Mwisho wa zama, ndivyo unavyoweza kusema baada ya mshambuliaji wa Real Madrid na Ubelgiji, Eden Hazard, kustafuu kuitumikia timu yake ya taifa ya Ubelgiji. 

Hazard na mastaa wengine kama Kevin De Bruyne na Romelu Lukaku wameshindwa kuipa mafanikio timu yao ya taifa na hiyo imepelekea Eden Hazard kustaafu na kupisha wengine wajaribu kulibeba taifa hilo.

Katika taarifa yake ya kujiuzulu katika soka la kimataifa, Eden Michael Walter Hazard (31), ameandika, “Ukurasa umefungwa leo. Ahsante kwa ushirikiano wenu usiopimika. Kizazi kipya [cha kuchukua nafasi yake] kimeshaandaliwa. Nitawakumbuka sana,” alimalizia nyota huyo wa zamani wa Chelsea ambaye amekumbwa na majeraha mfululizo toka alipojiunga na Real Madrid ya Hispania. 

Ubelgiji ilikuwa kundi F katika Michuano ya Kombe la Dunia pamoja na Croatia, Canada na Morocco ambapo Ubelgiji na Canada walifurushwa na kuishia hatua ya makundi huku Morroco na Croatia wakifuzu.