Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Pwani

MWENYEKITI wa Wazazi Mkoa wa Morogoro (CCM), Dk. Rose Rwakatare ametunukiwa Shahada ya Udaktari wa Heshima (PhD) na Chuo Kikuu cha All Nations Christian Church International University kilichopo Texas Marekani (ANCCI) kutokana na mchango wake kwenye jamii.

Hafla ya kutoa shahada hiyo kwa watu mbalimbali imefanyika leo Kibaha kwa Mbonde Mkoa wa Pwani ambapo mwakilishi wa chuo hicho ambaye ni raia wa Kenya, Profesa Purity Gatobu alitunuku Shahada hiyo.

Akizungumza mara baada ya kutunukiwa Sahahada hiyo, Dk. Rwakatare amesema kwa muda mrefu ametumia karama alizojaliwa na Mungu kusaidia makundi mbalimbali kwenye jamii wakiwemo wanawake, watoto na vijana kwa kuwapa nyenzo mbalimbali za kuwawezesha kuondokana na umaskini kama elimu ya ujasiriamali.

“Mimi pia ni Mwenyekiti wa Wazazi CCM Mkoa wa Morogoro kwa hiyo wenye shida nimekuwa msaada kwao kwa njia mbalimbali na mimi ni mlezi wa Kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni pale ninalea makundi mbalimbali kwenye jamii nashukuru sana kwa chuo hiki kunitambua kwa kazi zangu na imenipa moyo kwamba kumbe dunia inaona kazi ninayofanya,” alisema

Dk. Rwakatare ambaye pia ni Mkurugenzi wa shule za St Mary’s na East Africa, alisema Shahada aliyotunukiwa imempa ari ya kuendelea kutumikia jamii kwa kutoa msaada mbalimbali kwenye jamii.

Angella Bondo, ambaye naye ametunukiwa Shahada hiyo ya heshima, alisema kwa miaka 22 mfululizo amekuwa akitumikia jamii kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo kutoa elimu ya ujasiriamali ambapo amefanikiwa kuwafikia watanzania wengi.

“Unaposaidia jamii unawagusa wanawake, watoto, vijana na hata wanaume kwa hiyo nashukuru kwamba chuo hiki kimeona kazi zangu na kuamua kunitunuku shahada ya udaktari wa heshima na naahidi kwamba hii itakuwa chachu ya mimi kuendelea kuitumikia jamii,” alisema Angella.

Alisema pia amekuwa akitoa huduma kwenye makanisa mbalimbali likiwemo la Mlima wa Moto Mikocheni kupitia vipindi vya redio na kwamba amepata tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi kutokana na kazi zake ikiwemo ya kuwajengea uwezo wanawake ya kujiamini.

“Nimekuwa natumia muda wangu mwingi kuzungumza na kuwapa moyo wajane kwamba wanaweza kufanya mambo makubwa pamoja na hali wanayokabiliana nayo. Kwa hiyo nawahamasisha wasijisikie wanyonge wasimame na wafanye mambo makubwa na wengi wanaelewa somo na maisha yanasonga mbele bila wasiwasi,” alisema Angella.

By Jamhuri