DC Namtumbo aonya watendaji wasio waaminifu

Na Cresensia Kapinga,JamhuriMedia,Namtumbo

Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Malenya Ngolo amesema kuwa usimamizi mbovu wa vyanzo vya mapato kutoka kwa baadhi ya madiwani pamoja na wataalam,umesababisha baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo kuhujumu mapato jambo ambalo limesababisha kutoendelea kwa miradi na madiwani kukosa stahiki zao.

Hayo ameyasema jana kwenye kikao cha Baraza la Madiwani lililofanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo wakati akihutubia baraza hilo kwa mara ya kwanza toka ateuliwe na Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Samia suluhu Hassan.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo wakiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani cha robo ya pili cha kawaida kilichofanyika Jana kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo

Amesema kuwa kutokana na halmashauri hiyo kuwa na hali mbaya kwenye ukusanyaji wa vyanzo mapato amesema ni jukumu la kila mmoja kusimamia kwenye eneo lake na sio jukumu la mkuu wa Wilaya na kamati yake ya ulinzi na usalama.

Ngolo amesema kuwa wakusanyaji wa mapato waliopo maeneo mbalimbali wameharibu mawasiliano ya vifaa vya kukusanyia mapato (POS) na kupelekea mahesabu hayo kutoingizwa kama mapato ya halmashauri huku vitendea kazi hivyo hufanywa kwa maelewano kati ya baadhi ya madiwani na watendaji wa vijiji na kata na wale wanaokusanya mapato magetini na maeneo mengine.

“Kwa hili la ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri yetu kuwa na hali mbaya niwaambie ukweli mmenisikitisha sana mimi pamoja na wananchi, nawaagiza viongozi wenzangu madiwani, mkurugenzi, wataalam pamoja na watendaji tuchukuwe hatua za kusimamia makusanyo ya mapato na kwa wale watakaobainika kwenda kinyume na maagizo haya wachukuliwe hatua za kisheria mara moja ikiwemo kuwasimamisha kazi bila ya kuwaonea haya.”amesema mkuu huyo wa Wilaya.

Aidha amewaagiza viongozi kujitathimini namna ya utendaji wao wa kufanya kazi lakini pia kufanya mapitio ya kodi,ada,tozo, ushuru pamoja na kubuni na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza wigo wa mapato sambamba na kuimarisha mfumo wa ukusanyaji na kuhakikisha makusanyo yote yanakusanywa kwa kupitia mfumo wa kielektroniki ili kudhibiti upotevu wa mapato .

Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili.