Na Is- Haka Omar, JamhuriMedia, Zanzibar

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi(UVCCM) Zanzibar,umemshauri Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mtungi,kufuta usajili wa Chama cha ACT-Wazalendo kutokana na kufanya siasa za chuki,fitna na kumdhalilisha Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi, kupitia mikutano yao ya hadhara kisiwani Pemba.

Ushauri huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Mussa Haji Mussa,wakati akizungumza katika mahojiano maalum na vyombo vya habari katika Afisi Kuu ya Umoja huo Gymkhana Unguja,alisema viongozi wandamizi wa ACT-Wazalendo wameendelea kutoa kauli za kihuni,uchochezi na kashfa dhidi ya Rais Dk.Mwinyi zinazoashiria kuingiza nchi katika machafuko ya kisiasa.

Mussa,alidai kauli hizo hazina nia ya kujenga maridhiano ya kisiasa visiwani Zanzibar bali zinaenda kinyume na sheria ya usajili wa vyama vya siasa nchini ya mwaka 1992.

Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo Mussa,alisema UVCCM Zanzibar, inalaani vikali na haitovumilia vitendo hivyo vya utovu wa nidhamu vya kumdhalilisha kiongozi mwenye hadhi ya Rais anayeongoza wananchi wa Zanzibar kwa uadilifu.

“Kifungu kidogo (1) cha (20) cha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 kinamtambua Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa ndio mwenye mamlaka kisheria ambaye anaweza kusajili na kufuta usajili wa chama chochote cha siasa,tunashauri ACT-Wazalendo ifutwe kwani imeshindwa kufanya siasa za ushindani wa kisera badala yake inafanya siasa chafu zenye malengo ya kuirejesha Zanzibar katika machafuko ya kisiasa.”, alisema.

Naibu huyo Mussa, amefafanua kwamba hoja za viongozi hao wa ACT-Wazalendo hazina mashiko na hazionyeshi dhamira ya kuendeleza marishiano ya kisasa yanayojengwa na kulindwa na uwepo wa kauli za heshima mbele ya jamii.

Amesema CCM kupitia mkataba wake na wananchi wa Visiwa vya Zanzibar iliyoingia mwaka 2020, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025, tayari imetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 100 ndani ya kipindi cha kuelekea miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dk.Mwinyi.

Akifafanunua madai ya Ripoti ya CAG Zanzibar, Mussa amesema tayari Rais Dk,Mwinyi amezielekeza taasisi zinazohusika na masuala ya ulinzi na kuchunguza kesi za rushwa na uhujumu uchumi nchini kuchukua hatua kwa yeyote atakayehusika na tuhuma hizo,hivyo hakuna umuhimu wa wanasiasa kufanya jambo hilo kuwa sehemu ya kutafuta umaarufu wa kisiasa.

Naibu Katibu Mussa, alisema Dk.Mwinyi hivi karibuni alizindua kamati ya maridhiano iliyowahusisha viongozi wa CCM na ACT-Wazalendo kwa lengo la kujadili muelekeo mzuri wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), na kwamba pamoja na juhudi hizo bado Viongozi wa upinzani wameendeza mashambulizi dhidi ya Serikali anayoiongoza.

“ACT-Wazalendo wanafanya siasa na propaganda zilizopitwa na wakati za kuwaaminisha wananchi kuwa Serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Dk.Mwinyi haijafanya kitu toka iingie madarakani, huku viongozi wa Chama hicho wakisahau wema,hisani na uadilifu waliofanyiwa na Rais huyo sambamba na wao kuwa sehemu ya Serikali hiyo yenye muundo wa SUK” amefafanua Mussa.

Amefafanua kwamba Dk.Mwinyi,anaendelea kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ya ujenzi wa Masoko,Bandari,Viwanja vya ndege,uwekezaji wa Mahoteli makubwa na kutumia vizuri dhana ya Uchumi wa buluu kuimarisha uchumi wa nchi na kufikia dhamira ya kupatikana kwa zaidi ya ajira 300,000 kabla ya mwaka 2025.

Ameeleza kuwa Rais Dk.Mwinyi, amekuwa kiongozi mzalendo anayeamini katika siasa za maridhiano,umoja na mshikamano na kuchukia tabia za wanasiasa vigeugeu wanaotumia majukwaa ya kisiasa kutafuta umaarufu wa kisiasa.

“Dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuruhusu mikutano ya kisisasa ni kuvipa uhuru vyama vya siasa vifanye siasa za maridhiano na kuwaunganisha wananchi na sio chuki na dhihaka.

NAIBU Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Mussa Haji Mussa akizungumza na vijana katika moja ya kongamano la Umoja huo Jijini Zanzibar.

Aidha,Mussa aliwataka viongozi wa ACT kuwa na utamaduni wa kufanya utafti wa kina juu ya hoja wanazoibua kwani hazina mashiko na zinaonyesha udhaifu uliobeba chuki na visasi vyao vya asili kwa kutumia mwamvuli wa siasa kulipiza visasi kwa watu wasio na hatia katika siasa za sasa za ulimwengu wa sayansi na teknolojia zinazotoa nafasi kwa kila mwananchi kufuata chama chenye sera anazozipenda.

Akizungumzia suala la kauli ya Dk.Mwinyi ya ajira za vijana wa CCM Zanzibar, amewaonya Chama cha ACT kuacha upotoshaji kwani ajira zilizozungumziwa ni zile zinazotokana na miradi ya CCM na jumuiya zake inayowahusu Vijana wazalendo wa Chama Cha Mapinduzi.

Naibu huyo, Mussa amewambia ACT-Wazalendo kuwa wawambie Wananchi wa Zanzibar toka wamepata usajili mwaka 2014 wametekeleza mradi gani wenye maslahi kwa wananchi wote.

By Jamhuri