WAF – Tanga

Jopp  la madaktari bingwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan waliokita kambi kwenye Hospitali ya Jiji la Tanga iliyopo Kata ya Masiwani wamefanya upasuaji wa kuondoa mwiba uliokwama kwenye koo la mtoto mdogo wa mwaka mmoja na nusu uliodumu kwa muda wa wiki moja.

Dkt. Salehe Mlutu ambaye ni daktari bingwa aliyemfanyia upasuaji amesema mtoto huyo aliletwa jana baada ya wazazi kusikia kambi ya madaktari bingwa akiwa anakohoa sana hali iliyofanya wazazi wake kudhani kuwa ni kifua kinamsumbua lakini baada ya kufanyiwa vipimo ilibainika kuwa alikua na mwiba uliokua umekwama kwenye koo sehemu ya hewa.

Kufuatia hali hiyo mtoto alifanyiwa upasuaji wa dharura ambao ulifanikiwa ambapo haujawahi kufanyika katika Hospitali hiyo ambayo haina daktari bingwa wa aina yoyote, hivyo ujio wa madaktari bingwa wa Samia umekua mkombozi kwa wananchi wa Kata ya Kisiwani na maeneo ya jirani kupata huduma za kibingwa.

Naye Dkt. Peter Nicholaus ambaye ni kiongozi wa Madaktari Bingwa wanaotoa huduma katika Hospitali amesema toka wameanza kutoa huduma katika Hospitali hiyo wameona wagonjwa zaidi ya 100 wenye matatizo mbalimbali ikiwemo hitilafu katika moyo ambapo wagonjwa watano wamepewa rufaa kwenda katika Hospitali kubwa kwa ajili ya matibabu zaidi huku wengine wakifanyiwa upasuaji hapo hapo.

Aidha, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Rashid Said ameishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kufanikisha ujio wa Madaktari Bingwa hao Hospitalini hapo ambao imekua chachu ya uboreshaji wa huduma baada ya kupewa ujuzi. 

“Kipekee nichukue fursa hii kumshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujio wa Madaktari Bingwa hospitalini hapa ambao kiukweli wamekuwa faraja kubwa kwa wananchi wa Jiji la Tanga wanaofika hapa kupata matibabu pamoja na kurahisisha gharama za kuwaona Madaktari Bingwa ambao badala ya kuwaona Bombo au Muhimbili wamefika hapa na kuonana na wananchi kwa gharama nafuu”. Amesema Dkt. Rashid.

Dkt. Rashid ameongeza kuwa hapo awali Hospitali hiyo haikuwahi kufanya upasuaji wa aina hiyo lakini siku ya leo kutokana ujio wa madaktari bingwa hawa kwa mara ya kwanza imeweka historia ya kufanya upasuaji huo mkubwa hivyo badala ya upasuaji huu kufanyika Bombo au Muhimbili umewezekana kufanyika hapo.

Rehema Kijoi ni mmoja wa wananchi waliojitokeza hospitalini hapo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapeleka madaktari hao kufika Hospitalini hapo kutoa huduma za kibingwa ambazo hapo awali walikua wanazifuata sehemu za mbali na kwa gharama kubwa zaidi.

Please follow and like us:
Pin Share