Ndugu Rais, kitabu kilichoandikwa na Rais mstaafu Benjamin William Mkapa kimezinduliwa. Kwa mipango ya Mungu ulikizindua wewe mwenyewe. 

Ninasema ni mipango ya Mungu kwa sababu sisi wote tuna nafasi ya kuelewa alichokiandika Benjamin William Mkapa, lakini kwa kuwa baba ndiye umekalia kiti alichokuwa amekalia mwandishi, tunakuona una nafasi zaidi ya kuelewa na kujifunza na ikiwezekana kuyafanyia kazi maandiko hayo.

Kitabu kimezinduliwa wakati huu nchi inapopitia katika sintofahamu ya kinachoitwa uchaguzi wa serikali za mitaa. Ni sasa ambapo kilio kinasikika nchi nzima kwa bei ya unga wa mahindi kupanda sana huku bei ya mafuta ikipaa kupitiliza. Wananchi wanazidi kupigika.

Mkapa anakumbukwa kwa bei ya unga kilo moja aliyotukuta nayo wakati anaingia katika urais na akatuacha nayo bei ikiwa hiyo hiyo baada ya kuwa amekaa madarakani kwa miaka kumi. Pia alituacha na nauli ya daladala ya Sh 200 aliyotukuta nayo miaka kumi iliyokuwa imepita. Yako mema mengi aliifanyia nchi hii na watu wake, makubwa kwa madogo, ambayo leo anajivunia katika kitabu chake.

Labda ni kwa sababu mzee Kikwete alikuwa bado hajatuletea msamiati wake wa kujimwambafai, leo tunaweza kusema kwa uhakika kuwa Rais Benjamin William Mkapa hakujua kujimwambafai.

Kujimwambafai ni kujikweza kwa wenye mapungufu mengi au makubwa wakidhani kwa kufanya hivyo ni kujiinua. Acha unaowaongoza ndio wakuinue. Anayejiinua mwenyewe hujidhalilisha sana katika vifua vya watu wake anaowaongoza. Na kwa sababu hiyo jamii hutamani watu hao wapite kwa amani na kwa haraka.

Mkapa alikuwa rais mkali, aliyeamini katika ukweli na uwazi. Yanayosemwa sasa juu yake ni historia. Lakini historia ni zaidi ya njia iliyoachwa kwa ajili ya uzamani wake kwa sababu ina mengi yanayousababisha usasa uwe hivi ulivyo na kuumba au kuutengeneza ubaadaye!

Mkapa anaandika kuwa akiwa katibu wa Rais Nyerere walitumia muda wao mwingi wakifanya kazi kwa mikono yao katika shamba la mahindi kila walipokuwa Butiama kijijini kwao.

Ala! Kumbe Rais Julius Kambarage Nyerere alikuwa na kwao? Nyerere hakukufanya kwao kuwa mzigo wa taifa au kuwa mzigo wa Watanzania. Rais Nyerere katika hili alitofautiana hata na marais wenzake kama Rais Mobutu Sese Seko wa Zaire ambaye alitamani kukigeuza kijiji alichozaliwa kuwa Bustani ya Eden. Baada ya kuwa si rais tena, Badolite, kwa laana ya Muumba na laumu ya wananchi maskini, kimekuwa ni zaidi ya mahame.

Ala, kumbe!  Angalau katika hili Rais Benjamin William Mkapa alionyesha kwa vitendo kile alichorithi kutoka kwa Baba wa Taifa, Rais Nyerere. Benjamin William Mkapa kumbe naye alikuwa na kwao. 

Naye kwao hakukuwahi kuwa mzigo mzito kwa Watanzania. Hivi karibuni Watanzania wameshuhudia hata shule aliyosoma baada ya kuonekana imechoka sana imewalazimu wadau waichangie kama wanachangia harusi. 

Maandiko yaliyomo katika kitabu hiki yatuwezeshe kuelewa ukubwa wa dhambi ya umimi. Kuutukuza umimi wetu ni kumfanyia chukizo Mwenyezi Mungu.

