Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angelina Mabula, amezitaka idara za Ardhi katika halmashauri nchini kuyabaini mashamba yote yasiyoendelezwa (mashamba pori) na kupeleka wizarani mapendekezo ya kufutwa kwa hati zake.

Dk. Mabula amesema hayo wiki iliyopita alipokutana na watendaji wa sekta ya Ardhi pamoja na wakurugenzi wa halmashauri zote za Mkoa wa Kilimanajaro, akiwa katika ziara yake ya siku mbili mkoani humo kukagua utendaji kazi wa sekta ya Adhi.

Amesema pamoja na baadhi ya mashamba kufutwa katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na kutoendelezwa, kuna maeneo mengine maofisa Ardhi wameshindwa kuyatolea taarifa mashamba yasiyoendelezwa ili yafutwe kwa sababu wanazozijua wenyewe.

“Nataka taarifa ya mashamba pori yote katika halmashauri yabainishwe na kutolewa taarifa ili tuweze kupeleka mapendekezo ya kufutwa mashamba hayo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Dk. Mabula.

Kwa mujibu wa naibu waziri huyo, taarifa ya kubaini mashamba pori yote katika kila halmashauri ziwe zimewasilishwa wizarani kufikia Desemba mwaka huu na Januari 2020 timu maalumu itaundwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Dk. Mabula amesema ofisa Ardhi katika halmashauri yoyote atakayebainika kuficha ukweli kuhusiana na uwepo wa mashamba pori katika eneo lake atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

“Maofisa Ardhi mnashirikiana na baadhi ya wenye mashamba pori na mnashindwa kuleta mapendekezo ya kufutwa mashamba, sisi tunahitaji kuona kila ardhi inatumika katika malengo yaliyokusudiwa,’’ amesema Dk. Mabula.

Awali katika kikao hicho, baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri za Mkoa wa Kilimanajaro pamoja na maofisa Ardhi walimueleza naibu waziri huyo kuwa idara za Ardhi katika halmashauri zao zinakabiliwa na changamoto kubwa za upungufu wa watumishi katika fani mbalimbali za sekta ya Ardhi pamoja na bajeti finyu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Kastori Msigala, alieleza mathalani kuwa halmashauri yake inakabiliwa na upungufu wa watumishi katika fani za Mipango Miji, Upimaji na Uthamini, jambo alilolieleza kuwa linachangia kwa kiasi kikubwa kutofikiwa malengo katika sekta ya ardhi.

Katika hatua nyingine, Dk. Mabula ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa ofisi na nyumba za Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) katika Shamba la Miti la Kilimanjaro Kaskazini, maarufu kama Rongai, lililopo wilayani Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa  Mkoa wa Kilimanjaro, Stanley Msoffe, ujenzi wa ofisi na nyumba za watumishi wa TFS unaofanywa na NHC unaogharimu zaidi ya Sh milioni 532.9 unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2020.

631 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!