DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Wiki iliyopita katika ukurasa huu, tulizungumzia namna ambavyo fedha za kuwekeza zinavyoweza kupatikana kwa jamii kuchangishana kwa lengo maalumu, na tukatazama faida zilizopo katika uwekezaji wa pamoja. Tuendelee na sifa za Meneja wa Uwekezaji wa Pamoja.

Huyu ni lazima awe mwangalifu kwa kufuata kanuni husika, mfano kuhakikisha gharama za uendeshaji hazivuki kiasi kilichokubaliwa na uwekezaji unafanyika ndani ya maeneo yaliyokubaliwa, si vinginevyo.

Mwekezaji anaungana na wawekezaji wengine kuwekeza kwa pamoja, hivyo kwa umoja huo kuwa na mtaji mkubwa unaowezesha kufanya mambo ambayo peke yake labda asingeweza kuyafanya.

Umoja huu una tija kwa kuwa huongeza nguvu na ufanisi katika majadiliano ya kibiashara; lakini pia ukimpa uhuru wa kuingia au kutoka wakati wowote kutokana na masharti ya mfuko husika.

Waliomo kwenye mfuko mmoja mara nyingi huwa na lengo moja; mfano waliopo Wekeza Maisha wanalenga kukuza mtaji, lakini Mfuko wa Watoto huwa ni kwa ajili ya elimu na maisha ya mtoto baada ya shule. 

Wanaotaka gawio la mara kwa mara wao hujiunga na Mfuko wa Hati Fungani au wa Jikimu, huku Mfuko wa Umoja wenyewe hukuza mtaji.

Katika kuanza kuwekeza si lazima mtu kuwa na fedha nyingi, hata Sh 10,000 tu inatosha kwa kuwa siri pekee ni kuendelea kuwekeza kwa kujiwekea mpango maalumu.

Unaweza kuamua kuwa unatenga kiasi fulani cha fedha kwa siku, wiki, mwezi au mwaka na kukiwekeza kama akiba ya baadaye. 

Jaribu kutenga asilimia 10 tu ya kila mapato yako utaona faida yake ingawa kwa wenye kipato kikubwa, kuwekeza kwa mkupuo kunawezekana.

Teknolojia ya mitandao, mfano simu, imerahisisha na kuokoa muda kwa mwenye nia ya kuwekeza kwani hakuna haja ya kwenda benki mara kwa mara; unawekeza kupitia kwenye simu yako na ni jukumu la Meneja kukupa taarifa za uwekezaji kila unapohitaji. 

Uzuri mwingine, mwekezaji akiwa na shida ya fedha, anaweza kutoa kiasi fulani na kuacha kingine kulingana na mahitaji yake, na muda wowote anaweza kuongeza tena uwekezaji. 

Nafasi nyingine murua ni ya mwekezaji kujipangia kiasi cha kulipwa kila baada ya muda fulani, ambacho meneja atakilipa kwa akaunti husika bila shaka yoyote, ingawa bado unaweza kuiacha faida inayopatikana iendelee kukupa faida zaidi.

Ukifanya upembuzi yakinifu, kwa haraka utakuta kuwa uwekezaji wa pamoja ni fursa nzuri kwa maisha ya baadaye na ukitumiwa vizuri utamsaidia mtu kutatua changamoto mbalimbali, hasa maisha ya kustaafu.

Ustaafu ni kama kuanza ukurasa mpya wa maisha na wakati huo fedha huhitajika kwa wingi, hivyo uwekezaji wa pamoja unaweza kuwa kama pensheni mbadala na hata zaidi ya pensheni.

Kuwa na malengo ni muhimu sana. Mfano lini uvune, upande mbegu mara kwa mara au mara moja, haya ni malengo ya kawaida kwenye biashara yoyote.

Ni muhimu pia kumfanya upembuzi meneja kwani huyu ndiye, baada ya makubaliano maalumu na ya kisheria, utakayempa fedha zako awekeze kwa niaba yako, huku ukiendelea na shughuli nyingine. 

Kama anaweza au hawezi utamjua kwa kuangalia utendaji wake. Mfano, je, anafikia malengo na vigezo vilivyowekwa na hata kuvizidi kwa kiasi gani? 

Kigezo kimojawapo ni asilimia ya chini ambayo mwekezaji anatarajia, je, anaifikia na kuizidi kwa kiasi gani? Na hii ni kila mwaka au?  Elimu ya meneja na wafanyakazi wake inaridhisha?

