Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma watimize wajibu wao kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia wafanye pindi anapowateua ama kuwapa ajira.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuona watumishi wa umma mkiwatumikia Watanzania. Nenda kwa wananchi mkawasikilize. Huwezi kuwahudumia bila kuwasikiliza na huwezi kujua changamoto zao bila kuwasikiliza,” amesema.

Ametoa wito huo leo mchana (Jumatano, Oktoba 19, 2022) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa, wilaya na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kwenye ukumbi wao mara baada ya kuzindua jengo la Halmashauri hiyo.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Viongozi wakati alipowasili kwenye eneo la hospitali ya halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali hiyo mkoani Ruvuma, Oktoba 19, 2022.

Amewataka viongozi na watumishi hao wafanye kazi kwa kulenga matokeo. “Nataka tufanye kazi kwa matokeo, tufuate maelekezo na tuzingatie nidhamu. Tuna fedha za ndani na za Serikali Kuu. Tuzisimamie vizuri na naomba msijiingize kwenye matumizi mabaya ya fedha hizo,” aliwaonya.

Waziri Mkuu aliwapa mfano wa Mkuu wa shule ya sekondari Irugwa ambaye alipokea sh. milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa sita, lakini alizisimamia vizuri akamaliza madarasa, akajenga matundu matano ya vyoo, kuweka mfumo wa maji ya mvua na chenji iliyobakia akapiga lipu mabweni ya wasichana na kujenga mabafu licha ya kuwa shule iko kisiwani na kisiwa kiko mbali kutoka Nansio (makao makuu ya wilaya) na pia kiko mbali kutoka Mwanza ambako mahitaji yote yanafuatwa.

“Nanyi pia fanyeni hayo hapa Madaba, mtumishi wa umma jitahidi ufanye jambo ambalo wengine limewashinda.Rais Samia anatamani kuwa na watumishi wengi wa aina hiyo.” amesema.

Kuhusu hoja za CAG, Waziri Mkuu amesema Halmashauri hiyo ya Wilaya ilikuwa na hoja 46 ambapo hoja 28 zimefungwa na hoja 18 bado hazijafungwa. “Malizieni hoja hizi 18 zilizobakia,” amesisitiza.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akikagua ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya Madaba kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali hiyo, Oktoba 19, 2022. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Thomas Laban na kulia kwake ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Madaba, Dkt. Mussa Rashidi.

Kuhusu ujenzi wa hospitali ya Halmashauri hiyo, Waziri Mkuu amewataka wakamilishe ujenzi kwa viwango alivyoviona na akampongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bw. Sajidu Mohammed kwa usimamizi mzuri.

Mapema, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na kuweka jiwe la msingi. Ujenzi wake umeshatumia sh. bilioni 2.084.

Akizungumza na wananchi waliofika kushuhudia uzinduzi huo, Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na ujenzi wa hospitali hiyo na kwamba anataraji hatua ya ukamilishaji itazingatia viwango bora.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kukagua na kuweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa hospitali ya halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma, Oktoba 19, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Naye, Mbunge wa Madaba, Bw. Joseph Mhagama amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia wana-Madaba sh. bilioni 14.2 ambazo zimetumika kujenga miradi ya maji, barabara za vijijini, miundombinu ya afya na elimu.

Ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali iwajengee kituo kikubwa cha mabasi na soko kub

By Jamhuri