Ndugu Rais, Malcolm X, mwanaharakati wa haki za weusi huko Marekani alipata kusema: “Nitaufuata ukweli bila kujali nani anausema. Nitafuata haki bila kujali inampendelea nani au ipo dhidi ya nani.” 

Na kwa sababu hii, baba ninasema kwa sauti kubwa kuwa pamoja na kwamba kila raia ana wajibu wa kuhakikisha amani ya kweli inatamalaki katika nchi yetu, lakini katika hili wewe baba unayo nafasi ya kipekee.

Una nafasi ya kipekee kwa sababu wewe ndiye ambaye umeshika makali ya upanga. Mwaka huu 2020 ni mwaka unaohitaji uamuzi sahihi.

Baba, wananchi wameshuhudia unyama wa kutisha sana ukitendwa na baadhi ya marais katika nchi zao, hasa za Kiafrika, kutokana na wao kukiuka maagano na wananchi wao na kuamua kung’ang’ania madarakani, madaraka waliyoyapata kwa mtutu wa bunduki au kwa udanganyifu wa kura au kwa hila nyingine, huku wananchi wakiwa hawawataki! Iko mifano mingi. Katika nchi jirani ya Uganda wakati wa utawala wa Idi Amin Dada ulishuhudiwa mfano huo.

Rais aliweza kuamuru huyu atekwe, huyu alitekwa! Huyu ateswe, huyu aliteswa! Au huyu apotezwe au auawe, amri ilitimizwa! Wako marais walioua raia wao kwa mikono yao wenyewe na kusiwe kitu. Aliposema huyu au hawa wafunguliwe kesi, walifunguliwa kesi yoyote na kuwekwa ndani bila kufuata haki! Wapelelezi na waendesha mashitaka na mawakili wa uongo waliziendesha kesi zao zilizosimamiwa na mahakimu wasiomjua wala kuwa na hofu ya uwepo wa Mwenyezi Mungu!

Kupitia vyombo vya habari, baba nilikwishawahi kukuona kanisani. Kama ulikuwa unafanya ibada, Bwana akutangulie! Lakini wafafanulie wanao neno hili, kuwa: “Kila mamlaka hutoka kwa Mungu.” Haya yaliyoainishwa hapa baba bado ni sawasawa kusema kila mamlaka hutoka kwa Mungu?

Kiliposikika kilio kikuu kilicholeta simanzi kubwa katika nchi yote kuwa kuna wengine wanalalamika na kuna wengine wanaumia, kiliondosha furaha ya uhuru katika vifua vya watu wote wenye mioyo ya nyama. 

Niliwaona wengine wakipiga ishara ya msalaba na wengine wakiugulia kulingana na imani za dini zao. Baba, usikae mbali nao hao wote, bali uwategee sikio lako. Kama hawakuoni kuwa wewe ni faraja kwao, basi wote kwa pamoja tumwombe Muumba wetu ambaye ni mmoja kwetu wote wasituhesabie kuwa sisi ndio watesi wao.

Haya ni maovu yanayoweza kutendwa na shetani akiwatumia wafuasi wake. Lakini baba, tukumbuke kuwa sisi ni wapitaji tu katika hii dunia. Hapa si kwetu. Kwetu ni kule juu aliko baba. Yote tuyafanyao ni ya kitambo tu. Hivyo ni haki, vema na vizuri sana kukuambia kuwa unayo nafasi ya kipekee ya kuleta maridhiano katika nchi hii, hasa wakati huu ambao nchi na wananchi wanaelekea katika Uchaguzi Mkuu.

Kumbuka hali uliyowakuta nayo Watanzania. Walikuwa wanakula na kucheka bila kuwa na hofu katika vifua vyao. Kuyapuuza haya kutatuletea majuto, majuto ambayo hayatatusaidia kitu.

Mema mengi hayatarajiwi katika wakati huu, lakini hofu ya machungu makubwa yanayoweza kutokea kabla na wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi iko juu sana. Ni wewe baba uliye na nafasi ya kipekee kuepusha shari hii. 

