Aliyekuwa Mwalimu wa shule ya msingi Livingstone Erick Mbilinyi Mkazi wa Mtaa wa Mgendela Halmashauri ya Mji wa Njombe ameuawa na watu wenye hasira kali baada ya kupigiwa makelele ya “mwizi”.

Baadhi ya Waombolezaji pamoja na majirani waliohudhuria msibani na wakati wa mazishi ya Mwalimu huyo, wamesema wamehuzunishwa na kitendo cha kujichukulia sheria mkononi kilichofanywa na baadhi ya Wananchi bila kujiridhisha zaidi kwakuwa Mbilinyi hakuwa na tabia za ajabu.

Katibu Tarafa wa Njombe Mjini Liliani Nyemele kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Njombe Kissa Kasongwa ameonya Wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi.

“Tulipokea taarifa hizi zenye huzuni Jumapili usiku, tukio hili lisijirudie tena, Mwalimu amefariki bila hatia, Polisi Kata wamekuwa wakitoa elimu kupitia mikutano yetu nini cha kufanya juu ya Mtu unayemtilia shaka, tungekuwa tunayaishi maelekezo tusingefika hapa yaani tumekuwa wote sasa Wanasheria na kudhani kila Mtu unayemuona ni Mhalifu hiyo hapana, niwaombe sana tuwe watulivu kwa kipindi hiki tunachokipitia”

Mwalimu Erick Mbilinyi alifariki dunia Novemba 20, 2022 baada ya kuuawa na Wananchi wenye hasira alipoitwa mwizi mara baada ya kuingia katika moja ya nyumba mjini humo kwa kuwa alikuwa na tatizo la kiakili hali ambayo humtokea mara kwa mara.

Jeshi la Polisi Njombe linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo huku Watu kadhaa wakiwa tayari wameshikiliwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.

By Jamhuri