Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
 
Wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, alitoa hoja ya kutaka Serikali iunde Tume ya Kuchunguza mauaji na utekaji nchini.


Hoja hii ameitoa baada ya Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, kutoa orodha ya watu 83 ambao ama wamepotea bila maelezo au wamepotelea mikononi mwa jeshi la polisi.

Sitanii, sehemu kubwa ya makala hii nitarudia habari tuliyoichapisha mwishoni mwa mwaka jana (2023), ambayo hadi leo familia haijapata majibu ya nini kilitokea kwa ndugu yao na kwa kweli, kupitia habari hii, niiombe Serikali iichukue kwa uzito unaostahili.

Nimesoma kwenye moja ya mitandao baadhi ya watu wanambeza Mbowe kwa kutoa hoja hii wakidai anatafuta kiki ya kisiasa.

Ndugu zangu Watanzania, katika masuala ya kitaifa tunapaswa kuweka siasa kando na kusimama pamoja kama Watanzania.
Inawezekana wanaopuuza hoja ya Mbowe kutaka iundwe Tume ya Kuchunguza Mauaji na Kupotea kwa Watu, hayajawahi kuwafika katika familia au kupotelewa na ndugu.

Ulinzi wa maisha ya bibadamu ni jambo la msingi mno, hivyo hatupaswi kutoa majibu mepesi.

Jumamosi iliyopita, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, ametangaza mauaji ya watu watatu katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Singida, akitoa sababu nyepesi kuwa ni wivu wa mapenzi na tamaa ya kupata mali wanazojengewa na waganga wa kienyeji.
Hiyo pekee inanipa shida.

Inaashiria kuwa kuna Watanzania walioacha kuogopa mkono wa sheria au kutii sheria bila shuruti.
Sitanii, tunapaswa kujiuliza nini kimetokea? Ni elimu ya uraia imepungua, ni vijana wetu kutoshiriki mafunzo ya mgambo au kwenda Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambako tulikuwa tukifundishwa uzalendo na utii wa sheria?

Je, viongozi wetu wakipanda kwenye majukwaa ya siasa siku hizi katika hotuba zao wanatoa elimu ya uraia au wote wanashindana kushawishi wapiga kura watarajiwa?
Ziko wapi nyimbo za kizalendo? Sanaa inatumika kujenga nchi yetu au tumewekeza katika filamu za mapenzi, ushoga na mauaji ambazo sasa zinatafsiriwa kwa vitendo?

Naomba kuweka sehemu ya habari hiyo, kisha mwisho niweke hitimisho, uone jinsi familia zinavyoishi kwa mateso makubwa kwa kupotelewa na ndugu zao jambo lisilopaswa kuwapo hapa Tanzania.


 
Habari tuliyochapisha:
Akizungumza na JAMHURI, mfanyabishara mmoja wa Soko la Nyankumbu, (mjini Geita) anasema matukio hayo [ya utekaji na watu kupotea] yameanza tangu Januari mwaka huu.

“Hawa watu wanajitambulisha kuwa ni askari polisi, lakini wakishamchukua mtu wanayemtuhumu, basi mtu huyo hataonekana tena mtaani.

“Hali hii inatuletea hofu sana kiasi hata cha kushindwa kufanya shughuli zetu za kila siku,” anasema mfanyabiashara huyo kijana akiomba hifadhi ya jina.

JAMHURI limeelezwa kwamba matukio hayo ni mwendelezo wa yaliyowahi kujitokeza kipindi cha nyuma, ambapo walinzi walikuwa wakiuawa na watu wasiojulikana.

“Zipo familia zimepoteza wapendwa wao baada ya kutekwa na watu hao.
Sababu hasa hazieleweki, kwa kuwa hakuna mtu aliyetekwa akarejea nyumbani,” anasema kijana huyo.
 
Tukio la siku za karibuni
Tukio la karibuni zaidi la utekaji au ukamataji unaoendana na kupotea kwa watuhumiwa, limetokea Jumamosi ya Oktoba 14 mwaka huu (mwaka jana) saa mbili usiku.

Tukio hilo limetokea Mtaa wa Elimu, Nyankumbu mjini Geita, ambako Frank Bernard Thomas (36), mfanyabiashara wa samaki, alichukuliwa na watu wasiojulikana, hadi leo hajulikani alipo.

