Na Severin Blasio,JamhuriMedia,Morogoro

Mwanasheria wa Halmashauri ya Morogoro wakili Hella Mlimanazi ameshangazwa kuwepo kwa baadhi ya mabaraza ya kata kwenye halmashauri hiyo kufanya mashauri bila kupata mafunzo sambamba na kuapishwa.

Pia baadhi ya mabaraza hayo yamekuwa yakifanya kazi bila kuhuishwa(renew) kwa kupitisha muda uliowekwa kisheria ambao ni miaka mitatu.

Wakili Mlimanazi alibaini hayo alipokuwa kwenye muendelezo wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa mabaraza ya ardhi ya kijiji na kata kwa ajili ya utatuzi wa migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi katika halmashauri ya wilaya hiyo iliyoandaliwa na asasi ya UMWEMA kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society (FCS).

Akitoa mada ya uendeshaji wa mabaraza kwenye kata ya Bwakira juu wakili Mlimanazi alibaini changamoto hiyo kwa wajumbe wa baraza la kata hiyo kisha kulazimika kuwaapisha ili waweze kufanya kazi kisheria.

“Kwa kuwa mmeniambia toka mchaguliwe hamjaapishwa,nawaapisha rasmi ili maamuzi yenu yawe ya kisheria.Nendeni mkawahudumie wananchi kiuadilifu ikiwa ni pamoja na kuwa na siri” amesema Wakili Mlimanazi.

Amesema kuwa mabaraza hayo yapo kisheria na ni wajibu kwa wajumbe kutenda haki ili kuondoa migongano na kwamba fursa waliyopata ya mafunzo waitumie vizuri kwa mstakabali wa taifa.

Nao Washiriki wa mafunzo hayo walishukuru asasi ya UMWEMA kwa kutoa elimu hiyo na kwamba kupitia mafunzo hayo wameahidi kutumia elimu hiyo kwa makini ikiwa ni pamoja kufuata sheria zinazoongoza mabaraza.

“Kwa niaba ya wajumbe tulioshiriki natoa shukurani kwa UMWEMA kutuletea mafunzo haya..Lakini nitoe wito kwa asasi nyingine kuja huku kuendelea kutuelimisha” amesema mjumbe wa baraza Cosmas Matinga.

Awali mratibu wa mradi wa asasi ya UMWEMA Restuta Ngonyani amesema katika utekelezaji wake asasi hiyo ilifanya tathmini ya hali halisi ya migogoro ya ardhi kwenye baadhi ya kata zilizopo halmashauri ya Morogoro abazo ni Kisaki,Bwakira juu na Selembala wakabaini uwepo wa changamoto mbalimbali katika vyombo vya utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Ngonyani ametaja moja ya changamoto hizo kuwa ni kuta maamuzi ya kesi katika mabaraza bila kufuata sheria kutokana na wajumbe hao kukosa elimu ya uendeshaji wa mabaraza hayo na hivyo kusababisha kuongeza migogoro badala ya kuimaliza.

By Jamhuri