Kwa kawaida akaunti moja ni ya  mtu mmoja, lakini pia akaunti ya kikundi inaruhusiwa kwa kuwa uwekezaji huu ni wa mtu, watu na taasisi zote wakiwamo wafanyabiashara wadogo na wakubwa.

Kwa hakika huu uwekezaji ni rahisi na salama kwa asilimia kubwa ukilinganisha na uwekezaji mwingine wowote kutokana na muundo wake huku ukitoa nafasi kwa mwekezaji kumwandika mrithi anayemtaka.

Una ruhusu mlezi au mwangalizi kumwekezea mwenye umri chini ya miaka 18 na akifika wakati huo kumkabidhi kilichopo na akaamua kundeleza au kufika ukomo. 

Kumbuka kuwekeza na kutoa fedha ni rahisi. Ukishakuwa na akaunti unaweza ukawa unawekeza kwa simu, wakati wowote.  

Chukua hatua, jiulize kwanini uwekeze? Hii itasaidia kufanya tathmini kulinganisha faida na athari za iwapo ungeamua kuwekeza sehemu nyingine mbali na uwekezaji wa pamoja.  

Malengo yatakupa kigezo cha mfuko upi uwekeze, kwa kuangalia mfuko husika unawekeza wapi na wapi. Mfano muda ukiwa mrefu sana mfuko wenye hisa kama sehemu yake ya uwekezaji unaweza kutumika. 

Ila kama ni ya muda mfupi mfuko wenye kuwekeza zaidi ya asilimia 90 kwenye hati fungani utafaa zaidi. Hizi ni tathmini chache tu miongoni mwa nyingi. 

Mwekezaji anashauriwa kupata elimu ya kutosha kabla ya kufanya uamuzi na elimu kama hii hutolewa bure na UTT AMIS. 

Kwa maneno mengine ni vizuri Watanzania wakajipanua zaidi na kufanya uwekezaji kisasa. Ukiwa hauna fedha nguvu zako ndiyo mtaji, kama hauwezi kujiajiri ni lazima uwe mtumwa, yaani uajiriwe, ukiwa na fedha zako zinakufanyia kazi.

Pamoja na uwekezaji wa pamoja kuna huduma kama usimamizi wa mali/fedha. Hii huduma ni nzuri na ni njia ya kisasa kwa mwekezaji kumpa msimamizi fedha zake awekeze kwa ajili yake, yaani mwekezaji anampa meneja msimamizi mali, anasimamia huku akiratibu huduma mbalimbali kama wapi ziwekezwe na ushauri wa kodi.

Msimamizi hawekezi tu lakini pia anakuwa ndiye ‘bwana ushauri’ kwa mwekezaji huku akifanya tathmini ya hali halisi sokoni, mfano kuangalia uwezekano wa kukwepa dhoruba za uwekezaji na kuhakikisha faida zinapatikana. 

Yaani hapa mwekezaji anaweza kupata huduma kama usimamizi wa mali zake huku ukipata ushauri wa kitaalamu wa jinsi ya kuongeza uwekezaji wake kwa faida.

Katika huduma ya usimamizi wa mali, meneja ataangalia mtawanyo wa mali za mwekezaji, bajeti ya mwekezaji, hesabu zake, kodi na hata bima husika, kwa sababu meneja anajua, basi jukumu lake litakuwa kuhakikisha kuwa mali zinazoshikika na zisizoshikika zinawekezwa kwa ufanisi wa hali ya juu ili kuleta mapato makubwa. 

Huduma hii ya usimamizi wa mali  mara nyingi hulenga mashirika kama ya pensheni na watu wenye fedha nyingi. Kwa wale wenye fedha kidogo wataanza kwenye uwekezaji wa pamoja huku wakichanganya na shughuli zao nyingine ili kukuza mtaji ambao baadaye utawapa uwezo wa kuingia huku.

Kuna mambo makubwa mawili mwekezaji anatakiwa kuyafahamu, la kwanza nafasi ya meneja kwenye uwekezaji wake na pili mikakati ya meneja kuongeza rasilimali husika. 

Meneja atawekeza wapi, umuhimu wa hili ni kuwa utapata kubashiri faida au hasara, kwani kama meneja anawekeza kwenye kampuni ambazo hazisimamiwi vizuri na hazina biashara ya kutosha, hivyo basi kuleta hasara.

Tuwasiliane kwa 0712 625 310

By Jamhuri