Na Steven Augustino,JamhuriMedia,Tunduru

Mahakama ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma imemhukumu mkazi wa kijiji cha Namiungo,Mohamed Saudi Ngwelekwe (25) kutumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kumlawiti mtoto wake mwenye umri wa miaka 4 .

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Tunduru Honorius Kando baada ya mlalamikiwa huyo kukiri kumfanyia kitendo hicho mtoto wake (jina linahifadhiwa (4) pamoja na kukiri kosa dogo la kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake.

Akifafanua adhabu hiyo Hakimu Kando amesema kuwa mahakama yake imechukua maamuzi ya kumuhukumu kutumikia adhabu hiyo baada ya kujiridhisha bila kutia mashaka kuwa mtuhumiwa huyo alifanya kosa hilo na ndiyo maana amekubali.

Amesema kitendo kilichofanywa na mtuhumiwa huyo kimemfanya mlalamikaji huyo ambaye yupo chini ya miaka 18 ambapo kifungo kilicho tajwa kwenye shauri hilo kinaekeleza mtuhumiwa kupewa adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Awali wakimsomea shitaka hilo mwendesha Mashtaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Inspekta Stephen Msongaleli na Inspekta Machiya Ernest Nangi mbele ya Hakimu Kando walisema kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo Februari 24,2023 .

Walisema katika tukio hilo mtuhumiwa huyo alikabidhiwa mtoto huyo na mtalaka wake Sofia Mkwanda mwezi wa saba mwaka 2022 baada ya kufikia makubaliano kuwa atamtunza.

Walisema katika shauri hilo namba 50/2023 mtuhumiwa huyo ambaye alishtakiwa kwa makosa mawili kosa la kwanza lilikuwa ni la kulawiti kinyume na kifungu cha Sheria namba 254 (1)(a) cha sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejea mwaka 2022.

Kwa mujibu wa Waendesha Mashitaka hao kosa la pili lilikuwa ni la kujeruhi kinyume na kifungu cha sheria namba 225 cha sharia ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyo fanyiwa marejea mwaka 2022.

Baada ya mahakama hiyo kumtia hatiani mtuhumiwa huyo, waendesha mashitaka hao kwa pamoja waliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa ili liwe fundisho kwa watu wengine ambao wamekuwa na tabia za aina hiyo.

Akitoa utetezi mbele ya hakimu huyo, aliiomba mahakama hiyo kumpatia adhabu ndogo kwa vile hilo ni kosa lake la kwanza,anategemewa na wazazi na mtoto huyo.

Akizungumzia tukio hilo nje ya mahakama,babu wa mtoto huyo upande wa kiume Saudi Gwelekwe amesema kuwa tukio hilo ni la kifedheha kwa ukoo wao hivyo adhabu iliyotolewa mahakamani hapo ni stahiki yake.

Amesema mtuhumiwa ambaye alizaliwa mwaka 1998 alilelewa katika kituo cha kulelea watoto yatima kilichopo katika Kanisa la Bibilia Tanzania kituo cha Mbesa Missioni baada ya mama yake mzazi kufariki muda mfupi baada ya kujifungua.

Amesema akiwa huko alikaa miaka 4 ambapo alienda kumchukua na baada kulelewa akiwa nyumbani hadi alipofikia umri wa kujitambua na kuhamia kwenye mji wake akiwa mtu mwema tu ila haelewi tabia hizo za kinyama alijifunzia wapi.

Bibi wa mtoto huyo upande wa kike Stawa Selemani amesema kuwa mjukuu wake huyo alikutwa akiwa na vidonda sehemu mbalimbali za mwili wake hali ambayo iliwafanya wampeleke hospitali kwa ajili ya matibabu.

Amesema wakiwa huko ndipo akagundua mtoto huyo alikuwa anajisaidia bila utaratibu hali iliyoonesha aliharibiwa sana na walipo mhoji alieleza kuwa amekuwa akiingiliwa na baba yake kipindi kirefu na kwamba awali alianza kumchezea kwa kutumia vidole hali ambayo iliwafanya waende kuripoti kituo cha Polisi kwa ajili ya hatua za kisheria.

By Jamhuri