Thomas alikamatwa na watu wawili waliofika ghafla kibandani (gengeni) alipokuwa akinunua mahitaji ya familia, mita 100 tu kutoka nyumbani kwake. Mashuhuda wanasema kabla watu hao hawajaondoka na Frank, walijitambulisha kuwa ni askari polisi.

Jane Magala, muuzaji wa kibanda alipokamatiwa Frank akifanya ununuzi, anakiri kushuhudia kukamatwa kwake, akisema wahusika ni wanaume wawili waliojitambulisha kuwa ni askari polisi.


“Kabla hawajaondoka, niliwaomba waniachie mfuko aliokuwa nao (Frank, ambao ulikuwa na bidhaa kadhaa alizonunua kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kwa siku hiyo). Wakakataa.
“Baadaye, walipofika mbali kidogo, nadhani walibadili mawazo, wakaniita. Frank akanipe ule mfuko.

Nikauchukua na kuupeleka nyumbani kwa mkewe. Nikamwita na kumpa taarifa za kukamatwa kwa mume wake,” anasema Jane.

Jane anasema anamfahamu Frank kwa muda mrefu na anashangaa kwa nini akamatwe ilhali hana historia ya matukio mabaya ya uhalifu.


“Nashangaa eti sasa hajulikani alipo! Inasikitisha sana. Inasemekana hili si tukio la kwanza. Watu wengi wamekamatwa na kupotea kwa staili hii. Sasa tunaishi kwa hofu hapa Geita,” anasema.

Kauli ya Jane inaungwa mkono na watu wanaofanyabiashara ya samaki Soko la Nyankumbu, ambao pia wanashiriki kumtafuta au kutafuta taarifa za wapi aliko Frank kwa sasa.

JAMHURI limeelezwa kwamba baada ya kuondoka kibandani kwa Jane, watu hao walimpakia Frank kwenye gari lililokuwa limeegeshwa barabara ya Geita – Katoro; mita 120 kutoka kibandani alikokamatiwa.

Shuhuda mwingine aliyejitambulisha kwa jina la John Peter, anasema Frank aliingizwa kwa nguvu kwenye gari ambalo liliondoka kuelekea Geita mjini.

“Matukio haya yanatufanya kuishi kwa hofu. Kama anachukuliwa mtu na kupotezwa kirahisi namna hii, ndugu wanaishije?
“Sisi tulidhani wale watu ni askari polisi kwa jinsi walivyomkamata na kuondoka naye hadi kwenye gari,” anasema Peter.
 
Polisi wamduwaza mke wa Frank Efosia Ernest (22), mke wa Frank, anasema alitaarifiwa na Jane kuwa mumewe amechukuliwa na askari polisi alipokuwa kibandani kwake akinunua mahitaji, zikiwemo zawadi za watoto.

“Alikuja nyumbani huyo mama anayeuza kwenye kile kibanda (Jane). Akaniita na kuniambia mumeo amekamatwa na askari, wameondoka naye,” anasema Efosia.

Anasema usiku huo huo alimpigia simu shemeji yake aitwaye Doto kumpa taarifa kuwa kaka yake kakamatwa, Doto akamshauri aende Kituo cha Polisi Geita kufuatilia.

“Niliwataarifu ndugu wengine usiku huo huo. Tukaenda polisi. Tulipofika, walituambia kuwa kwa muda huo sio rahisi kumuona kwani ni usiku.Wakaniambia nirudi asubuhi,” anasema Efosia.


Asubuhi iliyofuata, Efosia akiambatana na nduguze, akiwemo baba mzazi wa Frank, mzee Bernard Thomas (66), mkazi wa Mpovu, Kata ya Mtakuja mjini Geita, walifika Kituo cha Polisi Geita wakiwa na kifungua kinywa kwa ajili ya ndugu yao, lakini hawakuruhusiwa kumuona.

“Nilijitambulisha na kuwaeleza kuwa nimekwenda kumuona mume wangu. Wakaniuliza anaitwa nani? Nikataja jina lake. Wakaniambia kuwa huyo huwezi kumuona.

Nikawaomba nimpatie chakula. Wakaita jina lake, nikasikia sauti yake akiitika akiwa katika chumba cha mahabusu.

“Askari wakachukua chakula kumpelekea, ila mimi sikumuona. Hapo nikaanza kushituka kwa kuwa hiyo si kawaida ukimpelekea chakula ndugu yako mahabusu!” anasema mama huyo.

