Ndunguru:Uwekezaji sekta ya madini umekua kwa kasi

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dodoma

Katibu Mkuu Mpya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Adolf Ndunguru amesema Uwekezaji katika Sekta ya Madini umekua kwa kasi ikiwemo kuongezeka kwa mapato ya Serikali yanayotokana na shughuli za madini nchini.

Ndunguru ameyasema hayo Mtumba jijini Dodoma wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi ya Katibu Mkuu baina yake na Katibu Mkuu Kheri Mahimbali ambaye aliteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Madini na kumhamishia TAMISEMI aliyekua Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Adolf Ndunguru.

Ndunguru ameongeza kwamba, sekta ya Madini ni sekta nyeti yenye uwezo mkubwa wa kuchangia uchumi wa Tanzania kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa na kwamba sekta hiyo inatarajia kuchangia asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

‘’Sekta hii ilikua ikichangia asilimia 5 lakini katika robo ya Tatu ya mwaka 2022, imechangia asilimia 9.7. Tumekaribia asilimia 10 fursa za uwekezaji ni nyingi. Una timu nzuri, hii timu ya wizara ndiyo watendaji wakubwa watakaokusaidia. Kwa watumishi wa madini, nimeiacha sekta hii kwenye mikono salama ya Mahimbali, mumpe ushirikiano kama mlivyonipatia mimi,’’ amesisitiza Ndunguru.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amemweleza Katibu Mkuu Ndunguru kuwa Wizara ya Madini inathamini mchango na mawazo yake kutokana na namna alivyosimamia sekta hiyo kwa kipindi cha Mwaka mmoja na mwezi mmoja aliohudumu kama Katibu Mkuu na kwamba mengi yamefanyika katika kipindi chake.

‘’Mengi yamefanyika wakati ukiwa hapa, unapokweda ndiko ambako shughuli za madini zinafanyika kwa kiasi kikubwa, tunategemea kuendelea kushirikiana na wewe, kuyaenzi mazuri yako na tutakupa ushirikiano wetu,’’ amesisitiza Mahimbali.

Naye, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini Augustine Ollal akizungumza kwa niaba ya watumishi amesema mafanikio mengi yametokea ndani ya kipindi cha mwaka na mwezi mmoja ambacho Katibu Mkuu Ndunguru alihudumu Sekta ya Madini na kuongeza kuwa, watendaji na watumishi wa wizara wataendelea kutoa ushirikiano ili kumwezesha Katibu Mkuu Mahimbali kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

‘’ Katibu Mkuu tutajipa nguvu zaidi kufikia maono yako, tunapokosea tusahihishe na yale uliyoyafanya ukiwa Wizara ya Nishati yaongeze zaidi ukiwa hapa madini, sisi tutakupa ushirikiano wetu wote,’’ amesema Ollal.