Katika toleo lililopita, tuliona jinsi Mkapa anavyosimulia yale aliyoyafanya wakati akiwa rais. Tuliona, kati ya mambo kadhaa, jinsi ambavyo uundaji wa mamlaka za udhibiti ulivyomsaidia kuweka mambo sawa katika sekta mbalimbali. Endelea… 

Mheshimiwa Mkapa anaendelea: “Mashirika tuliyoyabinafsisha kama ambavyo nilivyofanya kwa Regulatory Agencies. Pia ni kweli kuwa tulibinafsisha kwa watu wa nje kuliko wazawa.”

Pamoja na ugumu na utata wa baadhi ya mageuzi, kura zake katika uchaguzi wa mwaka 2000 ziliongezeka kwa asilimia 100.  Hii kwake ilikuwa ni kuambiwa “Songa mbele, endelea.” “Na niliendelea,” anasema.

Mheshimiwa Mkapa anasimulia kuwa maono yake  ni maisha ya hali ya juu, amani, utulivu na umoja, utawala bora, jamii iliyoelimika na uchumi shindani wenye uwezo wa kukua kiendelevu na mgawanyo shirikishi wa kipato.  Ili kuyapata hayo, ikaanzishwa Vision 2025, MKUKUTA, MKURABITA, Mini Tiger Plan 2020 na TASAF. 

Anasema wengi katika Baraza la Mawaziri, kwenye chama na serikali hawakuviunga mkono.  “Lakini sasa naiona TASAF kama ‘High Point’ ya urais wangu,” anasema Mheshimiwa Mkapa. 

Vilevile anaelezea kuhusu Bima ya Taifa, mageuzi katika elimu, DEDP na SEDP, na mradi wa maji Ziwa Victoria.

Kuhusu mahusiano ya ndani na nje, Mheshimiwa Mkapa anabainisha  kuwa uhusiano katika ya Bara na Zanzibar ulikuwa mgumu na tete lakini alifanikiwa kutatua matatizo.

Anasema alikuwa na wasiwasi pale Rais wa Zanzibar, Salmin Amour, alipotaka kubadilisha sheria na kutawala kipindi cha tatu.  Lakini baadaye yeye na wafuasi wake wakaamua yaishe.

Zanzibar ilianza kupeperusha bendera yake.

Anasema vifo vya watu 22 huko Pemba Januari 2001 vilimshtua na kumhuzunisha sana.  Anasema: “Hili litaendelea kuwa doa katika urais wangu ingawa sikuwapo lilipotokea.”

Anabainisha kuwa wakati wa utawala wake, wanadiplomasia walionyesha upendeleo kwa vyama vya upinzani na kukutana nao mara kwa mara. Pia wapo walioamini walistahili upendeleo kuliko wengine.

Kwa upande wa vyombo vya habari anasema ilibidi azoee kukosolewa, kwani waliamini alikuwa dictator ingawa alikuwa anashikilia msimamo. Anabainisha kuwa alihitaji kuuza sera zake, kwa hiyo akaanzisha utaratibu wa kulihutubia taifa kila mwezi, lakini mhimili mkuu wa kupokea na kutoa mawazo na habari ilikuwa Chama chake CCM na vikao vyake mbalimbali.

Mheshimiwa Mkapa anakiri kuwa, kabla hajawa Rais, hakujua kuwa kazi moja wapo ya Rais ni kutoa pole.

“Moja wapo ya mapungufu yangu ni kwamba si mwepesi wa kuonyesha hisia zangu. Mrithi wangu Rais Kikwete ni mzuri sana katika hili,” anasema Mheshimiwa Mkapa.

“Mwaka 1996 mafuriko yalisababisha maafa makubwa katika nchi. Kuzama kwa Mv Bukoba kulishtua na kuhuisha sana majanga mengine mengi. Niliwahurumia wafungwa wote waliostahili kunyongwa mpaka kufa,” anasema.