Umimi ni dhambi kubwa kwa sababu unawatesa wananchi wengine kwa manufaa ya ubinafsi tu!

Rais mstaafu Benjamin William Mkapa katika maandiko yake ameainisha aliyotufanyia Watanzania kwa ustawi wetu na kwa ustawi wa nchi yetu. Pamoja na mema yote hayo ameainisha pia na yale aliyoyafanya yanayomfanya leo aonyeshe kuyajutia.

Tunao baadhi ya viongozi ambao kwao kukosea ni mwiko, hivyo kumkosoa anakuona unatenda dhambi kubwa. Wapo viongozi hawajui kusema samahani. Kila anachofanya yeye ni chema, tena chema sana hata kwa yale yanayowafanya wananchi wawe na maisha magumu zaidi.

Kiongozi bora ni yule anayeyapima anayowafanyia wananchi kutokana na kuridhika kwao, si kuridhika kwake yeye. Tunapaswa kujifunza kutokana na unyofu aliokuwa nao muasisi wa taifa hili Mwalimu Nyerere, kuwa pamoja na mema yote aliyoifanyia nchi hii na makubwa aliyowafanyia Watanzania kama kuwafanya wajione ni ndugu, na wamoja, akawajengea upendo na mshikamano, hivyo kuwafanya wawe na amani ya kweli, vitu ambavyo marais wote wa dunia hii hawajafaulu kuwafanyia wananchi wao katika nchi zao, lakini mtu wa Mungu yule hakuwahi kujiuliza hadharani au kuwauliza Watanzania kama kuna mtu atakuja kuyafanya hayo makubwa iwapo yeye atakuwa hayupo au hatakuwa ni rais. 

Aliamini kuwa wote watakaokuja nyuma yake watakuwa ni viongozi wenye utu wa kuthamini utu wa binadamu wengine kama wanavyothamini utu wao wenyewe.

Nyerere aliamini katika utu wa watu, si katika vitu. Bado ninaamini kwa fikra za Mwalimu Nyerere ambazo timamu wengi wanaziheshimu, haya makubwa yote tunayojimwambafai kwayo, kwake asingeyaita maendeleo, kwa sababu katika fikra zake maendeleo ni lazima yawe ni yale yanayowagusa watu.

Hata katika mitandao ya siku hizi Nyerere bado anasema kama alivyosema zamani kuwa watu kwetu maana yake ni wakulima. Ni lipi katika haya makubwa tunayoyafanya yanayowagusa wakulima ambao ndio watu kwa fikra sahihi za Baba wa Taifa? Kujimwambafai si dhambi, lakini kwa haya Baba wa Taifa kama anayaona anatushangaa tunapojimwambafai.

Kati ya mambo anayoyajutia Mkapa leo, ni uamuzi wake na vijana wake mawaziri walipolazimisha kuziuza nyumba za serikali. Kujutia kwake katika hili kunamuonyesha jinsi anavyomtanguliza Mungu kutokea moyoni mwake. Angetokea wa kutofautiana na wazo hili ovu, leo huyo angetukuka mbele ya wananchi na mbele ya Mkapa mwenyewe. Lakini wako viongozi hawajui kusema samahani tulikosea.

Mkapa, Rais mstaafu lakini pia Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi mstaafu, anasema chama hicho wanadhani nchi bado ni ya chama kimoja. Anakikosoa chama. Lakini chama si majengo wala mafaili. 

Chama ni wanachama chini ya mwenyekiti wao. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na viongozi wenzake walioko sasa wakubali kuwa wanaokosolewa ni wao. Wabadilike!

Yawezekana tumemtukuza mno shetani na mambo yake kiasi kwamba ametufanya tusione umuhimu wa Katiba mpya ambamo humo tungepata Tume Huru ya Uchaguzi. Lakini hapa ulipofikia uchaguzi wa serikali za mitaa unamlazimisha kila timamu kukubali kuwa sasa Tume Huru ya Uchaguzi ni lazima, vinginevyo amechagua machafuko katika nchi. Tumuogope mtu huyo kama ukoma!

By Jamhuri