, Zebee,  Jah Sam, Slyngaz, B.J Goldman, Iamstylez Music, Galiano, Shakespeare, D-Dondadda na Abijade, nawashukuru prodyuza ambao wamezalisha muziki na kusimamia huu mradi ambao ni maprodyuza wa Cutsleeve Records na Fraga kutoka hapo Tanzania.”

Jdart amevishukuru vyombo vya habari vilivyoibeba Cutsleeve Riddim mpaka kufikia chati kubwa za muziki duniani kama vile kupendekezwa na chati za Billboard kama Selector World Boom, jambo linalomuongezea nguvu ya kuendelea kusapoti vipaji kutoka mataifa mbalimbali.