Anasema ingawa hakatai kukosolewa kisiasa au kisera, kukosolewa binafsi kuliumiza sana.  Kwa mfano madai kwamba alimpendelea baba mkwe wa mwanae katika kubinafsisha mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira yalimuumiza sana.

Anasema pia madai kuwa aliwapendelea NET GROUP Solutions Ltd  wakati wa kubinafsisha TANESCO kwa sababu ya shemeji yake kulimuumiza sana. 

Pia jambo moja lililojitokeza baada ya Mheshimiwa Mkapa kumaliza muda wake ni la External Payment Account (EPA).

Mheshimiwa Mkapa anaeleza kuwa anavyoelewa urais wake haukuwa wa kwanza kuruhusu ununuzi wa madeni kama huo. Anasema kwanza alisita ila Gavana wa Benki Kuu, Daud Balali, alimuelewesha na akasema watakaonunua hayo madeni walikuwa tayari kuchangia mfuko wa kampeni za uchaguzi wa CCM. 

Anasema wahuni walitumia uaminifu wake kwa chama kumshawishi akubali. “Ninajisikia kuwa nilitumika na kusalitiwa. Na ukweli ni kwamba mimi binafsi sikufaidika na sikupata chochote,” anasema Mheshimiwa Mkapa.

“Kuna kukosolewa kuhusu matumizi ya anwani ya Ikulu wakati mimi na mke wangu tulipochukua mkopo NBC kununua nyumba. Ukweli ni kwamba wakati ule tulikuwa tunaishi Ikulu, tulichukua mkopo kwa mashart ya kawaida ya biashara.  Kabla sijaondoka Ikulu, nilimaliza malipo ya mkopo huo na mshahara wangu wa mwisho na mafao yangu, tukapewa hati ya nyumba hiyo,” anasema Mheshimiwa Mkapa.

Anasema kulikuwa pia na suala la Radar ambayo ilkuwa lazima kuinunua kuimarisha ulinzi lakini manunuzi yaligubikwa na udanganyifu na hatimaye fedha zilizolipwa za ziada zilirudishwa kwa serikali.

Anasema anafikiri ni muhimu kutazama upya suala la umiliki wa uchumi ili watu wengi zaidi wahusike. Kuendelea kushamiri kwa umiliki hasa wa viwanda na mashamba makubwa na makampuni ya Kiasia au Kihindi inaweza ikaleta wivu, na kuleta shida kubwa.  Ana wasiwasi na siku za mbeleni kwani umaskini huenda bega kwa bega na uvunjifu wa amani.  Anasema lazima tujiulize kama tunajikita katika utulivu na amani.

Anamalizia kwa kutoa ushauri kwa viongozi wa wakati ujao (future).

“Onyesha nia na bidii kwa majukumu upewayo. Uwe tayari kuwashirikisha wengine katika mawazo, mafanikio, matatizo na upimaji wa utekelezaji, consult more. Usifanye kazi kwa kukurupuka na kutotabirika. Fuata na tii sheria na taratibu. Uwe tayari kusikiliza. Mtafute mlezi (mentor) kama mimi nilivyokuwa na Mwalimu.

Katika sehemu anabainisha umuhimu wa mke wake Mama Anna Mkapa. Mapema kabisa katika ukurasa wa 83, Mheshimiwa Mkapa anampa saluti Mama Anna kwamba yeye ndiye gundi iliyoshikilia familia. Anakiri kuwa yeye Mheshimiwa Mkapa si mtu rahisi kuishi naye, na anamshukuru kwa kuwa mtu wa subira na uwezo mkubwa.

Anasema Mama Anna amevumilia mengi wakati wa safari za mara kwa mara, kutokuwepo nyumbani mara nyingi na ndiye alibeba mzigo wa kuwalea watoto wao wawili.

4. Kustaafu

Sehemu ya tatu na ya mwisho ya simulizi hii, ni maisha ya Mheshimiwa Mkapa baada ya kustaafu urais.

