Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Pemba

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema anawaheshimu na kuwakubali wana CCM wa Pemba kwa misimamo yao thabiti katika kuilinda na kuitetea CCM bila kuyumba.

Dk. Nchimbi pia amewapongeza kwa jinsi ambavyo wameendelea kuwa imara kuifanya Pemba kuwa mojawapo ya ngome za Chama Cha Mapinduzi nchini, akiwasisitiza wana  CCM kuendelea kuwa wamoja, chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.

Hayo ameyasema leo Jumamosi, Machi 23, 2024, wakati akizungumza na baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM wa Pemba, waliofika kumlaki katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume Kisiwani Pemba, mara tu baada ya kuwasili uwanjani hapo, tayari kuanza ziara ya kikazi ya siku moja kisiwani hapa.

 “Kati ya wana CCM ninaowaheshimu na kuwakubali sana kwa jinsi wanavyoipenda CCM, wanavyoilinda, kuitetea na kuisemea ni wanaCCM wa Pemba. Asanteni sana kwa mapokezi yenu.

“Siku zote mmekuwa imara na daima hamkubali kuyumba. Hongereni sana kwa kuendelea kuifanya Pemba kuwa ngome ya CCM. Leo nimekuja kwa ziara ya siku moja tu, lakini nitakuja ziara nyingine ya kuzungumza na viongozi wote, wanachama wote na wananchi,” amesema Dk. Nchimbi.

Mapokezi hayo yaliyopambwa na ukaribisho wa kiutamaduni wa CCM, ambapo Katibu Mkuu Balozi Dk. Nchimbi alivalishwa skafu na vijana wa hamasa, mbali ya kuwepo viongozi wa ngazi mbalimbali za chama na Serikali na wanachama, yaliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Mohammed Said Mohamed (Dimwa), akiongozana na viongozi wengine, akiwemo Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Mohamed Abood Mohamed na wajumbe wengine wa NEC kutokea Pemba

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, akilakiwa na viongozi wa chama na Serikali mara baada ya kuwasili Kisiwani Pemba leo
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, akisalimiana na viongozi na wanachama mbalimbali

By Jamhuri