‘Mwaka 2030 utakuwa ukomo magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele’

Na WAF – Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendeleza juhudi za ugawaji wa dawa na matibabu kwa wagonjwa wa magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ili ifikapo 2030 magonjwa hayo yaweze kutokomezwa.

Hayo yamesemwa leo na Meneja Mpango Wa Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Dkt. George Kabona wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya Kampeni na mkakati wa kutokomeza magonjwa hayo kwenye ofisi ndogo za Wizara ya Afya UDOM Jijini Dodoma.

Dkt.Kabona amesema katika wiki hili la magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele huduma zinaendelea kutolewa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Mkoa wa Tanga, Dodoma na Arusha.

“Tanzania tunaadhimisha kwa kufanya matukio ya utoaji wa huduma ya upasuaji wa Mabusha, tumeweka kambi za kuzawazisha vikope na utoaji wa elimu unaendelea.” amesema Dkt. Kabona.

Dkt.Kabona amesema Mwaka huu wamepanga kutoa huduma ya upasuaji wa mabusha (Operation) kwa watu 350 Katika Mkoa wa Tanga na watafika mpaka Mkoa wa Mtwara ili kuendelea kutoa huduma hiyo.

Katika hatua za utokomezaji wa magonjwa hayo Dkt.Kabona amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupata matibabu ya magonjwa hayo kwenye kambi za matibabu pamoja na umezaji wa dawa.

Kwa upande wake Afisa Mpango wa Taifa Wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Bw. Oscar Kaitaba amesema Ugonjwa wa matende na mabusha hauna uhusiano wowote na ulaji wa madafu kama watu wanavyodhania bali huenezwa na Mbu wa aina zote.

“Watu wanakula madafu wanaacha vifuu kwenye mashamba ambapo maji yanapotuhama hupelekea mazalia ya Mbu ambapo Mbu hao wakimuuma mtu anapata Ugonjwa Huo.” amesema Bw. Kaitaba.

Afisa huyo amesema katika tafiti iliyofanyika Awali, Ugonjwa huo ulikuwa katika Halmashauri 119 hapa nchini na walifanikiwa kugawa dawa katika Halmashauri zote.