Mvutano unaendelea kati ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na wafanyabiashara wenye maduka katika Jengo la Biashara la Stendi Kuu ya Mabasi mjini Moshi.

Mvutano huo unahusu mkataba mpya wa upangaji baada ya ule wa awali wa miaka 15 kumalizika Desemba 30, mwaka jana. Wafanyabiashara wanapinga ongezeko kubwa la kodi.

Jengo hilo la ghorofa tatu lilijengwa kwa ubia na wahisani – Benki ya Dunia (Sh 139,009,423), Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) [Sh milioni 35] na Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL) [Sh milioni 3.71]. Lilizinduliwa mwaka 2013.

Katika ujenzi huo, Manispaa ya Moshi ilikaribisha wadau ambapo kati ya wananchi 600 walioonyesha nia ya kuchangia ni 126 waliojitokeza.

Walichangia kati ya Sh milioni 4.5 na Sh milioni 12 kutokana na ukubwa wa chumba cha biashara na baada ya kukamilika kwa ujenzi huo walianza kulipa Sh 20,000 kwa vyumba vilivyopo ghorofani na Sh 30,000 kwa vyumba vya chini.

Makubaliano yalikuwa wafanyabiashara hao kulipa kiasi hicho cha fedha kwa miaka 15; na baada ya muda huo jengo hilo lilitakiwa liwe mali ya manispaa.

Baada ya mkataba kumalizika Desemba 30, mwaka jana manispaa ambayo ndiyo mmiliki, imekaribisha wawekezaji wapya kwa bei mpya ya pango, lakini wafanyabiashara wachache wakiungwa mkono na wanasiasa wanagomea hatua hiyo.

Kodi mpya iliyotangazwa na manispaa ni Sh 450,000 kwa vyumba vya juu na Sh 500,000 kwa vyumba vya chini ambavyo vimekuwa lulu kwa wafanyabiashara wengi.

Hoja yao ni kwamba viwango vipya vya kodi ni vikubwa na havilipiki, lakini ni hao hao wafanyabiashara ambao wamekuwa wakilipa kodi ndogo ilhali wao wakiweka wapangaji kwenye vyumba hivyo kwa malipo makubwa.

Imebainika kuwa wafanyabiashara kadhaa walioingia ubia na manispaa hawafanyi biashara kwenye vyumba hivyo, bali wamevipangisha kwa wastani wa Sh 300,000 hadi Sh 600,000 kwa mwezi.

Please follow and like us:
Pin Share