Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa vita ya ukatili wa kijinsia ni pana sana na imekuwa ikiwaathiri zaidi watoto na wanawake.

Hayo ameyasema leo Julai 14,2023 wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wahariri na waandishi wa vyombo vya habari mbalimbali ambao wapo kwenye timu ya kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia inayosimamiwa na Wizara ya Katiba na Sheria.

Waziri Ndumbaro amesema kuwa vita hiyo ni kubwa sana na imekuwa ikikwamishwa na baadhi ya mifumo kwenye jamii.

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza katika mafunzo hayo.

“Vita hii ni pana na ngumu sana na imekuwa ikiwaathiri sana watoto na wanawake kiasi cha kuingilia haki za watoto na kukosa elimu.

“Hivi karibuni kulikuwa na taarifa za mwanafunzi huko Tunduru kukatishwa masomo na wazazi wake kisha kuozeshwa kinguvu Serikali ikaingilia kati na kusambaratisha ndoa hiyo” amesema Ndumbaro.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kusimamia haki za Watanzania na ameteua wajumbe wa Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha taasisi za Haki Jinai nchini inayoongozwa na Mwenyekiti Jaji Mohamed Othman Chande na Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu Balozi Ombeni Sefue.

Ameongeza kuwa pia wamebaini kuwepo kwa ukatili mkubwa kwa wanawake wanaowania nafasi mbalimbali za za uongozi kwenye vyama vya siasa na kufanyiwa ukatili wa kijinsia wenye lengo la kumdhoofisha na kumkatisha tamaa kuwania uongozi.

“Ukatili wa kijinsia ni uhalifu kama uhalifu mwingine hivyo jambo hili linahitaji ushirikiano ili kulimaliza na. Dio maana tuliunda tume ambayo imebaini changamoto nyingi za ukatili wanazofanyiwa wanawake wanaowania nafasi mbalimbali za uongozi” amesema.

Pia waziri Ndumbaro amewaasa waandishi wa habari kutumia taaluma zao katika kuelimisha jamii ili kusimamia haki.

“Simamieni misingi ya uandishi na utoaji wa taarifa kwa umma ili isije kuwa taarifa zenu badala ya kuonesha ubaya ili kuzuia uendelezwaji wa matukio haya, zikachochea tena ukatiliā€, amesema Ndumbaro.

Baadhi ya wahariri na waandishi wakifuatilia mafunzo hayo.

Pia amewataka wanahabari kujikita kwenye kutoa taarifa zenye mwendelezo wa ushughulikiwaji wa tukio husika kwa lengo la kusaidia wananchi kufahamu hatua zinazochukuliwa hadi kufikia haki ya mhusika.

Wazuru Ndumbaro pia amevitaja vyombo mbalimbali vinavyotumika kumsaidia manusura ikiwemo huduma za usaidizi wa kisheria, simu za dharura, malazi na vituo vya dharura vya hifadhi ya manusura wa ukatili wa kijinsia huku akiwataka wandishi kuzipa umuhimu taarifa hizi katika kurasa za kwanza za machapisho ili kusaidia kujenga ufahamu na uelewa kwa wananchi kuhusu wapi pa kukimbilia kupata msaada kunapotokea changamoto za ukatili wa kijinsia.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Msaada wa Kisheria Ester Msambazi akizungumza katika mafunzo hayo.

Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Msaada wa Kisheria Ester Msambazi, amesema kuwa Wizara imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha mwananchi anapata huduma za kisheria kwa urahisi na kwa gharama nafuu. “Moja ya wadau tunaofanya kazi nao kwa ukaribu ni tasnia ya Habari kwa kuwa wana mchango mkubwa sana katika kuwafikia wananchi kupitia vipindi vya redio, televisheni, magazeti na hata njia nyingine wanazozitumia.” amesema.

Ameaema kuwa mafunzo hayo ni awamu ya tatu ambayo yamekuwa Wizara ya Katiba na Sheria na kuwepo kwa mafanikio makubwa kutokana na utendajikazi wa waandishi.

By Jamhuri