Tanzania inaongoza miongoni mwa nchi 15 duniani ambazo zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa kupunguza idadi ya watu wanaoishi kwenye umaskini wa kupindukia.

Hayo yamebainishwa na Benki ya Dunia ambayo inasema kuwa Tanzania imeibuka kidedea baada ya kuwa na matokeo mazuri kati ya mwaka 2000 na 2011 kwa kufanikiwa kuondoa watu zaidi ya milioni tano kwenye umaskini uliokithiri.

Mafanikio haya yamezidi kuongezeka hasa miaka ya hivi karibuni kama ilivyobainishwa na Utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi kwa Tanzania Bara wa Mwaka 2017/18, uliochapishwa Juni mwaka huu.

“Kati ya 2000 na 2011, umaskini wa kupindukia ulipungua kutoka asilimia 86 hadi asilimia 49.1 nchini Tanzania kwa kiwango cha wastani wa asilimia 3.2 kwa mwaka na kusababisha punguzo la Watanzania milioni 5.3 kutoka kwenye umaskini uliokithiri,” Benki ya Dunia imesema.

Orodha ya taasisi hiyo ya fedha duniani inaonyesha kuwa saba kati ya nchi zilizofanya vizuri zinatoka Afrika – kusini mwa Jangwa la Sahara zikiwemo pia Chad ambayo ni ya tatu duniani na Jamhuri ya Kongo iliyo kwenye nafasi ya nne.

Nyingine ni Burkina Faso (ya tisa), DR Congo (ya 10), Ethiopia (ya 13) na Namibia (ya 15). Mataifa mengine ni Tajikistan (ya pili), Jamhuri ya Kyrgyz (ya tano), China (ya sita), India (ya saba), Moldova (ya nane), Indonesia (ya 11), Vietnam (ya 12) na Pakistan (ya 14).

Benki ya Dunia, ambayo moja ya majukumu yake makubwa ni kuhakikisha watu wanaoishi kwenye umaskini wa kupindukia duniani hawafiki asilimia tatu ifikapo mwaka 2030, irishirikisha nchi 114 katika utafiti huo wa kubaini vinara wa kupambana na kupunguza maisha duni.

Nchi zilizoshirikishwa kwenye utafiti huo ni zile ambazo zimefanya utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi angalau mara mbili katika miaka ya hivi karibuni, mmoja ukiwa ni kati ya mwaka 1995 na 2005 na mwingine kati ya 2010 na 2019.

Utafiti wa Tanzania Bara wa mwaka 2017/18 ulikuwa utafiti wa tano kufanyika kisayansi nchini katika mfululizo wa tafiti zilizofanyika nchini tangu mwaka 1991/92. Matokeo yake yanaonyesha kuwa umaskini wa mahitaji ya msingi ulipungua kutoka asilimia 28.2 mwaka 2011/12 hadi asilimia 26.4 mwaka 2017/18. Vilevile, kiwango cha umaskini wa chakula kilipungua kutoka asilimia 9.7 mwaka 2011/12 hadi asilimia nane mwaka 2017/18.

“Utafiti wa HBS 2017/18 unaonyesha kuwa wastani wa matumizi ya kaya moja kwa mwezi kwa Tanzania Bara ni Sh 416,927. Kiwango hiki cha matumizi ni kikubwa kwa maeneo ya mijini (Sh 534,619) kuliko maeneo ya vijijini (Sh 361,956),” Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) inaeleza kwenye utafiti huo.

279 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!