Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Abubakari Kunenge amekemea vikali vitendo vya ukatili vinavyoendelea kushamiri ndani ya mkoa huo baada ya Neema John , kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi baada ya kufanyiwa ukatili na mumewe kwa kupigwa na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kumwagiwa maji ya moto na kukimbia kusikojulikana.

Akielezea tukio hilo,Kunenge amesema kuwa tangu kufanyika kwa kitendo hicho ni siku ya 10 ambapo mtuhumiwa alikimbia na kumwacha mkewe akiwa na majeraha makubwa yaliyotokana na kipigo hicho huku akimwacha na watoto wanne akiwemo mtoto mchanga wa siku 26.

Kutokana na ukatili huyo, RC Kunenge ameitaka Ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Pwani kulibeba suala hilo na kumsaidia mwanamke huyo hadi atakapopona.

“Vitendo hivi ni vya hovyo kabisa, huu ni sawa na uuaji kwani kumpiga mkeo namna hii,ni kwamba amedhamiria kumuua, vyombo vya sheria vimsake na kumchukulia hatua kali ili fundisho kwa wengine” amesema.

Ametoa rai kwa wanawake na jamii kwa ujumla kuacha kuficha viashiria vya matendo ya ukatili kwani vinachangia vifo na hata ulemavu.

Kunenge amewataka viongozi wa dini, Serikali,kijamii, vyama vya siasa, kuendelea kutoa elimu kwa jamii, kuhusiana na kuacha vitendo hivi vya kikatili ambavyo haviendani na sera, sheria,kanuni na mila na hata desturi za nchi yetu.

Hata hivyo amewaasa watendaji wa ustawi wa jamii pamoja na mkoa kuacha kukalia taarifa za aina hiyo, wazitoe kwa wakati pasipo kuficha ili ofisi yake izifanyiwe kazi.

“Haiwezekani vitendo hivi vinatokea, taarifa mnazipata mitandaoni,mtu anapelekwa Kituo Cha afya Mlandizi,Tumbi, Serikali hamjui,mnasubiri kutumiwa picha mitandaoni, haiwezekani, mnasubiri mkuu wa mkoa ndio nifuatilie wajibu wenu.

“Mimi nitashughulikia mambo mangapi,kwa hili nitawashughulikia na kuwajibisha wale wote waliohusika kwa namna moja au nyingine”Inakera yaani RC nitoke ndio nishughulikie wajibu wenu, na atakayebainika kuhusika kuzembea nitamwajibisha kwa hili,”amesema Kunenge.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Pwani Pius Lutumo amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kusema bado mhusika hajapatikana ,Jeshi la Polisi linaendelea na msako.

“Ujue hawa wafugaji huwa wanatabia ya kufanya tukio na kukimbilia maporini ,lakini licha ya hilo tupo kazini na tutahakikisha tunamkamata “amesisitiza Lutumo.

Lutumo ameitaka jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi, na wenye ndoa kuacha kufanya ukatili kwa wenza wao kwani kwa kufanya hivyo ni ukiukwaji wa haki ya binadamu.

Kwa upande wake mwanamke aliyefanyiwa ukatili Neema John akiwa Hospital ya Rufaa ya Mkoa ya Tumbi kwa matibabu ameeleza anashukuru kupata matibabu na anaendelea vizuri kidogo.

“Kosa langu lilikuwa kuchelewa kuwasha moto ndipo mume wangu akaamua kunipiga kiasi hiki mgongoni,usoni na kunimwagia maji ya moto mapajani na mguuni”amesema Neema kwa uchungu.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Gunini Kamba, amesema mgonjwa huyo alipokelewa akitokea Mlandizi lakini sasa anatibiwa Hospital ya Tumbi na wanashukuru anaendelea na matibabu.

Kaimu Mganga Mkuu Mfawidhi Hospital ya Rufaa ya Mkoa Tumbi,Dkt.Devotha Julius amesema Neema kiafya anaendelea vizuri na bado yupo kwenye matibabu.

“Hata hivyo kumekuwa na wagonjwa wanaofikishwa hospitalini hapo kupata matibabu kutokana na kufanyiwa ukatili kati ya watatu hadi wanne kwa mwezi hivyo bado elimu inatakiwa kuwa endelevu ili kupunguza matukio ya ukatili,’ amesema.

By Jamhuri