Na Magreth Lyimo,WANMM

Kamati za urasimishaji zimeelekezwa kutokuwa miungu watu na badala yake zimetakiwa kusimamia na kuwa kiunganishi kati ya wananchi na wataalamu wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) watakaoenda kutekeleza zoezi la urasimishaji katika Jiji la Dodoma.

Hayo yamebainishwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis G. Mwamfupe wakati akifungua mafunzo kwa Kamati za Urasimishaji kutoka Mitaa ya Bihawana, Mapinduzi A, Mapinduzi B na Mpunguzi katika ukumbi wa Mkandarasi Jijini Dodoma.

Prof. Mwamfupe amesema ‘‘kamati zilizochaguliwa zinapaswa kutoa ushirikiano mkubwa kwa wataalamu wa mradi ili kutimiza malengo yaliyopo kwa kuwa ni viungo kati ya wataalamu na wananchi na sio kwenda na kujifanya miungu watu na kusahau kuwawakilisha wananchi waliowachagua’’.

Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis G. Mwamfupe wakati akifungua mafunzo kwa Kamati za Urasimishaji kutoka Mitaa ya Bihawana, Mapinduzi A, Mapinduzi B na Mpunguzi yaliyoandaliwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika ukumbi wa Mkandarasi, tarehe 4/3/2023 Jijini Dodoma

Ameendelea kusisitiza kuwa, kamati hizo zina jukumu la kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na ni vyema zikashawishi kuondokana na mila potofu hasa kwa wale wanaosema ukipimiwa ardhi inashuka thamani ambapo alisema kuwa hizo ni fikra potofu na zinatakiwa kupingwa kwa sababu unapopimiwa unaongeza thamani na kukupa uhakika wa mipaka yako

‘‘Makazi holela yanawanyima wakazi nchini mwetu kuweza kutumia makazi yao waliyoyajenga kwa shida na kwa kipindi kirefu kama kitu cha kuwasaidia katika mikopo hivyo nchi ikaona kuwa miongoni mwa mambo ya kuwainua wananchi wake ni kutambua makazi yao ili yawe rasmi’’ amesema Prof Mwamfupe.

Diwani wa Mtaa wa Bihawana, Kata ya Mbabala Mhe. Paskazia Mayala aliahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wataalamu lakini pia kutoa elimu zaidi kwa jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na kusema kuwa mradi wa uboreshaji milki za ardhi ni mzuri kwa kuwa hakutakuwa na mtu kuhamishwa ila utapimiwa pale pale ulipo.

Mwakilishi wa wananchi katika Kamati ya Urasimishaji Bw. David Marco ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Mapinduzi B Kata ya Ng’ong’onha ameeleza kuwa, wananchi wa mtaa wake wamepokea mradi huu kwa kuwa wataalamu walitoa elimu sana wakati wa zoezi la uhamasishaji na wananchi wameona watanufaika kwa kupimiwa viwanja vyao pasipo kuhamishwa.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mwanadamizi kutoka Wizara ya Ardhi ambae pia ni Mtaalamu wa masuala ya Jamii katika Mradi Tumaini Setumbi amesema kuwa Mradi huo utahakikisha haki zinasimamiwa kwa makundi yote maalumu ya kinamama, Wazee, Watoto na watu wenye ulemavu ili waweze kupata haki zao za umiliki wa Ardhi sawa na watu wengine.

“Idadi ya Wanawake wanaomiliki Ardhi ni ndogo ukilinganisha na Wanaume hivyo moja kati ya kazi yetu ni kuielimisha jamii kuwa Wanawake pia wanayo haki sawa na Wanaume katika kumiliki Ardhi” ameongeza Setumbi.

Mafunzo hayo kwa kamati ni mwendelezo wa mafunzo ambayo yanatolewa na Mradi ili kupata uelewa wa pamoja kati ya wataalamu wa mradi pamoja na Kamati za urasimishaji zitakazo saidia kuwa kiungo kati ya wananchi na wataalamu lengo likiwa ni kuhakikisha ushirikishwaji wa mwananchi katika hatua zote za mradi unasimamiwa kwa karibu.

By Jamhuri