Anasema kwa kawaida chakula hupokewa ukiwa unamuoa ndugu yako na kabla ya kukichukua, unapaswa kukionja, utaratibu ambao haukufanyika siku hiyo.

Katika hali ambayo hawakutarajia, siku iliyofuata askari mmoja, kwa mujibu wa Efosia, aliwaeleza kuwa Frank hakuwamo mahabusu. Wakaenda kutazama kitabu cha kusajili watuhumiwa, kweli jina lake halikuwapo.

Hali hiyo iliwatia wasiwasi na kujiuliza, sauti iliyoitika jina la Frank lilipotajwa ilikuwa ya nani? Na ni nani aliyepelekewa chakula mahabusu na akala?
“Ikabidi niende kwa Mkuu wa Kituo (OCS). Yeye akanielekeza kwenda kwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID).

Akaniambia kuwa nyaraka hazionyeshi kwamba Frank alifikishwa kituoni hapo,” anasema Efosia huku akibubujikwa machozi, na kusema:

“Sasa hata sijui mume wangu yuko wapi na nani atanisaidia kulea watoto wetu. Yeye ndiye nilikuwa namtegemea. Ndiye alikuwa mtafutaji.”

Hatua iliyofuata ilikuwa ni kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Geita na kisha kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD).

Efosia anasema DC alimwita OCD na kumpa muda wa kufuatilia suala hilo, ambapo siku tatu baadaye, OCD akasema kuwa amepitia nyaraka zote na hakuna zinazoonyesha kuwa Frank alifikishwa kituoni hapo.

“Tumefanya kila kinachowezekana bila mafanikio. Tunajiuliza, nani aliyeitika ndani ya mahabusu Frank alipoitwa? Nitaishi vipi na watoto wetu? Sasa nimebaki kutegemea ndugu,” analalamika Efosia.

Doto, mdogo wake Frank, anasema siku alipopigiwa simu na shemeji yake, alikuwa safarini kuelekea Musoma.

“Niliporudi nyumbani nikaungana na ndugu zangu kufuatilia alipo Frank bila mafanikio. Tumebaki tukijiuluza, ndugu yetu kachukuliwa na watu gani?


“Kama mtu anakosa lolote bora akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, sio kumpeleka kusikojulikana,” anasema Doto ambaye anawalaumu polisi akiamini kuwa ni wao tu ndio wenye majibu sahihi.
 
Wadai Frank ana historia safi Mzee Thomas, baba yake Frank, anatetea uadilifu wa mwanaye akisema tangu utotoni hadi alipoanza kujitegemea hakuwahi kuwa na kesi yoyote au tuhuma za uhalifu. Frank na baba yake walikuwa wakifanya pamoja biashara ya samaki Soko la Nyankumbu.

“Hakuwahi kuwa na kesi au kulalamikiwa na mtu yeyote kwamba hili linaweza kuwa sababu ya kukamatwa na sasa kupotea kabisa. Mimi sijawahi kusikia kwa kweli,” anasema mzee huyo.

Kauli ya mzee huyo inarandana na kauli ya Jane, jirani wa Frank aliyeshuhudia akikamatwa nje ya kibanda chake cha biashara. Hata washirika wake kwenye biashara ya samaki Soko la Nyankumbu, nao wanatetea tabia ya Frank, wakidai kuwa hana historia mbaya.


 
Viongozi wa mtaani
Balozi wa eneo analoishi Frank, Jumanne Mahuba, anasema alipokea taarifa ya kupotea kutoka kwa ndugu na kuifikisha kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa.

“Ninamfahamu. Hana tabia mbaya. Huwa tunashirikiana vizuri kwenye shughuli za kijamii. Sasa tunajiuliza, kwa nini amepotea baada ya kuondoka na watu wanaoaminika kuwa ni askari polisi?

“Kwa kawaida mtu akikamatwa na polisi, unakwenda kituoni unamkuta! Sasa hii inakuwaje?” anahoji Mahuba.

Anasema kwa mujibu wa utaratibu uliozoeleka, kabla ya mtu kumkamatwa, maofisa wa vyombo vya dola huwashirikisha viongozi wa mtaa.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Elimu, Hassan Mshore, anathibitisha kupokea taarifa za tukio hilo na kwamba baada ya kuzipokea aliwaelekeza ndugu kwenda kituo cha polisi.
 
RPC apiga chenga
 JAMHURI limemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Geita, Safia Jongo, kutaka kujua sababu za Frank kutokuwapo mikononi mwa chombo cha dola anachokisimamia.

Afande Safia hakutaka kulizungumzia sula hilo wala kusema iwapo ana taarifa zozote, badala yake akaamua kuzungumzia masuala ya usalama mkoani Geita kwa ujumla wake.

“Mkakati wa sasa wa Jeshi la Polisi mkoani hapa ni kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao kwa kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi kila mtaa.

“Hii inakwenda sambamba na kukabiliana na matukio ya uharifu na matukio ya aina hiyo,” anasema RPC akionekana wazi kutotaka kumzungumzia Frank, ingawa ndugu wa Frank pamoja na mkewe wakidai kuwa walikwishafika ofisini kwake.
 
Kauli yake ya awali
 Julai mwaka huu, Afande Safia amewahi kukiri kupokea taarifa za kupota kwa watu wawili, lakini pia hakutaka kutoa ufafanuzi wa kina, akidai kuwa matukio hayo yameundiwa timu maalumu ya kuyachunguza kutoka ‘makao makuu’.

Katika tukio la kupotea kwa Oscar Ibrahim (24) mkazi wa Shilabela, Geita, alipoulizwa na kuelezwa kwamba wahusika wa matukio ya aina hiyo hujitambulisha kuwa ni askari polisi, RPC alisema: “Si kila mtu anayejitambulisha kuwa ni askari polisi basi kweli ni askari polisi.”
 
Mlolongo wa matukio
 Wilaya ya Geita imekumbwa na matukio ya watu kutekwa mara kadhaa, ukiachana na kutekwa na kupotea kwa Oscar na Frank, wengine waliokumbwa na zahama hiyo ni Pius John wa Nyankumbu, Francisco Kalinganile (47) mkazi wa Biharamulo mkoani Kagera aliyetekwa Katoro akitoka kununua ng’ombe mnadani.


Wote hao tangu kutekwa kwao hawajaonekana hadi leo. Matukio haya yanadaikuwa kuwa ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), Ibara ya 14 inasema kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata hifadhi ya maisha yake kutoka katika serikali na jamii kwa mujibu wa sheria za nchi.

Sitanii, polisi kusema “si kila anayejitambulisha kuwa ni polisi ni polisi” ni kauli ya habari mbaya kabisa. Kwamba polisi wana taarifa za uwapo wa polisi feki na wanakiri hivyo, inasikitisha.

Hawa waliokamatwa wanapaswa kufikishwa kwenye vyombo vya dola na wakipewa adhabu jamii ifahamishwe adhabu waliyopewa hata kama ni kunyongwa hadi kufa, kwa mawazo yangu naamini hii itarejesha utii kwa sheria.

 Naunga mkono hoja ya Mbowe, asibezwe kwa kusema eti ni mpinzani. Iundwe Tume ya Kuchunguza Mauaji na Kupotea kwa Watu.

Thamani ya maisha ya binadamu ni kubwa mno na haina kipimo. Ndiyo maana hata magerezani tunawatibu wafungwa, tena waliohukumiwa kifungu cha maisha au kunyongwa hadi kufa!

Hivi leo familia ya Ben Sanane unadhani inajisikiaje? Kwamba mtu anapotea kama kuku aliyenyakuliwa na kicheche? Hivi kweli kabisa hadi leo ni kwamba hakuna mtu mwenye taarifa anayefahamu Ben Sanane alikwenda wapi?

Hakuna mtu hata mmoja aliyeona anaondoka au aliyesikia anaitwa kama aliitwa kwa simu? Tukinyamazia matukio kama haya, hasa kama hili la Frank wa Geita la watu kuitwa polisi akaitika wakapokea hadi chakula chake, lakini asionekane, ipo siku tutalipa gharama kubwa kama nchi.

Kama tumeunda Kikosi Kazi cha Kuchunguza Hali ya Siasa nchini, Kikosi Kazi cha Uviko – 19, Tume ya Sera ya Mambo ya Nje, Tume ya Haki Jinai na sasa Tume ya Kodi, hili la uhai wa binadamu ni zito kuliko yote hayo.

Tume ikiundwa itabaini sababu za kweli na hasa hawa wanaopotelea kwenye mikono ya dola, kisha itatoa maelekezo nini kifanyike mauaji yasijirudie tena. Mungu ibariki Tanzania.

0784404827

Please follow and like us:
Pin Share