Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itazijenga upya Mahakama zote za Zanzibar Unguja na Pemba kwa bajeti ya mwaka wa Fedha, 2023/2024.

Aidha, imeeleza dhamira yake ya kukamilisha miradi yote ya maendeleo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kwa sekta zote zikiwemo, Afya, Elimu, Maji safi, Miundombinu ya barabara, ujenzi wa ofisi zote za Serikali pamoja na Sekta ya michezo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo aliposhuhudia utiwaji wa saini Fedha za mkopo wa shilingi bilioni 470 zilizotolewa na benki ya NBC kwa kushirikiana na Benki ya NMB na Wizara ya Nchini Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Ikulu – Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi amesema hii ni mara ya kwanza kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukopa Fedha kutoka benki za ndani na kuahidi kuzirejesha fedha hizo kwa kipindi kifupi kwani Serikali inauwezo wa kufanya hivyo na sasa inaakiba ya kurejesha gharama nusu za mkopo huo.

Dk. Mwinyi amesema Fedha hizo zimekusudiwa kukamilisha miradi yote ya maendeleo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja wa Fedha 2023/2024.

Amesema, awali Serikali ilitumia dola za kimarekani milioni 100 sawa na shilingi bilioni 230 za Tanzania kwaajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo Fedha za ahuweni ya uviko 19.

Alisema, kupitia Fedha hizo, Serikali ilifanikiwa kujenga skuli za ghorofa na hospitali za wilaya kwa Wilaya zote za Unguja na Pemba.

Rais Dk. Mwinyi ameshukuru benki za NBC na NMB kwa ushirikiano wao wanaoutoa kwa kuungamkono juhudi za Serikali za kuwainarishia wananchi maendeleo.

Aidha, amezitaka benki hizo kuongeza kima kikubwa zaidi kwa kuikopesha Serikali mara baada ya kurejesha mkopo huo.

Rais Dk. Mwinyi ameeleza dhamira ya Serikali kuondosha tatizo la maji Safi na salama kwa maeneo yote ya Unguja na Pemba hasa kwa mikoa ya Kusini na Kaskazini, Pemba ambako alieleza kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji Safi.

Mapema akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Sada Mkuya Salum amesema fedha hizo zitatumika kwa mujibu wa Sheria na taratibu zilizowekwa ili kukamailisha miradi ya maendeleo kwa wakati.

Waliotia saini kwenye hafla hiyo ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dk. Juma Malik Akil, Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC, Theobald Sabi na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NMB, Juma Kimori

By Jamhuri