Namna ya kuzungumza mtoto akusikilize, aongee

ARUSHA

Na Dk. Pascal Kang’iria 

Tangu zamani jamii duniani imekuwa ikipitia maisha ya kila namna – yenye uzuri na ubaya ndani yake. Vizazi kadhaa vimepita vikirithishana tamaduni mbalimbali.

Sehemu kubwa ya kufanya utamaduni kuwa makini na wenye tija, ni kupitia malezi. Kipindi cha malezi ni kuanzia mimba mpaka kabla ya mtoto kubalehe (wa kiume) au kuvunja ungo (wa kike).

Mchakato huu wa malezi umekuwa ukitumika nyakati zote kuleta ustawi katika jamii mbalimbali duniani. Ni mchakato mpana sana wenye mlolongo mrefu.

Kila jamii ina utaratibu wake wa kufanya na kutekeleza suala hili, hivyo kufanya pia kila familia kuwa na namna yake ya kutekeleza huu mchakato. 

Hata ndani ya familia moja moja bado utaratibu unaweza kuwa tofauti kwa mtoto mmoja ukilinganisha na mwingine wa familia hiyo hiyo.

“Kuzaa mtoto hakutoshi kukufanya kuwa mzazi bora na mwenye kuongoza katika maadili, sawa na kuwa na kinanda hakufanyi mmiliki kuwa mpigaji mahiri,” anasema Levine

Maelezo ya mtaalamu huyu yanatoa mwanga kwa suala hili kuwa linahitaji mkakati kabambe kufikia malengo yaliyokusudiwa. 

Mawasiliano ndiyo njia pekee inayotumika katika malezi. Hapa naweka mkazo hasa katika namna ya kuyafanya hayo mawasiliano, maana ndipo shida nyingi zinazoendelea katika dunia ya leo zinapoanzia.

“Dhana ya malezi ni uwekezaji wa muda mrefu, si mkopo wa muda mfupi,” anasema mtaalamu mmoja wa malezi.

Hoja hii ya uwekezaji katika malezi inaonekana kama haieleweki kwa wengi, hasa wazazi wenye watoto. Mara nyingi huwa tunajua katika biashara tunahitaji kuwapo ili mambo yaende kama jinsi tunavyohitaji.

Uangalizi wa karibu wa biashara yoyote huhitajika ili kupata matokeo kusudiwa. Mahali pengine mtu aliyewekeza inamlazimu kuweka hata kamera ili kuwa na ufuatiliaji wa karibu wa kila kitu kinachoendelea eneo lake la biashara.

Huu uangalizi wa karibu husaidia kufanya maboresho pale yanapohitajika ili malengo yafikiwe. Utahitaji kujua mwitikio wa wateja wako upoje na hata kujua mahitaji yao ni nini hasa ili uweze kuwatimizia. 

Kama mzazi ambaye ulihitaji kupata mtoto, unahitaji kumsikiliza ujue anahitaji nini au yupo na nini ili umsaidie kufikia malengo yake ya maisha ambayo huyajui.

Hujui anatakiwa kuwa nani au ameandaliwa kuwa nani  katika maisha ya baadaye. 

Hitaji la kuwepo karibu na kufuatilia ukuaji wa mtoto wakati wa malezi ni muhimu sana, hivyo kipindi cha malezi ni kipindi cha kila mmoja kupata muda wa kumsikiliza mwenzake ili maisha yaonyeshe maana.

Kwa sehemu kubwa suala zima la malezi huathiri afya ya akili ya kiumbe tangu kikiwa tumboni mpaka kipindi chote cha ukuaji wake na mwisho kutengeneza aina fulani ya mtu.

Afya ya akili ni uwezo wa kujikubali na kukubali wengine, kupokea na kuchukuliana hisia na kukabiliana na matatizo na changamoto unazokutana nazo maishani. 

Kimsingi maisha yetu kila siku ni changamoto na yana misukosuko mingi. Mtoto anatakiwa kutambulishwa katika aina hii ya maisha vizuri ili kutosha kuwa mtu mwenye manufaa katika maisha yake popote atakapokuwa.

Udhaifu utakaojitokeza katika malezi ya kiumbe, hatimaye huleta udhaifu katika utu wake na mwisho kushindwa kuwa mtu mwenye manufaa katika jamii. 

Kila mtu huzaliwa akiwa na vipawa kadhaa ndani yake, mazingira sahihi ya malezi makini hufanya vipawa kukua na kuwa vyenye manufaa katika kila jamii atakayoishi baadaye. 

Maisha yana mawimbi mengi ambayo kwa kiasi kikubwa yasipowekewa namna nzuri ya kuyakabili yataharibu mifumo yote makini katika maisha ya mtu na kuharibu afya yake ya akili.

Namna bora ya kukabiliana na mawimbi ya aina zote za maisha tunaipata kupitia aina ya malezi mtu atakayoyapitia kipindi chote, kuanzia kutungwa mimba yake mpaka wakati wa kubalehe/kuvunja ungo.

‘Malezi makini’ si jambo rahisi na huenda yasiwe na njia moja ya kufika katika hitimisho tazamiwa. 

“Wakati mzuri wa kuzuia ulimi wako ni pale ambapo unajisikia kuwa ni lazima uongee kitu,” anasema Josh Billings. 

Wazazi wengi huwa ni waongeaji na watoa maelezo mara kwa mara wakiamini hii ndiyo njia sahihi ya kufanya mambo yaende. 

Wakati unapokuwa umechafukwa hasa, basi si muda sahihi wa kuongea kitu.

“Watoto wangu kamwe hawasikilizi neno lolote kutoka kwangu,” anasikika mama mmoja akisema. Mwingine akasema: “Mara zote nikimuuliza mtoto wangu swali, anapandisha mabega na kunijibu kwa kifupi, nitafanyaje aweze kuongea?”

Kijana mmoja anasema: “Ninapojaribu kufungua mdomo wangu kuongea, napata ishara ya kukatishwa kuongea na baba na kama nikiulizwa swali huwa napata jibu la silabi moja tu.” 

Kila mtu anapoongelea elimu ya malezi, anasisitiza mawasiliano kwa watoto, ukweli ni huu mara zote huwa tunawasiliana (kwa maneno au vitendo). 

Lakini swali la muhimu ni hili, je, unawasiliana? Kujua nini na kwa namna gani unawasiliana ni rahisi kuliko kuwasiliana. 

Kulingana na Oxford English Dictionary, maneno ya Kiingereza ya kawaida kama 500 yana maana tofauti tofauti zaidi ya 23, hivyo kuna uwezekano mkubwa ya kila unachowasiliana na mwanao kisiwe na maana halisi ya unachokizungumza. 

Mfano; maneno ya wazazi – ‘huwa hunisikilizi ninaposema’, ‘Kumbuka kuwa mwema’, ‘Ulikuwa nyumbani kwa bibi yako…’  – Je, mwanao anakuelewa? 

Tangu watoto kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri, huwa wanapata shida sana kuelewa kauli ambazo hazipo wazi sawasawa. 

Wazazi makini wanatumia ujumbe sawasawa/uwazi na kuondoa utata katika lugha wanayotumia. Mfano wa ile kauli ‘kumbuka kuwa mwema’ ambapo mtoto James aliambiwa katika sherehe zake za siku ya kuzaliwa. 

Ingepaswa kuwa hivi: “Kumbuka kumshukuru Chacha na mama yake kwa muda wao walioutoa kuja kwenye sherehe zako.”

Hitimisho 

Ujumbe sahihi unamfundisha mtoto wako kuwa na tabia iliyo njema. Mfanye mwanao kujua pale anapofanya vizuri na pale anapokosea umsaidie kurekebisha tabia. 

Hakuna mtoto mwenye tabia mbaya au mtoto mbaya, kila mtoto huja akiwa safi ila huharibiwa hasa na tabia za wazazi wake, na hayo mazingira anayokulia ambayo hata hivyo hao wazazi ndio walimuweka katika hayo mazingira. 

Kama mzazi, kuwa makini katika maongezi yako lakini pia kuwa makini sana katika matendo/tabia yako. 

Watoto wapo hivi tunavyowaona kutokana na aina ya wazazi alionao na jinsi wanavyomtambulisha katika dunia hii. Zaidi ya yote, mtoto wako anaposikia ujumbe sahihi (maneno au matendo) kutoka kwako ni rahisi kukujibu au kutenda kwa usahihi pia (reciprocity).

Mwandishi wa makala hii anajitambulisha kama Dk. Pascal Daniel Kang’iria, Daktari Msaikolojia Tiba ya Afya ya Akili na Utengamano (Clinical Psychiatrist). Anapatikana jijini Arusha kwa simu: 0713 430 096 na barua pepe: padack7@gmail.com

1262 Total Views 8 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!
Show Buttons
Hide Buttons