Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jimbo la Mbeya vijijini kimetangaza kumfutia uanachama Joseph Mwasote ‘China wa China’ ambaye ni Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mbeya akidaiwa kuwa chanzo cha migogoro ndani ya chama hicho.

Akitangaza maazimio ya Kamati Tendaji ya CHADEMA Mbeya vijijini mwenyekiti wa jimbo hilo Jackson Mwasenga amesema mwanachama wake Joseph Mwasote ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA na makamu Mwenyekiti Kanda ya Nyasa amesema amekuwa chanzo cha migogoro ndani na nje ya jimbo hilo.

Wasema kuwa wamemwita mara kadhaa lakini hakuitikia wito na kwamba amekuwa akizunguka kwenye kata mbalimbali kupanga timu ya kuwapindua viongozi wa jimbo.

“Haijalishi tumekosea au hatujakosea lakini Kamati Tendaji ya Jimbo (Mbeya vijijini) kwa pamoja tumeazimia kumfutia uanachama Joseph Mwasote. Migogoro mingi chanzo ni yeye, kwenye kata huko anazunguka kwa nia yake binafsi anaunda kikundi cha kwenda kuwaondoa viongozi wa jimbo” amesema Jackson Mwasenga, Mkiti CHADEMA Mbeya vijijini.

Hata hivyo bado wako wanachama wanaodaiwa kukamatwa kwa saa kadhaa na Polisi wakidaiwa kutaka kuandamana kwenye ofisi ya jimbo mjini Mbalizi walipofika kutaka kujua hatma ya mwenyekiti wao kuondolewa.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo Joseph Mwasote mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mbeya ameeleza kusikitishwa na maamuzi ya jimbo lakini pia bado hajakabidhiwa barua ya kufutiwa uanachama wake.

“Lakini wameikosea katiba sana (ya CHADEMA). Anayeshikilia uanachama wangu ni Tawi (Isanga-Imezu), anayeshikilia uanachama wangu ni mamlaka yangu ya nidhamu ngazi ya juu. Yaani leo mkuu wa wilaya akamuondoe Mkuu wa Mkoa! ni shida”,” amesema Mwasote.

Kwa miaka ya hivi karibuni, Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA mkoani Mbeya kimekuwa kikihusishwa na migogoro ya ndani mara kwa mara hali ambayo inaharibu taswira na nia ya chama kwa wafuasi wake ambapo sababu mbalimbali zimekuwa zikitajwa ikiwemo uchu wa madaraka, kushindwa kutii itifaki ndani ya chama na kutofuata taratibu za ndani ya chama.