Na WAF – Dodoma

Tafiti zinaonesha kuwa kiwango cha vifo vya watoto chini ya miaka mitano kwa Mwaka 2022 kimefika vifo 43 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai ukilinganisha na vifo 67 kwa kila Watoto 1,000 waliozaliwa hai ilivyokuwa kwenye Utafiti uliofanyika mwaka 2015/2016.

Hayo yamesema jana na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kwenye uzinduzi wa matokea muhimu ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania wa Mwaka 2022 uliofanyika katika ofisi za Taifa ya Takwimu Jijini Dodoma.

“Na kwa upande wa kiwango cha vifo vya watoto wachanga kabla ya kutimiza mwezi mmoja vimepungua kutoka vifo 37 mwaka 1990 hadi vifo 18 mwaka 2021 kwa kila vizazi hai 1,000 ambapo vimepungua kwa asilimia 51.” Amesema @ummymwalimu

Pia, Waziri Ummy amesema Vifo vya Watoto chini ya mwaka mmoja navyo vimepungua kutoka vifo 65 mwaka 1990 hadi vifo 28 mwaka 2021 kwa kila vizazi hai 1,000 ambapo kwa jumla ni punguzo la asilimia 56.

“Haya ni matokeo makubwa ya juhudi zinazofanywa na Serikali katika utekelezaji wa malengo tuliyojiwekea katika mpango wa Tatu wa maendeleo ya Taifa ambao unalenga kupunguza vifo vya Watoto chini ya umri wa miaka mitano hadi vifo 40 katika kila watoto 1,000 wanaozaliwa hai ifikapo mwaka 2025/26.” Amesema Waziri Ummy

Katika kuonesha umuhimu wa Tafiti Waziri Ummy amesema matokeo haya muhimu ya Utafiti yataiwezesha Serikali ya awamu ya Sita inayoogozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na wadau mbalimbali kufuatilia na kutathmini malengo yaliyofikiwa katika mipango ya maendeleo ya kitaifa, kikanda na kimataifa hasa katika eneo la Afya ya Uzazi na Mtoto.

“Utafiti huu ni moja kati ya tafiti muhimu katika sekta ya afya kwani hutoa tathmini ya ubora wa huduma zinazotolewa nchini, changamoto zilizopo katika sekta ya afya na kushauri namna ya kukabiliana nazo.” alisema Waziri Ummy.

Aidha, Waziri Ummy amesema kwa Tanzania kiwango cha udumavu (urefu kwa kulinganisha na kigezo cha umri) kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano (5) kimeendelea kupungua kutoka asilimia 34 kwenye Utafiti wa mwaka 2015/16 mpaka asilimia 30 kwenye Utafiti wa mwaka 2022.

“Kwa mwaka 2022 matokeo yanaonesha asilimia 3.3 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano (5) wana ukondefu (wembamba kwa kulinganisha na kigezo cha urefu wao) ikilinganishwa na 4.5% kwa Utafiti wa mwaka 2015/16.” alisema Waziri Ummy.

Hata hivyo Waziri Ummy ameitaka mikoa ambayo inaongoza kwa Udumavu na Ukondefu kuiga juhudi zinazofanywa na mikoa mingine ili kupunguza magonjwa hayo.

By Jamhuri