Na Mwandishi Wetu ,JamhuriMedia, Mbeya

Mwanaume mmoja aitwaye,Ombeni Kilawa (43,) mkazi wa Kijiji cha Lusese, Kata ya Igurusi wilayani Mbarali anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kwa tuhuma za kumuua mke wake kwa kumchinja na kisu shingoni .

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya Kamshina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi,Benjamin Kuzaga amemtaja marehemu aliyeuwawa kuwa ni Happynes Mwinuka ((40) ambaye naye ni mkazi wa Kijiji cha Lusese wilayani humo.

Happynes Mwinuka ((40), enzi za uhai wake

Aidha Kamanda Kuzaga amesema kuwa tukio hilo limetokea Machi 13, mwaka huu, katika kitongoji cha Masista Kijiji cha Lusese wilayani Mbarali.

Akielezea zaidi Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya Benjamin Kuzaga amesema kuwa mauaji hayo yalitokea baada ya kuzuka ugomvi wa baina ya wanandoa hao wakiwa nyumbani kwao na kupelekea mtuhumiwa Ombeni Kilawa ambaye ni mume wa marehemu kuchukua kisu na kimkata mke wake shingoni na kupelekea umauti .

Hata hivyo inaelezwa kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa kimapenzi baada ya mtuhumiwa kumhisi na kumtuhumu mke wake kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume wengine.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, linatoa wito kwa jamii kuwa pindi wanapopatwa na tatizo au changamoto katika ndoa zao isiwe suluhisho lake kujichukulia sheria mkononi.

Kuzaga amesema kuwa kitu muhimu ni kutafuta ushauri kwa wazazi, walezi, wasimamizi wa ndoa, viongozi wa dini, katika madawati ya jinsia na watoto waliopo kila Wilaya ya Kipolisi, katika ofisi za halmashauri au kutafuta haki kwenye Mahakama ili kuepuka madhara.