Kwanza, Mheshimiwa Mkapa ametumika sana kimataifa katika nyadhifa na taasisi mbalimbali ingawa hapendi kusafiri. Taasisi hizo ni pamoja na Club de Madrid, The African Wildlife Foundation, Investment Climate Facility for Africa, UN Iniative “Delivering as One”, UNCTAD Panel of Environment Persons, UN Commission on the Legal Empowerment of the Poor, Mwenyekiti wa Seventh Centre tangu mwaka 2006, Trustee the Aga Khan University na The Mkapa Foundation. Kote huko amejichanganya na watu wenye akili nyingi.

Pili, amehusika sana katika upatanisho wa migogoro huko South Sudan, Congo Mashariki na Kenya.

Mheshimiwa Mkapa anamalizia simulizi hii kwa kugusia mambo kadhaa.

Kwanza, anaona Rais mstaafu anathaminiwa zaidi uongozi na uwezo wake kimataifa zaidi kuliko nyumbani, jambo ambalo hata Mwalimu aliliona. Mara nyingi huitwa kwenye hafla ambapo anakuwa kama ua au pambo ukutani, lakini anatakiwa kwenye kazi muhimu na nyeti za kitaifa.

Pili, anaongelea umuhimu wa kuanzishwa kwa baraza dogo kama sehemu ya Bunge kupitia miswada iliyopitishwa na Bunge kabla ya utekelezaji. 

Tatu, anazungumzia kukosekana kwa itikadi na fikra pevu za kina juu ya mustakabali wa taifa letu.  Inabainishwa kuwa tunahitaji ukombozi wa pili, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. 

Tunahitaji kama taifa, na mtu mmoja mmoja kuona aibu kuwa ombaomba. Tunahitaji kujitegemea na kuthamini uendelevu (sustainability) wa maendeleo.

Nne, anagusia mwendo wa goigoi katika kuimarisha Jumuia ya Afrika Mashariki (EA). Anasema: “Sioni juhudi kubwa, naona siasa tu, watu wamepoteza picha kubwa – Big Picture”.

Tano, anagusia uongozi. Anabainisha kuwa uongozi bora ni kipaji au karama na sayansi pia. Unazaliwa na karama hizo lakini unajifunza pia. Nia yaani commitment ni muhimu. Kiongozi bora ni lazima awe mfano wa kuigwa katika utendaji kazi wake, uaminifu na uadilifu.

Anatilia mkazo suala la ongezeko la vijana na kwamba hakuna sera, ya namna ya kushughulikia ongezeko kubwa la watu.  Anagusia pia suala la siasa halaiki, yaani populism na athari zake.

Kuhusu siasa na demokrasia, anabainisha kuwa CCM bado inajiona kama bado ipo kwenye siasa za chama kimoja.  Anasema kunahitajika more political interaction na engagement.

Mheshimiwa Mkapa anaendelea kubainisha kuwa uwepo wa vyama vingi vya siasa unadhoofisha demokrasia. Watu wanaingia katika siasa kusaka manufaa ya kiuchumi si kwa nia tukufu ya kuwatumikia watu na taifa. 

Wafanyabiashara wanasaka na kulinda masilahi, wasomi hutafuta kusafiri na posho, wabunge wachache wanajali masilahi ya jimbo, wengi wanapenda safari za nje. Hakuna interaction ya wabunge kuhusu sera na utekelezaji wake.

Mwisho, Mheshimiwa Mkapa anajiuliza kama tutaweza kudumisha amani na umoja wetu kama taifa. Anagusia kuibuka hapa na pale viashiria vya ukabila, udini, na ukanda.

Mwisho kabisa, Mheshimiwa Mkapa anamalizia kwa kusema: “Nitamuachia Mungu wangu na nyinyi kuamua ni tofauti gani nimeifanya humu duniani.”

678 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!