Hakuna mwingine mwenye uwezo wa kuepusha ghasia na machafuko katika nchi yetu zaidi yako wewe uliyeshika makali ya upanga. Haki ni lazima ionekane ikitendeka. Maridhiano, kusamehe na kusameheana ndiyo tofauti kubwa aliyopewa mwanadamu na Mwenyezi Mungu kumtofautisha na wanyama na viumbe vyake vingine. 

Kwa kuwa hayo ni mema, basi hayawezi kumpendeza shetani asilani. Na kwa kuwa naye shetani ana kundi lake la watu wanaomsujudia, basi Muumba wetu atuepushe tusije kuhesabiwa kati yao waliojaa kiburi.

Itapendeza na kutufurahisha sana ikiwa tutachaguliwa katika uchaguzi ujao. Tusihangaike kupiga bao, mahesabu yako wazi. Utatukuzwa kwa mema yako. Babu zetu walisema: “Chema chajiuza, kibaya chajitembeza.”

Ndugu Rais, katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa: “Umekuwa ukipokea ushauri kutoka pande nyingi. Huyu akikwambia hivi, unamsikiliza. Na yule akikwambia vile, naye unamsikiliza, bila kujua kuwa miluzi mingi humchanganya mbwa.” 

Matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa umethibitisha yaliyoandikwa kuwa ujuzi ni mwalimu mzuri kuliko elimu. Ushindi wa nguvu hauwezi kuisuluhisha mioyo ya wananchi, bali utazidi kuivimbisha na kutafuta kisasi. Vita ni mbaya kwa aliyeshindwa, maana hupata hasara kubwa. Pia vita ni mbaya kwa anayeshinda, maana huandamwa na kisasi siku zote za maisha yake.

Ilizoeleka katika historia mtawala kuwa na anayemwamini ambaye humtumia kwa kila atakacho kufanya. Tulimwona Idi Amin Dada akiwa na Maliyamungu, Nyerere akiwa na Kawawa, lakini mara zote wakubwa ndio walioonekana kuwaendesha waliokuwa chini yao. Katika hii miaka minne wananchi wameona tofauti.

Ujio wa Bashiru Ally, baba wengine waliona kama Mungu kakutumia msaidizi. Lengo lake Muumba yawepo maridhiano kati ya watu wake. Wasiwepo wanaolalamika na wengine wanaoumia! Bashiru alileta faraja kubwa aliposema atawapeleka viongozi vijana mafunzoni wakafundwe. 

Akataka viongozi wengine nao wajivue uheshimiwa waende vijijini na mashambani wakawaelimishe wananchi miradi hii mingi na mikubwa inayofanywa na serikali ina faida gani kwao?

Ndugu Rais kumbuka baba, uliiambia dunia kuwa Watanzania si wajinga. Waliofungiwa watakapowaambia wananchi wapime mantiki iliyopo katika kujenga treni ya nne kwa gharama kubwa, wakati kwa tatu zilizopo hakuna mzigo wala abiria anayebaki wasije kuitwa wachochezi.

Watataka waeleweshwe busara iliyopo ya kuendelea kununua ndege huku watoto wao waliotakiwa kuandikishwa kuanza shule wakiendelea kurundikwa tu kama mifugo kwa kukosa vyumba vya madarasa na madawati. 

Wanafunzi waliokosa kuingia sekondari kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa wametapakaa kwa maelfu nchi nzima. Wengine wa vyuo vikuu hadi leo haijulikani wanaishije baada ya kupatiwa ridhaa ya mikopo bila kuingiziwa fedha!

Hivi wakihoji kwa nini wasiusimamishe angalau mradi mmoja tu fedha hizo si zingetatua kero zote hizi? Baba wataitwa wachochezi? Kwa nini baba tusijipange kuyatafutia majibu mapema? Tukisubiri kuja kuwaita wachochezi wanaotupa ushauri huu. Wataliliwa na dunia kwa kiwango kilekile alicholiliwa Nelson Mandela na wapigania uhuru wenzake. Inaumiza sana kulazimika kumkumbuka Samwel Doe, Rais aliyekatwa masikio akiwa hai!

By Jamhuri